20-002: Ulinzi wa Hekima

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

 

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

http://tgvs.org/archives/2443   

 • (a) 20-002: Mithali sura ya 2
 • (b) Jamii: Kitabu cha Mithali
 • (c) Mfululizo: Biblia Sura kwa Sura

 

UFUPISHO WA SURA HII:

 • (a) Wahusika: Mungu, Sulemani, Mwanae.
 • (b) Tabia ya Mungu: Uaminifu, Haki, Hekima
 • (c) Fungu Kuu: Mithali 1:5-7
 • (d) Neno Kuu: Hekima, Dhambi
 • (e) Msisitizo: Hukumu ya Bwana (2:8, 21-22)

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu. Jina Lako litukuzwe milele. Asante Bwana kwa nafasi nyingine ya uhai. Asante kwa zawadi ya Neno Lako. Kabala ya kuanza kipindi hiki, tunaalika uwepo Wako, Bwana. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Bariki kila mmoja Bwana. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

ULINZI WA HEKIMA (Mithali 2:1-22)

Muhtasari Wa Mawazo Makuu:

Utangulizi (2:1)

Masharti ya kupata Hekima

 • Lazima tuwe wasikivu (2:1)
 • Lazima tuwe wenye kuitikia (2:2-3)
 • Lazima tuwe wenye kunuia (2:4)

Matokeo ya kupata Hekima

 • Furaha katika Bwana (2:5-8)
 • Ukombozi wa Bwana (2:9-22)

Faida ya kupata Hekima

 • Utambuzi/ Ufahamu (2:9)
 • Furaha (2:10)
 • Uhifadhi (2:11 – 22)

Maswali muhimu katika sura hii

Tufanye nini basi na Mithali hii?

Sauti Ya Injili


 

UTANGULIZI

Mungu wetu ni mwema sana na ametupatia uhuru wa uchaguzi. Kuna ahadi nyingi sana katika maandiko kwa ajili yetu. Lakini pia ili kupata mibaraka fulani maishani mwetu, kuna masharti kadha wa kadha: twapaswa kusikia, kuzingatia, kuitikia, na kunuia kuitii Sauti ya Bwana na maagizo Yake.

Katika Injili ya Yohana 12:47, 48; Kristo Yesu akifundisha, anasema: “47 Na mtu akiyasikia maneno Yangu, asiyashike, Mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. 48 Yeye anikataaye Mimi, asiyeyakubali Maneno Yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.”


 

 

MITHALI SURA YA PILI (2)

1 Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu;

2 Hata ukatega sikio lako kusikia hekima, Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu;

3 Naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu;

4 Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika;

5 Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu.

6 Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani Mwake hutoka maarifa na ufahamu;

7 Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili; Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu;

8 Apate kuyalinda mapito ya hukumu, Na kuhifadhi njia ya watakatifu Wake.

9 Ndipo utakapofahamu haki na hukumu, Na adili, na kila njia njema.

10 Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi.

12 Ili kukuokoa na njia ya uovu, Na watu wanenao yaliyopotoka;

13 Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza;

14 Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu;

15 Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao.

16 Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;

17 Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake.

18 Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu.

19 Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima.

20 Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.

21 Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake.

22 Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang’olewa.