1/5/17: Roho Mtakatifu na Neno la Mungu

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA

Fungu La Kukariri

 • Timotheo 3:16-17
 • 16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; 17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

OMBI: Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika mwongozo wa kujifunza Biblia. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


Somo la Leo:

ROHO MTAKATIFU NA NENO LA MUNGU

2 Petro 1:19-21.

 • 19 Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.
 • 20 Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu.
 • 21 Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

 

SWALI # 1: Je fungu hili la 2 Petro 1:19-21, lina maana gani?

SWALI # 2: Je, kuna uhusiano gani kati ya Roho Mtakatifu na Neno la Mungu?

SWALI # 3: Je, kuna uhusiano gani kati ya Kristo Yesu; Roho Mtakatifu na Neno la Mungu?

SWALI # 4: Je kuna tofauti gani hapa kati ya hekima ya mwanadamu na fikra ya mwanadamu inayoongozwa na Roho Mtakatifu?


[1:21a] = “Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu”

 • Maandiko matakatifu si ya asili ya kibinadamu, wala si matokeo ya mapenzi ya mwanadamu. Mkazo katika kishazi hiki, ni kwamba,  hakuna sehemu yo yote ya maandiko iliyoletwa kwetu kwa sababu watu walinuia hivyo. Ni vyema kusisitiza kuwa: BIBLIA SI MATOKEO YA JUHUDI YA BINADAMU. Hata Manabii wanaotajwa katika maandiko,  wakati mwingine waliandika kile ambacho hawakukifahamu kikamilifu (1 Ptro 1:10, 11), lakini hata hivyo walikuwa waaminifu kuandika kile kilichofunuliwa kwao na Mungu.

1 Petro 1:10-12

 • 10 Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi.
 • 11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.
 • 12 Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia.

[1:21b] = “Bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu”.

 • Sentensi hii ina maana kwamba {Grammatically}: walikuwa daima wakibebwa na kuongozwa na Roho wa Mungu

 

ZINGATIA MAFUNGU YAFUATAYO:

 • Luka 1: 70
  • Kama Alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu
 • 2 Samweli 23:2.
  • Roho ya Bwana ilinena ndani yangu, Na neno lake likawa ulimini mwangu
 • Marko 12:36.
  • Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.
 • Matendo 28:25.
  • Na walipokuwa hawapatani wao kwa wao, wakaenda zao, Paulo alipokwisha kusema neno hili moja, ya kwamba, Roho Mtakatifu alinena vema na baba zetu, kwa kinywa cha nabii Isaya
 • Warumi 1:1-2.
  • 1 Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu;
  • 2 ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu;
 • Waebrania 1:1
  • Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi.
 • Waebrania 3:7.
  • Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake,
 • 2 Petro 1:21.
  • Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
 • Ufunuo 19:10
  • Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii

Kwa hiyo wapendwa, Roho Mtakatifu ndiye mtunzi, mwanzilishi, asili; ndiye Muumbaji, ndiye mgunduzi, mtayarishaji na mtoaji wa  Maandiko matakatifu.  

Katika Agano la kale peke yake, waandishi wa biblia wamerejelea maandiko yao kama maneno ya Mungu, au  “Neno la Bwana” takribani kama mara 3800 hivi;  (Kwa mfano: Yer 1:4; 2 Pertro 3:2; Rum 3:2; 1 Wakorintho 2:10).

 • Yer 1:4
  • Neno la Bwana lilinijia, kusema;
 • 2 Pertro 3:2
  • Mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu.
 • Rum 3:2
  • Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu.
 • 1 Wakorintho 2:10
  • Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.

