2/27/17: Roho Mtakatifu Hutuunganisha Kupitia Ubatizo

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA

FUNGU LA KUKARIRI

Waefeso 4:3-5

3 Na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. 4 Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. 5 Bwana mmoja, Imani moja, Ubatizo mmoja.

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu. Jina Lako litukuzwe milele. Asante Bwana kwa nafasi nyingine ya uhai. Asante kwa zawadi ya Neno Lako. Kabala ya kuanza kipindi hiki, tunaalika uwepo Wako, Bwana. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Bariki kila mmoja Bwana. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

Somo la Leo:

ROHO MTAKATIFU HUTUUNGANISHA KUPITIA UBATIZO

 

SWALI # 1: Ni kwa namna gani ubatizo hutuunganisha sisi pamoja na Kristo na pia pamoja na Roho?

 • 1 Wakorintho 12:13.
 • Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

 

Aya ya kwanza inasomeka hivi:

 • “Ni Roho Mtakatifu ndiye anayetuunganisha katika mwili wa waumini. Kuingia hadharani katika ufalme wa Kristo wa kiroho hufanyika kwa njia ya ubatizo. Tunabatizwa na kuingia katika mwili maalumu wa kanisa. Kwa hiyo, ubatizo una vipengele dhahiri vya ushirika wa pamoja na matokeo muhimu ya ushirika wa pamoja. Kama wafuasi wa Kristo, hatuwezi kuishi kwa ajili tu ya nafsi zetu sisi wenyewe. Sote tunahitaji kutegemezwa, hamasa, na msaada kutoka kwa wengine. Na kwa hakika hatuwezi kutimiza utume wa kiungu peke yetu. Hiyo ndiyo sababu Mungu amelianzisha kanisa. Kumfuata Kristo, humaanisha kumfuata Yeye katika ushirika wa waumini wengine. Kwa hiyo ubatizo na kanisa vina vitu vinavyoonekana wazi vinavyosaidia kuvikamilisha.”

 

SWALI # 2: Ni jambo gani linaloashiriwa kupitia ubatizo wa Biblia?

1Pet 3:21

 • Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo

Warumi 6:3-7

 • 3 Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?
 • 4 Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.
 • 5 Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;
 • 6 Mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;
 • 7 Kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.

 

Maelezo ya ziada kutoka kwenye Lesoni ya leo:

 • “Tendo la kuzikwa pamoja na Yesu Kristo kupitia ubatizo katika mauti kwenye kaburi la maji na kufufuliwa katika maisha mapya katika ushirika pamoja na Yesu Bwana na Mwokozi wetu huwakilisha usulubishwaji wa maisha ya zamani na maungamo ya hadharani ya kumkubali Kristo kama Mwokozi wetu.”
 • “Ubatizo ni tamko la dhati la kuukana ulimwengu. Kwa tamko hilo la imani, nafsi imekufa katika maisha ya dhambi. Maji humfunika mtaradhia huyo, na mbele ya ulimwengu wote wa mbinguni ahadi ya pamoja hufanywa. Katika jina la Baba, Mwana, na la Roho Mtakatifu, mtu huzamishwa katika kaburi lake la maji, akizikwa pamoja na Kristo katika ubatizo, na kufufuliwa kutoka majini kuingia katika maisha mapya ya uaminifu kwa Mungu.”— Ellen G. White Comments, The SDA Bible Commentary, vol. 6, uk. 1074.
 • “Ubatizo ni hatua nzuri ambayo kwayo wote wanaotamani kutambuliwa kuwa wako chini ya mamlaka ya Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu lazima waridhie. Kwa maneno mengine, ubatizo ni alama ya toba ya kweli, usulubishwaji wa maisha ya zamani, na huashiria kuzaliwa mara ya pili au uongofu. Huhusisha vilevile wajibu wa agano wa pande mbili. Mwumini huahidi kuwa mwaminifu kwa Mungu na kwa amri Zake, na Mungu anatuhakikishia kuwa tunaweza kutegemea msaada Wake wakati wowote tunapouhitaji.”

