19-133: Ndugu wakae Pamoja, kwa Umoja.

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

 

TGV BIBLIA KUSOMA MPANGO

 

MUHTASARI WA SURA HII:

 • (a) Wahusika: Bwana, watu Wake
 • (b) Tabia ya Mungu: Umoja
 • (c) Fungu Kuu: Zaburi 133:1
 • (d) Neno Kuu: Umoja
 • (e) Msisitizo: “Wote wawe na Umoja”

 

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu. Jina Lako litukuzwe milele. Asante Bwana kwa nafasi nyingine ya uhai. Asante kwa zawadi ya Neno Lako. Kabala ya kuanza kipindi hiki, tunaalika uwepo Wako, Bwana. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Bariki kila mmoja Bwana. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

NDUGU WAKAE PAMOJA, KWA UMOJA.

Zaburi 133 (NKJV)

1 Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.

2 Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake.

3 Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele. 


 

 MUHTASARI WA MAWAZO MAKUU

 • (1) Umoja ni nini?
 • (2) Tamko kuhusu Umoja (133:1)
 • (3) Maelezo ya Umoja (133:2 – 3a)
 • (4) Baraka za Umoja (133:3b)
 • (5) Tufanye nini basi na Zaburi hii?

 

UMOJA NI NINI?

UMOJA- ni kuwa kitu kimoja (oneness), maelewano, makubaliano. Umoja ni kuleta pamoja sehemu tofauti tofauti au zilizosambaratika ndani ya muunganiko mzima mmoja. 

Tukumbuke kwamba, mapenzi ya Mungu ni kuwa tuwe na umoja.  Sikiliza ombi la Kristo katika injili ya Yohana 17: 21 “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma”

Lengo la Mungu ni viumbe vyake vote viwe na umoja; Hamu yake ya Umoja ni dhahiri, pia, katika maisha ya watu Wake. Moja ya Tabia ya Mungu ni Umoja, yaani Mungu mmoja katika nafsi tatu: Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.

Tabia yao ni moja, mipango, nia, makusudi, madhumuni, n.k.; ni moja.

Umoja ulionekana dhahiri siku ya Pentekoste (Matendo 2:1) “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

Kanisa ni Umoja katika utofauti, ni ushirika wa Imani, Tumaini na Upendo ambao huunganisha waumini pamoja

Efe. 4:3-5

 • 3 Na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.
 • 4 Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.
 • 5 Bwana mmoja, Imani moja, Ubatizo mmoja.

 

MASWALI MUHIMU KATIKA SURA HII

{Pitia majibu yaliyowekwa hapo chini}

 • (1)   Je, kuna dhambi ya kuepukwa hapa?
 • (2)   Je, kuna dhambi ya kutubu hapa?
 • (3)   Je, kuna ombi la kuomba hapa?
 • (4)   Je, kuna mtazamo wa kuigwa hapa?
 • (5)   Je, kuna agizo au wajibu wa kufanya hapa?
 • (6)   Je, kuna makosa au mapungufu ya kuepukwa hapa?
 • (7)   Je, sura hii inatufundisha nini kuhusu Mungu?
 • (8)   Je, sura hii ina umuhimu gani katika mpango wa wokovu wetu?

 

MAJIBU YA MASWALI MUHIMU

 • (1) Utengano, ugomvi
 • (2) Kutoelewana,  malumbano, magomvi, uhasama; mgogoro, ugomvi, msuguano, n.k.
 • (3) Abramu (Mwanzo 13:8)
 • (4) Tuwie mamoja (Wafilipi 2:2)
 • (5) N/a
 • (6) Umoja Haramu (cf. Ufunuo 13; 17)
 • (7) Msingi wa Umoja wa kweli hutegemea Umoja na Mungu
 • (8) Lazima tuwe na Umoja katika Kristo Yesu.

ANGALIZO: Umoja haramu ni umoja wenye mtazamao/ malengo/ nia ya kuvunja Amri za Mungu. Kwa mfano;  Ufunuo 17:13 “Hawa wana shauri moja, nao wampa yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.”

 

MAONI YA ZIADA

Kuwa mmoja katika Kristo ni kufa, kuzikwa na kufufuka pamoja Naye. Kwa maneno mengine, tunapokea maisha mapya kabisa. Tunapokuwa na umoja katika Kristo, maisha yetu yanabadilishwa kabisa.  Utu wetu wa kale unazikwa kabisa, badala yake tunavishwa utu upya ndani ya Kristo Yesu.

