Moto wa Kigeni

KESHA LA ASUBUHI

Jumanne: 04/04/2017

SOMO: MOTO WA KIGENI

Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya Bwana, ambao yeye hakuwaagizaWalawi 10:1.

Baada ya Musa na Haruni, Nadabu na Abihu walikuwa na cheo cha juu kabisa katika Israeli. Walikuwa wameheshimiwa na Bwana kwa namna ya pekee, kwa kuruhusiwa pamoja na wale wazee sabini kuutazama utukufu Wake pale Mlimani.

Lakini hilo lisingekuwa sababu ya uasi wao kupewa udhuru au kupuuzwa kwamba hauna uzito.

Fursa zote hizi zilifanya dhambi yao kuwa mbaya zaidi. Kwa sababu wanadamu wamepokea nuru kubwa, kwa sababu kama ilivyokuwa kwa wale wakuu wa Israeli, wamepanda mlimani, na wamepewa fursa ya kufanya ushirika pamoja na Mungu, na kukaa katika nuru ya utukufu Wake, hebu wasijidanganye kwamba baada ya hapo wanaweza kutenda dhambi bila hofu ya kuadhibiwa, kwamba kwa sababu wameheshimiwa sana kiasi hicho, Mungu hatakuwa makini sana kuadhibu udhalimu wao. Huu ni udanganyifu wa kufisha.

Nuru na fursa kuu zilizoletwa kwao hudai matokeo ya uadilifu na utakatifu unaolingana na nuru hiyo waliyopewa. Chochote ambacho ni pungufu ya hili, Mungu hawezi kukikubali.Baraka au fursa kuu hazipaswi kutuliwaza kuwa tuko salama au kutukosesha uangalifu.Hazipaswi kutupatia idhini ya dhambi au kumfanya mpokeaji ajisikie kwamba Mungu hatashughulika naye kwa umakini kamili….

Nadabu na Abihu katika ujana wao hawakuwa wamefunzwa kuwa na mazoea ya kujitawala…. Mazoea ya kuendekeza nafsi katika tamaa na anasa, yaliyokuzwa kwa muda mrefu, yalipata nafasi ya kuwatawala kiasi kwamba hata wajibu wa dhamana hiyo takatifu sana haikuwa na uwezo wa kuyavunja.

Hawakuwa wamejifunza kuyaheshimu mamlaka ya baba yao, na hawakutambua ulazima wa utii kamili kwa maagizo ya Mungu.

Kosa la Haruni la kuwadekeza wanawe liliwaandaa kuwa walengwa wa hukumu za Mungu. Mungu alikusudia kuwafundisha watu kwamba lazima wamkaribie kwa ustahivu na kicho, na katika namna aliyoichagua Yeye Mwenyewe. Hawezi kukubali utii nusu.

Haikutosha kwamba katika wakati huu makini wa ibada karibu kila kitu kilifanywa kama alivyokuwa ameagiza….

Hebu mtu yeyote asijidanganye mwenyewe kwa imani kuwa sehemu ya amri za Mungu si muhimu, au kwamba atakubali mbadala wa kile ambacho ameagiza.

REHEMA ZA BWANA NI MPYA KILA SIKU ASUBUHI: Maombolezo 3:22-23