1/3/17: Roho Mtakatifu na Ukweli wa Maandiko

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA

Fungu La Kukariri

Timotheo 3:16-17

 • 16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; 17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

OMBI: Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika mwongozo wa kujifunza Biblia. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

Somo la Leo:

ROHO MTAKATIFU NA UKWELI WA MAANDIKO

Wakati ambapo ufunuo ni tendo la kiungu ambalo Mungu hutumia ili kuifunua kweli yake kwa wanadamu waliochaguliwa, uvuvio ni utendaji wa Roho Mtakatifu unaolinda ukweli wa kile walichoandika waandishi wanadamu, ili maneno yao yaweze kupata ukubali kamili wa Mungu. Mungu anauchukia ushuhuda wa uongo (Kut. 20:16) na hawezi kusema uongo (Ebr. 6:18). Anaitwa Mungu wa kweli (Zab. 31:5; Isa. 65:16). Katika namna hiyohiyo, Roho Mtakatifu anaitwa “Roho wa kweli” (Yn. 14:17).

 

NUKUU ZA MAFUNGU HAYO:

Kutoka 20:16

 • Usimshuhudie jirani yako uongo

Waebrania 6:18

 • Ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu;

Zaburi 31:5

 • Mikononi Mwako naiweka roho Yangu; Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.

Isaya 65:16

 • Hata itakuwa yeye atakayejibariki duniani, atajibariki kwa Mungu wa kweli; naye atakayeapa duniani, ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za kwanza zimesahauliwa, na kwa kuwa zimefichwa machoni pangu.

Yohana 14:17

 • Ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.

 

SOMA MAFUNGU YAFUATAYO KISHA JIBU MASWALI:

Zaburi 119:160.

 • Jumla ya neno Lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki Yako ni ya milele.

SWALI # 1: Hili hutufundisha nini kuhusu lolote analotufunulia Mungu?

Yohana 17:17.

 • Uwatakase kwa ile Kweli; Neno Lako ndiyo Kweli.

SWALI # 2: Je, ni jambo gani analotuambia Yesu hapa kuhusu Neno la Mungu?

 • Neno la Mungu linaaminika na linastahili kukubaliwa kikamilifu. Siyo kazi yetu kukaa na kuyahukumu Maandiko; badala yake, Maandiko ndiyo yenye haki na mamlaka ya kutuhukumu sisi.
 • “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo” (Ebr. 4:12).
 • Ingawa, kwa kweli, Biblia iliandikwa na wale walioishi katika nyakati na mahali na tamaduni maalumu (ingeliwezekanaje kuwa vinginevyo?), hatupaswi kutumia ukweli huo ili kuhafifisha au kutupilia mbali ujumbe wa Biblia uliokusudiwa kwa ajili yetu. Mara mlango huo unapofunguliwa, Biblia huwa chini ya uchanganuzi wa wanadamu na ya maamuzi yao ya kile kilicho kweli. Matokeo yake ni kuwa, watu wengi, wakati wakidai kuiamini Biblia, hukataa mambo kama vile uumbaji wa siku sita, gharika ya ulimwengu mzima, kuzaliwa kwa njia ya bikira, ufufuo wa mwili halisi wa Yesu, na Marejeo halisi ya Pili. Haya ni machache tu miongoni mwa kweli nyingi za Kibiblia ambazo watu wenye makosa, wakiwa wamekaa katika kuyahukumu Maandiko, wameyatupilia mbali. Hiyo siyo njia ambayo yeyote miongoni mwetu anapaswa kupitia.

 

SWALI # 3: Kwa nini ni muhimu sana kuyasalimisha mawazo yetu wenyewe chini ya Neno la Mungu badala ya kufanya kinyume Chake?

Zaburi 119:103-105

 • 103 Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu.
 • 104 Kwa mausia Yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.
 • 105 Neno Lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.

Timotheo 3:16-17

 • 16 Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; 17 ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.

 

OMBI: Asante sana Baba yetu wa mbinguni kwa tafakari ya somo la Leo. Tusaidie kuyatii na kuyashika yaliyonenwa humu, tusaidie tukurudie Wewe, na kila saa kuwa chini ya uongozi Wako. Bariki watoto Wako sasa wanapoendelea kutafakari somo hili. Kaa pamoja na kila mmoja wetu hadi hapo kesho tena. Asante sana Bwana, tumeomba haya katika Jina la Yesu Kristo, Amina.