 

ZINGATIA MABO YAFUATAYO:

 • Ubatizo wa Biblia ni ubatizo wa maji mengi
 • Ubatizo unaashiria kufa, kuzikwa, na kufufuka na Kristo
 • Ubatizo unaashiria kuachana na dunia, dhambi na tamaa zake zote (cf. Somo la Tamaa)
 • Ubatizo ni ishara ya nje ya utakaso kutoka mdhambi hadi mteule
 • Ubatizo ni ishara ya kumvaa Kristo
 • Ubatizo ni ishara ya umoja (cf. Somo la Jana)
 • Lazima kila msafiri wa kwenda mbinguni abatizwe kwa maji (maji mengi) na kwa Roho

 

TUFANYE NINI BASI NA SOMO LA LEO?

 • Tutubu tukabatizwe katika Maji Mengi
 • Tukaoshwe dhambi zetu na kuliita Jina Lake
 • Tuachane na Tamaa za dunia (1 Wakorintho 6:11)
 • Tumvae Kristo
 • Tuzaliwe upya kila dakika (utakaso)
 • Tumruhusu Roho Mtakatifu atuunganishe na Kristo

 

MAFUNGU YA ZIADA

 • Matendo 22:16
  • Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake
 • 1 Wakorintho 6:11;
  • Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu.
 • Tito 3:4-5
  • 4 Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;
  • 5 Si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;
 • Wagalatia 3:27
  • Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.
 • Waefeso 4: 5
  • Bwana mmoja, Imani moja, Ubatizo mmoja.

 

SWALI MUHIMU TUNAPOFUNGA KIPINDI HIKI

 • Je, umefanya uamuzi kwa ajili ya ubatizo wa waaminio?
 • Ikiwa sivyo, nini kinachokuzuia usimfuate Kristo katika ubatizo?
 • Ikiwa umebatizwa kwa kuzamishwa majini, ni kwa jinsi gani agano lako la ubatizo limebadilisha maisha yako ya kiroho katika kutembea na Yesu?

 

MWITIKIO WETU: NZK # 117.

 

Wamwendea Yesu: (Have You Been To Jesus?)

 

1.Wamwendea Yesu kwa kusafiwa. Kuoshwa kwa damu ya kondoo?

Je, neema yake yatumwagiwa? Waoshwa kwa damu ya Kondoo?

 

Kuoshwa, kwa damu Itutakasayo ya Kondoo?

Ziwe safi nguo nyeupe sana; waoshwa kwa damu ya Kondoo.

 

2.Wamwandana daima Mkombozi.Waoshwa kwa damu ya Kondoo?

Yako kwa Msulubiwa mavazi? Waoshwa kwa. Damu ya Kondoo?

 

3.Atakapokuja Bwana-arusi Uwe safi katika damu!

Yafae kwenda Mbinguni mavazi: Yaoshwa kwa damu ya kondoo?

 

4.Yatupwe Yalipo na takataka; Uoshawe kwa damu ya Kondoo:

Huoni kijito chatiririka Uoshwe kwa damu ya Kondoo?

 

OMBI: Asante sana Baba yetu wa mbinguni kwa tafakari ya somo la Leo. Tusaidie kuyatii na kuyashika yaliyonenwa humu, tusaidie tukurudie Wewe, na kila saa kuwa chini ya uongozi wa Roho Wako. Tusaidie Bwana, Leo, tunapoendelea kuisikia sauti Yako, tusifanye migumu mioyo yetu, tukaja kuangamia kama baba zetu walivyoangamia. Tupatie shauku ya kujifunza Neno Lako tena na tena, na kulishika, Bwana.  Tubatize upya kila siku Bwana. Bariki watoto Wako sasa wanapoendelea kutafakari somo hili. Kaa pamoja na kila mmoja wetu hadi hapo kesho tena. Asante sana Bwana, tumeomba haya katika Jina la Yesu Kristo, Amina.

 

MWISHO

(Karibu katika Mjadala/ Maswali/ Nyongeza)

 

The Gospel’s Voice © 2017