2/26/17: Roho Mtakatifu Hutuunganisha na Kristo

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA

Fungu La Kukariri

Waefeso 4:3-5

 • 3 Na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.
 • 4 Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.
 • 5 Bwana mmoja, Imani moja, Ubatizo mmoja.

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu. Jina Lako litukuzwe milele. Asante Bwana kwa nafasi nyingine ya uhai. Asante kwa zawadi ya Neno Lako. Kabala ya kuanza kipindi hiki, tunaalika uwepo Wako, Bwana. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Bariki kila mmoja Bwana. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

Somo la Leo:

ROHO MTAKATIFU HUTUUNGANISHA NA KRISTO

Aya ya kwanza inasomeka hivi:

 • “Roho Mtakatifu hutuunganisha sisi katika njia za namna nyingi. Tusingeendelea kuwepo kama kanisa endapo Roho Mtakatifu asingeliweza kwanza kutuunganisha pamoja na Kristo. Kristo ndiye kichwa cha kanisa (angalia Waefeso 1:22, 23; 5:23). Kupitia Roho Mtakatifu, tunaunganishwa kabisa na Kristo Mwenyewe. Kuunganishwa na Kristo ni msingi wa baraka zote za wokovu, kwa sababu vyote tulivyo navyo katika Bwana hutokea Kwake. Kitendo sisi cha kutwaliwa kama wana na mabinti wa Kristo, kuhesabiwa kwetu haki pamoja na utakaso wetu, kuishi kwetu maisha ya ushindi dhidi ya dhambi, na kutukuzwa kwetu mwishoni, vyote hivi hupokelewa kupitia mwunganiko wetu na Kristo. Kwa hiyo, lazima Yeye awe msingi wa uzoefu wetu wote wa Kikristo.”

 

SWALI # 1: Je, Waefeso 2:18, 20-22 na 1 Petro 2:6, 7 hutuambia nini kuhusu kazi ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu katika uundwaji wa kanisa?

Waefeso 2:18, 20-22

 • 18 Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja. 20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. 21 Katika Yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. 22 Katika Yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.

1 Petro 2:6, 7

 • 6 Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.  7 Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.

 

Mwandishi wa Lesoni anaendelea kusema hivi:

 • “Kupitia Roho, tunayo nafasi ya kumwendea Mungu Baba. Yesu ni mwamba, msingi wa wokovu wetu, na ambaye sehemu zingine zote za jengo zima zinainuliwa juu yake.”
 •  “Kazi ya Roho Mtakatifu katika kiwango cha mtu binafsi huongoza kwenda kwa jumuia maalumu ya imani: kanisa. Tunapokuwa tumepata uzoefu wa wokovu kupitia imani katika Kristo Yesu pekee, na baada ya kuguswa na upendo wa Mungu, kuna mazingira yenye mvuto mzuri ya “ushirika wa Roho Mtakatifu” (2 Kor. 13:14) kanisani. Waumini mmoja mmoja hujengwa katika nyumba mpya ya Mungu “katika Roho” (Efe. 2:22). Kama wafuasi wa Kristo tunapaswa kuwa na shauku ya “kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani” (Efe. 4:3). Katika kila njia iwezekanavyo, bila kuridhia na kushusha viwango kwa mambo yale yasiyoweza kamwe kuridhiwa, tunahitaji kutafuta amani katika ushirika wa waumini.”

 

Soma Wakolosai 3:12-14 kisha jibu swali la pili.

Wakolosai 3:12-14.

 • 12 Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,  13 mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. 14 Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.

 

SWALI # 2: Unaweza kudhihirishaje sifa hizo na kuchangia katika umoja kanisani?

Sifa zinazotajwa katika fungu hili (Wakolosai 3:12-14) zinaweza kuchangia kwa hali moja au nyingine kuleta umoja katika jamii ya Mungu. Hebu tafakari sifa/ tabia zifuatazo:

 1. Moyo wa rehema,
 2. Utu wema,
 3. Unyenyekevu,
 4. Upole,
 5. Uvumilivu,
 6. Kuchukuliana, na Kusameheana,
 7. UPENDO, “ndio kifungo cha ukamilifu”

SWALI # 3: Kwa nini sifa hizi ni za msingi sana kwa ajili ya umoja wa kanisa?

 • Tunapokuwa na tabia zilizotajwa hapo juu, tutajengwa pamoja, kama familia moja ya Mungu, na mienendo na mvuto wetu utadhihirisha wazi kuwa tupo chini ya utawala na uongozi wa Roho wa Mungu.

Waefeso 2:22: “Katika Yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”


 

MWITIKIO WETU: NZK # 40 – “Nijaze Sasa”

(1) Njoo, Roho Mtukufu uoshe moyo wangu, Utakase nia yangu, njoo, nijaze sasa.

 • Roho Mtukufu, njoo, nijaze sasa;
 • Utakase nia yangu, njoo, nijaze sasa.

(2) Unijaze moyo wangu Ijapo sikuoni, Nami ninakuhitaji, njoo, nijaze sasa.

(3) Nimejaa udhaifu, nainamia kwako; Roho Mtukufu sasa, nitilie na nguvu.

(4) Unioshe nifariji niponye, nibariki,Unijaze moyo wangu; ndiwe mwenye uwezo.

 

OMBI: Asante sana Baba yetu wa mbinguni kwa tafakari ya somo la Leo. Tusaidie kuyatii na kuyashika yaliyonenwa humu, tusaidie tukurudie Wewe, na kila saa kuwa chini ya uongozi wa Roho Wako. Tusaidie Bwana, Leo, tunapoendelea kuisikia sauti Yako, tusifanye migumu mioyo yetu, tukaja kuangamia kama baba zetu walivyoangamia. Tupatie shauku ya kujifunza Neno Lako tena na tena, na kulishika, Bwana.  Bariki watoto Wako sasa wanapoendelea kutafakari somo hili. Kaa pamoja na kila mmoja wetu hadi hapo kesho tena. Asante sana Bwana, tumeomba haya katika Jina la Yesu Kristo, Amina.


 

MWISHO

(Karibu katika Mjadala/ Maswali/ Nyongeza)

 

The Gospel’s Voice © 2017