Roho Zenye Tamaa

KESHA LA ASUBUHI

Ijumaa: Aprili 7; 2017

SOMO: ROHO ZENYE TAMAA

Wakayasahau matendo Yake kwa haraka, Hawakulingojea shauri lake. Bali walitamani sana jangwani, Wakamjaribu Mungu nyikani. Akawapa walichokitaka, Akawakondesha roho zao”  Zaburi 106:13-15.

Wakati wowote ambapo tamaa yao ya chakula ilizuiwa, wana wa Israeli hawakuridhika, na wakanung’unika na kumlalamikia Musa na Haruni, na dhidi ya Mungu.

Mungu aliwapatia watu hawa kile ambacho hakikuwa bora kwao, kwa sababu walidumu kukitamani; wasingeweza kuridhika na vitu vile ambavyo vingekuwa faida kwao.Shauku zao za uasi zilitoshelezwa, lakini waliachwa wakabiliane na matokeo husika.Walikula bila kujizuia, na ulafi wao uliadhibiwa haraka….

Idadi kubwa ya watu walikufa kutokana na homa kali, wakati ambapo wale waliokuwa na hatia kubwa kuliko wote miongoni mwao waliadhibiwa mara tu baada ya kuonja chakula ambacho walikuwa wamekitamani sana.

Mungu angeliweza kuwapatia nyama kirahisi kama ilivyokuwa kwa ile Mana, lakini kizuizi kiliwekwa kwao kwa ajili ya ustawi wa afya zao.

Lilikuwa kusudi Lake kuwapatia chakula bora kilichofaa kwa ajili ya mahitaji yao kuliko chakula kile chenye magonjwa ambacho wengi walikuwa wamekizoea huko Misri.

Shauku zao zilizopotoka zilipaswa kuletwa katika hali ya kiafya zaidi, ili waweze kufurahia chakula ambacho hapo awali alipewa mwanadamu—mazao ya nchi, ambayo Mungu alimpatia Adamu na Hawa katika Bustani ya Edeni. Ilikuwa ni kwa sababu hii ndiyo maana wana wa Israeli walikuwa wamezuiwa kutumia chakula cha wanyama kwa kiwango kikubwa.

Shetani aliwajaribu kupuuzia katazo hili kwamba lilikuwa la uonevu na ukatili.

Aliwafanya watamani vitu vilivyokatazwa, kwa sababu aliona kwamba uendekezaji wa tamaa ya chakula isiyodhibitiwa ungesababisha tamaa ya anasa, na kwa njia hii watu wangeletwa kirahisi chini ya utawala wake.

Mwanzilishi wa magonjwa na taabu atawashambulia wanadamu katika maeneo yale ambayo anaweza kujipatia fursa kubwa zaidi.

Kupitia majaribu yaliyoelekezwa kwenye tamaa ya chakula, kwa kiwango kikubwa, amewaongoza wanadamu kuingia dhambini tangu pale alipomshawishi Hawa kula lile tunda lililokatazwa.Ni kupitia njia hiihii ndivyo alivyowaongoza watu wa Israeli kumnung’unikia Mungu.

Kutokuwa na kiasi katika kula na kunywa, ikisababisha kama ifanyavyo, katika kuendekeza tamaa za mwili, huandaa njia kwa ajili ya wanadamu kupuuzia wajibu wote wa kimaadili.Wanashambuliwa na majaribu, huwa na uwezo mdogo wa kukabiliana nayo na kuyashinda.

REHEMA ZA BWANA NI MPYA KILA SIKU ASUBUHI : MAOMBOLEZO 3: 22-23