Ingawa waandishi wa kibinadamu wa maandiko walijishugulisha katika mchakato mzima wa kuandika Maandiko Matakatifu, ukweli ni kwama, Mungu Roho Mtakatifu ndiye aliyesimamia mchakato mzima. Mungu Roho Mtakatifu ndiye aliyeongoza fikra zao wakiandiaka, akiwapa  maneno ya kuandika (misamiati), na matokeo yake ni kwamba waliandika bila kukosea hata nukta moja ya kama ilivyo nuiwa na Mtunzi Mkuu mwenyewe, yaani: MUNGU ROHO MTAKATIFU


HITIMISHO:

Kwa hivyo wapendwa; Nakala halisi za maandiko zimevuviwa, kama fungu letu kuu/ fungu la kukariri katika wiki hii, linavyosema: “16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; 17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” (2 Timotheo 3:16-17)

 

HAYANA MAKOSA; KASORO; AU DOSARI YO YOTE:

 • Yohana 10:34, 35;
  • 34 Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?
  • 35 Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka);
 • Yohana 17:17;
  • Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.
 • Tito 1:2
  • Katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;
 • Mithali 30: 5
  • Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.

 

Kumbuka mambo yafuatayo tunapofunga somo hili:

 1. Mtunzi wa Maandiko Matakatifu ni Mungu Roho Mtakatifu
 2. Nakala halisi za Maandiko (The original copies of Scripture) zimevuviwa
 3. Biblia haina makosa/ kasoro
 4. Mungu amedhihirisha mapenzi Yake kwetu katika Maandiko Matakatifu
 5. Mungu Roho Mtakatifu hawezi kamwe kuoingana na Neno Lake; yaani Maandiko Matakatifu
 6. Maandiko Matakatifu ndiyo mamlaka pekee tuliyopewa na tunayopaswa kuzingatia na kutii.
 7. Maandiko Matakatifu yametolewa kwa faida yetu sisi: “16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; 17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” (2 Timotheo 3:16-17)

 

TUFANYE NINI BASI NA SOMO LA LEO?

Mpendwa, ebu sikia “SAUTI YA INJILI” i.e. “SAUTI YA BWANA” ikinena nawe leo:

 • Zaburi 95:7-9
  • 7 Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
  • 8 Msifanye migumu mioyo yenu; Kama vile huko Meriba Kama siku ya Masa jangwani.
  • 9 Hapo waliponijaribu baba zenu, Wakanipima, wakayaona matendo yangu.
 • Waebrania 3:7-9
  • 7 Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake,
  • 8 Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa,
  • 9 Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini.

 

MWITIKIO WETU: NZK # 40 – “Nijaze Sasa”

Njoo, Roho Mtukufu uoshe moyo wangu,

Utakase nia yangu, njoo, nijaze sasa.

Chorus:

 • Roho Mtukufu, njoo, nijaze sasa;
 • Utakase nia yangu, njoo, nijaze sasa.

 

Unijaze moyo wangu Ijapo sikuoni,

Nami ninakuhitaji, njoo, nijaze sasa.

 

Nimejaa udhaifu, nainamia kwako;

Roho Mtukufu sasa, nitilie na nguvu.

 

Unioshe nifariji niponye, nibariki,

Unijaze moyo wangu; ndiwe mwenye uwezo.

 

OMBI: Asante sana Baba yetu wa mbinguni kwa tafakari ya somo la Leo. Tusaidie kuyatii na kuyashika yaliyonenwa humu, tusaidie tukurudie Wewe, na kila saa kuwa chini ya uongozi wa Roho Wako. Tusaidie Bwana, Leo, tunapoendelea kuisikia sauti Yake, tusifanye migumu mioyo yetu, tukaja kuangamia kama baba zeu walivyoangamia. Tupatie shauku ya kujifunza Neno Lako tena na tena, na kulishika, Bwana.  Bariki watoto Wako sasa wanapoendelea kutafakari somo hili. Kaa pamoja na kila mmoja wetu hadi hapo kesho tena. Asante sana Bwana, tumeomba haya katika Jina la Yesu Kristo, Amina.


 

MWISHO

(Karibu katika mjadala/ Nyongeza)

 

© Sauti Ya Injili SDA     www.tgvs.org