Mithali 11

1 Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.

2 Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.

3 Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.

4 Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti.

5 Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.

6 Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe.

7 Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea; Na matumaini ya uovu huangamia.

8 Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake.

9 Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa.

10 Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele.

11 Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.

12 Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.

13 Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.

14 Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.

15 Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama.

16 Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote.

17 Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake.

18 Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika.

19 Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe.

20 Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa Bwana; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.

21 Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazao wa wenye haki wataokoka.

22 Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili.

23 Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu.

24 Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.

25 Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.

26 Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake.

27 Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia.

28 Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani.

29 Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.

30 Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu.

31 Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?