Mlevi mno kuliko kutojali

KESHA LA ASUBUHI

Jumatano: Aprili 05/2017

SOMO: MLEVI MNO KIASI CHA KUTOJALI

“Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima” { Mithali 20:1.}
Nadabu na Abihu kamwe wasingetenda dhambi hiyo ya kufisha kama wasingekuwa kwanza wamelewa kwa kutumia pombe bila kujitawala.

Walielewa kuwa maandalizi makini na yenye taadhima ya hali ya juu kabisa yalihitajika kabla ya kujihudhurisha katika patakatifu, ambapo Uwepo wa Mungu ulijidhihirisha; lakini kwa sababu ya kutokuwa na kiasi kukosa kujitawala, walichanganyikiwa na utambuzi wao wa kimaadili ukahafifika kiasi kwamba hawakuweza kupambanua tofauti kati ya vitu vitakatifu na vile vya kawaida.

Kwa Haruni na wanawe wengine waliosalimika, onyo lilitolewa: “Usinywe divai wala kileo chochote,… kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi.”

Matumizi ya vinywaji vya kulevya vina athari ya kuudhoofisha mwili, kutatanisha akili, na kushusha viwango vya kimaadili. Huwazuia watu wasitambue kicho kwa mambo matakatifu au uwezo wenye mamlaka wa maagizo ya Mungu.

Wote walioshikilia nyadhifa takatifu za madaraka walipaswa kuwa watu wanaofuata kanuni za kiasi kwa ukamilifu kabisa, ili akili zao ziweze kuwa makini kutofautisha kati ya jema na baya, ili waweze kuwa na uthabiti wa kanuni, na hekima ya kusimamia haki na kuonesha rehema._Wajibu huohuo uko juu ya kila mfuasi wa Kristo….

Kanisa la Kristo katika vizazi vyote limepewa onyo la dhati na la kuogofya sana: “Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi” (1 Kor. 3:17).

Suala la wana wa Haruni limewekwa kwenye kumbukumbu kwa ajili ya faida ya watu wa Mungu, na linapaswa kuwafundisha wale wanaojiandaa kwa ajili ya marejeo ya pili ya Kristo, kwamba uendekezaji wa uchu potofu wa chakula huharibu hisia makini za roho, na kwa hiyo huathiri nguvu za kufanya maamuzi ambazo Mungu amempatia mwanadamu, kiasi kwamba mambo ya kiroho na matakatifu hukosa utakatifu wao.

Uasi huonekana kuwa jambo la kuvutia, badala ya kuwa dhambi ichukizayo mno kupita kiasi
REHEMA ZA BWANA NI MPYA KILA SIKU ASUBUHI, MAOMBOLEZO 3: 22-23