43-005: Kitabu cha Yohana 5

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

MASWALI MUHUMU KATIKA SURA HII

 1. Je, mada kuu ni ipi katika sura hii?
 2. Je, wahusika wakuu ni nani katika sura hii?
 3. Je, matukio makuu yapo eneo/ maeneo gani?
 4. Je, kuna dhambi ya kuepukwa au kukiri?
 5. Je, kuna amri/wajibu fulani wa kuzingatiwa?
 6. Je, kuna ahadi yo yote kwa ajili yangu hapa?
 7. Je, kuna mfano wo wote wa kuigwa hapa?
 8. Je, tufanye nini basi na injili katika sura hii?

MUHTASARI WA SURA HII

YALIYOMO, (Mawazo Makuu):

 1. Yesu Amponya Mtu Penye Bwawa La Bethzatha
 2. Mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka 38.
 3. Wayahudi, Sabato, na Aliyeponywa
 4. Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena
 5. Wayahudi wakamwudhi Yesu
 6. Uungu na Mamlaka ya Yesu Kristo
 7. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.
 8. Kumwamini Yeye aliyenipeleka
 9. Saa inakuja, na Sasa Ipo
 10. Saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia Sauti Yake.
 11. Siyatafuti Mapenzi Yangu Mimi, Bali Mapenzi Yake Aliyenipeleka.
 12. Yuko Mwingine Anayenishuhudia (Roho)
 13. Ushuhuda mkubwa kuliko ule wa Yohana (Baba)
 14. Na Hayo Ndiyo Yanayonishuhudia (Maandiko)

 

Neno Kuu: Uponyaji, f. 8.

Tabia ya Mungu: Upendo, Huruma, Ufahamu

Tabia ya Kristo: Hukumu, Utii, Huruma, Upendo

Mistari Ya Msisitizo: Yohana 5:23, 24, 28, 29, 39.

Wahusika:

 1. Yesu Kristo
 2. Mungu Baba
 3. Roho Mtakatifu
 4. Vipofu, Viwete, nao Waliopooza
 5. Wafarisayo/ Wayahudi
 6. Yohana Mbatizaji
 7. Musa

OMBI: Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

YESU AMPONYA MTU PENYE BWAWA LA BETHZATHA

1 Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu.

2 Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano.

3 Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke.

4 Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.]

 

MTU, AMBAYE AMEKUWA HAWEZI MUDA WA MIAKA THELATHINI NA MINANE.

5 Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane.

6 Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima?

7 Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.

8 Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende.

9 Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.

 

WAYAHUDI, SABATO, NA ALIYEPONYWA

10 Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro.

11 Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende.

12 Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike, uende, ni nani?

13 Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale.

 

ANGALIA, UMEKUWA MZIMA; USITENDE DHAMBI TENA

14 Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.

15 Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima.

 

WAYAHUDI WAKAMWUDHI YESU

16 Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato.

17 Akawajibu, Baba yangu anatenda kazi hata sasa, Nami ninatenda kazi.

18 Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba Yake, akijifanya sawa na Mungu. Basi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin, nawaambia,

 

UUNGU NA MAMLAKA YA YESU KRISTO

19 Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo Yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.

20 Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, Naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizo atamwonyesha, ili ninyi mpate kustaajabu.

21 Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao.

22 Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote;

 

ASIYEMHESHIMU MWANA HAMHESHIMU BABA ALIYEMPELEKA.

23 Ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.

 

KUMWAMINI YEYE ALIYENIPELEKA

24 Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye Neno Langu na kumwamini Yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.

 

SAA INAKUJA, NA SASA IPO

25 Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.

26 Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.

27 Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu.

 

SAA YAJA, AMBAYO WATU WOTE WALIOMO MAKABURINI WATAISIKIA SAUTI YAKE.

28 Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.

29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.

 

SIYATAFUTI MAPENZI YANGU MIMI, BALI MAPENZI YAKE ALIYENIPELEKA.

30 Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.

 

YUKO MWINGINE ANAYENISHUHUDIA (ROHO)

31 Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli.

32 Yuko mwingine anayenishuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli.

33 Ninyi mlituma watu kwa Yohana, naye akaishuhudia kweli.

34 Lakini Mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka.

35 Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda.