Tutakuwa chini ya Ongozi wa Roho Mtakatifu. Yeye atatuongoza sisi kwa Kristo. Yeye (Roho Mtakatifu) “anatuongoza kwa Yesu, anayesamehe dhambi zetu na kututakasa. Hata hivyo, Roho wa Mungu anaitwa pia “Mtakatifu.” Hii ina maana kuwa anaichukia dhambi. Lakini hufurahi tunapokuwa watiifu kwa Mungu katika mambo yote na hufikiri na kuzungumza mambo ambayo ni safi na matakatifu. Kwa upande mwingine, hii pia humaanisha kuwa anahuzunishwa tunapoendekeza chochote ambacho hakifai kwa wito wetu wa kiungu. Kusudi lolote kwa upande wetu wa kung’ang’ania dhambi au kuhafifisha ubaya wa dhambi humhuzunisha Yeye. Kumhuzunisha Roho Mtakatifu ni jambo ovu na hatari kabisa.” (SS Lesson -1Q 2017, Jumatatu – Machi 13, 2017)


 

TUFANYE NINI BASI NA SURA HII?

SWALI:  Je, kuna kitu hapa kutekeleza kwa maisha yangu?

Ndiyo, sisi kama watu wa Mungu lazima tuwe na umoja; lakini  ni jinsi gani umoja huu umoja utadhihirishwa?

 

Angalia tabia/ maelezo yafuatayo ya Umoja ambayo lazima yadhihirishwe miongoni mwa watu wa Mungu

 • (1) Kushirikiana  (Matendo 4:32)
 • (2) Kutoa usaidizi (Yoshua 22:3)
 • (3) Kushirikiana katika matatizo (Wafilipi 4:14)
 • (4) Kuishi kwa maelewano (Zaburi 133:1)
 • (5) Umoja katika malengo (Wafilipi 1:27; Mt 18:19-20)
 • (6) Umoja: Nia moja na shauri moja (1 Wakorintho 1:10)
 • (7) Umoja: Kuabudu pamoja (Rum 15:5-6)
 • (8) Kujifunga mmoja kwa mwingine [commitment] (1 Samweli 18:1-4; Ruthu 1:16-17; 1Wathesalonike 2:8)

 

Matendo 4:32

Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika.

Yoshua 22:3

Hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika mausia ya amri ya Bwana, Mungu wenu.

Php 4:14

Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu.

Ps 133:1

Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.

Php 1:27;

Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili

1 Wakorintho 1:10;

Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja

Rum 15:5-6

5 Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu;

6 Ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

1 Wathesalonike 2:8

Vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.


 

NUKUU YA ROHO YA UNABII.

Siri ya Umoja wa familia — ” Chanzo cha mgawanyiko na ugomvi katika familia na katika Kanisa ni utenganisho kutoka kwa Kristo. Kumkaribia Kristo ni kukaribiana sisi kwa sisi. Siri ya Umoja wa kweli katika Kanisa na katika familia si diplomasia, si usimamizi, si juhudi fulani ya kutatua/ kushinda matatizo — ingawa kutakuwa na mengi ya haya kufanywa — lakini Umoja na Kristo. ” {Adventist Home, 179.1}

 

SAUTI YA INJILI

Kusikiliza sauti ya Mungu ikinena nasi tunafunga kipindi hiki:

 

Yohana 17:21 – 23  (Ombi la Kristo)

21 Wote wawe na umoja; kama Wewe, Baba, ulivyo ndani Yangu, nami ndani Yako; hao nao wawe ndani Yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba Wewe ndiwe uliyenituma.

22 Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama Sisi tulivyo umoja.

23 Mimi ndani yao, nawe ndani Yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa Ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda Mimi. 


 

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu mpendwa, tunashukuru kwa tafakari ya Neno Lako katika sura hii. Twaomba Roho Wako aendelee kutufundisha sura hii tena na tena. Tusamehe tuachane na dhambi zilizotajwa katika fundisho la Zaburi hii.

Tukumbushe kusameheana, kumwangalia Kristo daima, na kugundua mapenzi Yako katika maisha yetu. Tukumbushe kupendana daima, na kuwa na Umoja wa kweli. Tukamilishe katika umoja (Yoh 17:23) ndipo tutakuwa kama mtunga Zaburi akisema: “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja”

Asante Bwana kwa ombi hili fupi. Tumeomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo, aliye Bwana na Mkombozi wetu, Amina!


 

 

The Gospel’s Voice © 2017