2-4-17: Kwa Walio Uhamishoni

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA

http://tgvs.org/archives/2460

  • Robo hii: Lisha Kondoo Zangu
  • Wiki hii: Urithi Usioharibika (2/13)
  • Jamii: Kila Jioni

Fungu La Kukariri (1 Petro 1:22)

Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo.

 

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu. Jina Lako litukuzwe milele. Asante Bwana kwa nafasi nyingine ya uhai. Asante kwa zawadi ya Neno Lako. Kabala ya kuanza kipindi hiki, tunaalika uwepo Wako, Bwana. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Bariki kila mmoja Bwana. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

Jumapili: (2/4/17)

KWA WALIO UHAMISHONI

SWALI #1: Soma 1 Petro 1:1. Tunaweza kujifunza kitu gani kutoka katika aya hii moja ambacho kitatusaidia kupata sehemu ndogo ya muktadha?

1 Petro 1:1

“Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule wa Utawanyiko, wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia”

 

Petro anajitambulisha kwa uwazi. Jina lake ndilo neno la kwanza katika barua hii. Hata hivyo, mara moja anajitambulisha kama “mtume wa Yesu Kristo.” Kwa hiyo, kama vile Paulo alivyofanya mara kwa mara (Wagalatia 1:1, Warumi 1:1, Waefeso 1:1), Petro mara moja anathibitisha “sifa” zake, akisisitiza mwito wake mtakatifu. Alikuwa ni “mtume,” yaani “mtu aliyetumwa,” na aliyemtuma ni Bwana Yesu Kristo.

Petro anatambulisha eneo ambalo barua yake ilielekezwa: Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia, na Bithinia. Haya yote ni maeneo ndani ya Asia Ndogo, karibu sawa na eneo la Uturuki ya leo mashariki ya mlango wa bahari wa Bosporus.

Zipo hoja kuhusu iwapo Petro alikuwa akiandika zaidi kwa waumini wa Kiyahudi au kwa waumini wa-Mataifa. Maneno anayotumia Petro katika 1 Petro 1:1 “Utawanyiko/wageni,” ni maneno ambayo kwa asili yanawahusu Wayahudi waliokuwa wakiishi nje ya Nchi Takatifu katika karne ya kwanza. Maneno kuteuliwa(BHN) na kutakaswa katika 1 Petro 1:2 yanafaa kwa wote Wayahudi na Mataifa. Kuwaeleza wale ambao wako nje ya jumuia kuwa ni “Mataifa” (1 Petro 2:12; 4:3) pia husisitiza tabia ya Kiyahudi ya wale ambao Petro anawaandikia.

Wafasiri wengine wanatoa hoja, kwa kujibu, kwamba kile Petro anachokisema katika 1 Petro 1:18;4:3 kingekuwa sahihi zaidi kusemwa kuhusu waongofu wa Mataifa wanaoingia katika Ukristo kuliko kwa wale wa Kiyahudi. Hata hivyo, je Petro angeweza kweli kuwaandikia Wayahudi kuhusu “mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;”? Au je angeweza kusema kwa wasomaji Wayahudi, “Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali” (1 Petro 4:3)?

Hata hivyo, kilicho cha maana sana kwetu si nani aliandikiwa, bali, kile ambacho ujumbe unasema.


 

MWISHO

(Karibu kwa mjadala/ Nyongeza)