 

USHUHUDA MKUBWA KULIKO ULE WA YOHANA (BABA)

36 Lakini ushuhuda nilio nao Mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma.

37 Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti Yake hamkuisikia wakati wo wote, wala sura Yake hamkuiona.

38 Wala Neno Lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na Yeye.

 

NA HAYO NDIYO YANAYONISHUHUDIA (MAANDIKO)

39 Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.

40 Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima.

41 Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu.

42 Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu.

43 Mimi nimekuja kwa jina la Baba Yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo.

44 Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?

45 Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi.

46 Kwa maana kama mngalimwamini Musa, Mngeniamini Mimi; kwa sababu yeye aliandika habari Zangu.

47 Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?


HITIMISHO:

MASWALI MUHUMU KATIKA SURA HII

Je, mada kuu ni ipi katika sura hii? = Uungu wa Yesu Kristo

Je, wahusika wakuu ni nani katika sura hii?

Je, matukio makuu yapo eneo/ maeneo gani?

 1. Yerusalemu
 2. Penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha,

Je, kuna dhambi ya kuepukwa au kukiri?

 1. Kutomwamini Mwana Pekee wa Mungu
 2. Kutoamini Ishara Zake

Je, kuna amri/wajibu fulani wa kuzingatiwa?

 1. Simama, jitwike godoro lako, uende.

Je, kuna Onyo fulani la kuzingatiwa?

 • 39 Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. 40 Wala hamtaki kuja Kwangu mpate kuwa na uzima.

Je, kuna ahadi yo yote kwa ajili yangu hapa?

 • 28 Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.
 • 29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.

Je, kuna mfano wo wote wa kuigwa hapa?

Je, tufanye nini basi na injili katika sura hii?

Katika sura hii tumeona

 • Uponyaji wa mtu katika bwawa la Bethesda.
 • Yesu alivyokabiliana na Wayahudi.
 • Ushahidi uliotolewa mara nne kuhusu Uungu/ Ukuu wa Yesu.

Yesu Kristo, mwana wa Mungu,aliye na uwezo, mamlaka, na nguvu;   hufurahia sana kusaidia wanyonge, na kudhihirisha upendo na Rehema Zake kwa wale ambao wako tayari kuamini, na kusaidiwa.

Kumbuka Jambo fulani hapa:

Yesu aliuawa kwa sababu ya madai yake ya Uungu.

 • Yohana 2:13-21
  • 13 Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu.
  • 14 Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi.
  • 15 Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao;
  • 16 akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.
  • 17 Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila.
  • 18 Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya?
  • 19 Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.
  • 20 Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?
  • 21 Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake.

Kama alikuwa hana cheo cha Uungu/ au {madai yanayoelezwa katika fungu la 23}; angekuwa anakufuru.

Kama ana cheo cha Uungu kulingana na {madai yanayoelezwa katika fungu la 23}; basi hakukufuru.

Uthibitisho wa swali hili ni Ufufuko Wake.

Swali hili linajibiwa kwa kishondo katika uwezo Wake wa ufufuo.

Kwa hiyo, kwa wale ambao bado hukataa/ hukanusha ukweli kuhusu Uungu Wake, hata leo, wako sawa sawa na wale waliomsulubisha.

 • Marko 14:57-64
  • 57 Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema,
  • 58 Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.
  • 59 Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana.
  • 60 Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini?
  • 61 Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?
  • 62 Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni.
  • 63 Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi?
  • 64 Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa.

 

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu mpendwa, tunashukuru kwa tafakari ya Neno Lako katika sura hii. Twaomba Roho Wako aendelee kutufundisha sura hii tena na tena. Tukumbushe kuyasoma maandiko, na kuendelea kuyasikia “maneno ya Unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu”.Tusaidie kuwa “watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali tukijidanganya nafsi zetu”. Ebu mmoja aguswe na kubadilishwa na Neno hili zuri la Kristo Yesu. Asante Bwana, na twaja katika Jina la Yesu Kristo, aliye Bwana na Mkombozi wetu, Amina!


  NYONGEZA, AUDIO MESSAGE

 • Sikiliza Injili fupi ya Sura hii hapo chini.
 • Somo hili linapatikana katika Tovuti, Facebook na Mobile App: (The Gospel’s Voice)
 • BWANA ATUBARIKI SOTE!

 

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

 • Sauti Ya Injili SDA © 2016. All Rights Reserved.
 • tgvs.org