1-4-17: (Urithi Usioharibika)

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA

http://tgvs.org/archives/2454
(a) Robo hii: Kulisha Kondoo
(b) Wiki hii: Urithi Usioharibika (2/13)
(c) Jamii: Kila Jioni

Fungu La Kukariri (1 Petro 1:22)

“Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo”

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu. Jina Lako litukuzwe milele. Asante Bwana kwa nafasi nyingine ya uhai. Asante kwa zawadi ya Neno Lako. Kabala ya kuanza kipindi hiki, tunaalika uwepo Wako, Bwana. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Bariki kila mmoja Bwana. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

Jumamosi: (1/4/17)

UTANGULIZI: (Urithi Usioharibika)

Kila wakati mtu anapojifunza Biblia, akizingatia kitabu kimoja au hata sehemu moja ya kitabu, maswali machache yangehitajika kujibiwa, kama ingewezekana.

Mosi, ingekuwa vyema kuelewa hadhira iliyokusudiwa. Pili, huenda muhimu zaidi, ingekuwa vyema kuelewa kuwa sababu hasa ya maandiko haya ilikuwa ni nini. Kulikuwako na suala gani hasa (kama lipo) ambalo mwandishi alikuwa anataka kulizungumzia (kama vile Paulo anavyoandika kwa Wagalatia kuhusu makosa ya kiteolojia yaliyokuwa yanafundishwa kuhusu wokovu na sheria)? Kama tujuavyo, Sehemu kubwa ya Agano Jipya iliandikwa kama nyaraka, au barua, na watu kwa kawaida wanaandika kwa kusudi la kupeleka ujumbe mahususi kwa wapokeaji wake.

Kwa maneno mengine, tunaposoma kitabu cha Petro, ingekuwa vyema kufahamu, kwa kadiri iwezekanavyo, muktadha wa kihistoria wa barua yake. Alikuwa akisema kitu gani, na kwa nini? Na kwa kweli, muhimu kuliko yote: Ni ujumbe gani tunaweza (sisi ambao, kwa uvuvio, uliandikwa kwetu pia) kupata kutoka kwake?

Na kama ambavyo tutaona punde, hata katika aya chache za mwanzo, Petro ana kweli nyingi muhimu za kudhihirisha kwetu leo, tuliotengwa na karne nyingi kutoka wakati alipoandika.
SOMA MAFUNGU YAFUATAYO KWA AJILI YA SOMO LA JUMA HILI:

1 Petro 1:1, 2;

1 Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule wa Utawanyiko, wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia; 2 kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani na ziongezwe kwenu.

Yohana 3:16;
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele

Ezekieli 33:11,12;
11 Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?

12 Na wewe, mwanadamu, waambie wana wa watu wako, Haki yake mwenye haki haitamwokoa, katika siku ya kukosa kwake; na kwa habari ya uovu wake mtu mwovu, hataanguka kwa ajili ya uovu huo, siku ile atakapoghairi na kuuacha uovu wake; wala yeye aliye mwenye haki hataweza kuishi kwa haki yake, siku ile atakapotenda dhambi.

1 Petro 1:3–21;

3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;

4 tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.

5 Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.

6 Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;

7 ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.

8 Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu,

9 katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu.

10 Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi.

11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.

12 Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia.

13 Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.

14 Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;

15 bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.

17 Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.

18 Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;

19 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.

20 Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu;

21 ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.

22 Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo.

23 Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele.

24 Maana, Mwili wote ni kama majani, Na fahari yake yote ni kama ua la majani. Majani hukauka na ua lake huanguka;

25 Bali Neno la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Mambo ya Walawi 11:44, 45;

44 Kwa kuwa mimi ni Bwana, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi.

45 Kwa kuwa mimi ni Bwana niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu.