Mrudishie Mungu Kilicho Chake

Mrudishie Mungu Kilicho Chake

  • Jumanne: 2/28/17
  • Mwl. Peter Marwa

Mwanzo 28:22.

  • Na jiwe hili nililolisimisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.

Kulingana na desturi ya kuadhimisha matukio ya muhimu, Yakobo aliweka kumbukumbu ya rehema ya Mungu, ili wakati wowote apitapo kwenye njia hiyo apate kukawia kidogo kwenye kituo hiki kitakatifu ili amwabudu Bwana… Akiwa na shukrani nyingi alikariri ahadi kwamba Mungu angekuwa pamoja naye; kisha akafanya agano takatifu, “Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.”

Yakobo hakuwa hapa kwa ajili ya kuwekeana masharti na Mungu. Bwana alikuwa amekwisha muahidi mafanikio, na agano hili lilikuwa ni mbubujiko wa moyo uliojawa na shukrani kutokana na uhakika wa upendo na rehema za Mungu. Yakobo alijisikia kwamba Mungu alikuwa na madai kwake ambayo ilikuwa ni lazima kwa Yakobo kuyatambua na kwamba ishara maalumu za fadhila za Mungu ambazo alipewa zilihitaji mrejesho. Ndivyo kila baraka ambayo tunapewa zinavyotutaka tuoneshe mwitikio kwake aliye Chanzo cha rehema zote. Inampasa Mkristo apitie tena mara kwa mara maisha yake yaliyopita na akumbukie kwa shukrani namna ambavyo Mungu amefanya ukombozi wa thamani kwa ajili yake, akimuunga mkono kwenye mitihani ya maisha, akimfungulia njia mbele zake wakati kila upande ulipoonekana kuwa na giza na wenye kutisha, akimchangamsha alipokaribia kuzimia. Inampasa awatambue wote kama vithibitisho vya ulinzi wa malaika wa mbinguni. Kwa kutazama baraka hizi zisizohesabika, yapasa aulize mara kwa mara, akiwa na moyo wa unyenyekevu na wenye shukrani, “Nimrudishie Bwana nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea?” (Zaburi 116:12).

Muda wetu, talanta zetu, mali tulizonazo, yapasa vitolewe kwake yeye ambaye ametupatia baraka hizi kwa kutuamini. Wakati wowote ukombozi wa pekee unapofanywa kwa niaba yetu, au pale tunapopewa fadhila mpya ambazo hatukuzitegemea, inatupasa tutambue wema wa Mungu, siyo tu kwa kuonesha shukrani zetu kwa maneno, lakini, kwa zawadi na matoleo kwa ajili ya kazi yake, kama Yakobo. Tunapodumu kuendelea kupokea baraka za Mungu, vivyo hivyo inatupasa kudumu katika kutoa.