18-3-17 Kazi Ya Roho Mtakatifu

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA

http://tgvs.org/archives/2345
(a) Jumamosi: Machi 18, 2017
(b) Jamii: Kila Jioni
(c) Muundo: Mjadala
(d) Muda: Dakika 10-15

Somo la 12: Machi 18-24, 2017


Kazi Ya Roho Mtakatifu

Fungu la Kukariri:

Warumi 15:13
Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu.
Jumamosi: Machi 18, 2017

UTANGULIZI:

Tunapofikia mwisho wa usomaji wetu robo hii juu ya Roho Mtakatifu na maisha ya kiroho, tutajikita katika kazi moja nyingine muhimu sana ya Roho ambayo bado hatujajifunza.

Yesu alipowatangazia wanafunzi kuwa angelikwenda kwa Baba, aliahidi kuwatumia Roho Mtakatifu. “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina Langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yn. 14:26).

Kulingana na Yesu, Roho Mtakatifu ni parakletos, yaani, “Msaidizi,” au “Mfariji,” au “Mtetezi” anayetuombea. Wakati huohuo Yesu pia alitangaza kazi ambayo Mtetezi huyu angeifanya: Yeye “atauhakikisha” ulimwengu kwa habari ya dhambi na haki na hukumu (Yn. 16:8).

Katika juma letu la mwisho tutajifunza kwa kina zaidi kazi hii maalumu ya Roho Mtakatifu. Sisi pia tutajifunza jinsi kazi hii ya Roho inavyohusishwa vipengele viwili vingine muhimu vya huduma yake kwa ajili yetu: uhakika wetu wa wokovu, na tumaini lenye utukufu linalohimiza maisha yetu kama wanafunzi wa Yesu Kristo.

 

SOMA MAFUNGU YAFUATAYO KWA AJILI YA SOMO LA JUMA HILI:

Yohana 16:8-11;
8 Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.
9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini Mimi;
10 kwa habari ya haki, kwa sababu Mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena;
11 kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.

Warumi 5:10;
Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.

Waebrania 4:15, 16;
15 Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali Yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.
16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

1 Petro 5:8, 9;
8 Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.
9 Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.

1 Yohana 5:12, 13;
12 Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.
13 Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.

Zaburi 31:24.
Iweni hodari, mpige moyo konde, Ninyi nyote mnaomngoja Bwana.