2/26/17: Tumaini kwa Mkimbizi

Tumaini kwa Mkimbizi

  • Mhutubu: Mwl. Peter Marwa
  • Fungu kuu: Mwanzo 28:12
    • Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. 

Huku akiwa ametishiwa kifo kutokana na ghadhabu ya Esau, Yakobo alitoka nyumbani mwa baba yake akiwa mkimbizi; lakini alikwenda na baraka za baba yake; Isaka alikuwa amefanya upya tena ahadi ya agano kwa Yakobo na alikuwa amemuagiza, kama mrithi wake, kutafuta mke kutoka katika familia ya mama yake Yakobo kule Mesopotomia. Hata hivyo, Yakobo alifanya safari yake ya upweke akiwa na moyo mzito sana.akiwa ameshikilia fimbo tu mkononi mwake, ni lazima alisafiri maili mamia kwenye nchi iliyokaliwa na kabila za watu wakali, waliokuwa wakitangatanga. Katika hali yake ya majuto na kutojiamini alijitahidi kuepuka watu, asijeonwa na kaka yake aliyekuwa na hasira. Aliogopa kuwa alikuwa amepoteza milele baraka ambazo Mungu alikuwa amekusudia iwe yake; na Shetani alikuwa karibu ili kushinikiza majaribu dhidi yake …

Giza la kukata tamaa liliusonga moyo wake na hakuwa na nguvu hata ya kuomba. Lakini alikuwa mpweke kabisa kiasi cha kujisikia hitaji la ulinzi kutoka kwa Mungu kuliko alivyowahi kujisikia kabla. Huku akilia na kujidhili kabisa aliungama dhambi yake na kusihi apate uthibitisho kwamba hakuwa ameachwa kabisa… Mungu hakumwacha Yakobo. Rehema zake bado zilienda kwa mtumishi wake aliyekosa, aliyekuwa katika mashaka. Kwa huruma, Bwana alidhihirisha kile ambacho ndicho hasa alichokihitaji Yakobo – Mwokozi….

Akiwa amechoshwa na safari yake, msafiri huyu alilala chini kwenye ardhi, akifanya jiwe kuwa mto wake. Usingizini, aliona ngazi, iliyokuwa angavu kwa mng’ao wake, ambayo kitako chake kilikuwa duniani, wakati kilele chake kikifikia mbinguni. Kwenye ngazi hii, malaika walikuwa wakipanda na kushuka; na juu yake alikuwepo Bwana wa utukufu….

Katika utulivu wa usiku wa manane, Yakobo aliamka kutoka usingizini. Mng’ao wa njozi aliyoipata ulikuwa umetoweka. Sasa, mwonekano hafifu wa vilima vya upweke na juu yake mbingu zilizoangazwa kwa nyota, vilionekana mbelel yake. Lakini alikuwa na hisia nzito kwamba Mungu alikuwa pamoja naye. Kuwepo kwake asiyeonekana kulijaza upweke. Naye akasema, “Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua.”… “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.”