43-004: Kitabu cha Yohana 4

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

MUHTASARI WA SURA HII

 Yaliyomo, (Mawazo Makuu):

 1. Mwanamke Msamaria
 2. Wayahudi hawachangamani na Wasamaria
 3. Kama ungaliijua karama ya Mungu
 4. Kila anywaye maji haya ataona kiu tena
 5. Bwana, naona ya kuwa u nabii!
 6. Kumwabudu katika Roho na Kweli
 7. Mimi ninayesema nawe, Ndiye.
 8. Njoni, Mtazame Mtu
 9. Chakula Changu ndicho Hiki
 10. Ufahamu wa Kristo katika nafsi za Watu
 11. Uinjilisti Samaria
 12. Nabii hapati heshima katika nchi Yake mwenyewe.
 13. Enenda; mwanao yu hai.

 Neno Kuu: Maji ya Uzima

Tabia ya Mungu: Upendo, Huruma, Ufahamu

Tabia ya Kristo: Uinjilisti, Bible study, Utii, Huruma, Upendo

Mistari Ya Msisitizo: Yohana 4:7, 10, 14, 23, 24.

Wahusika:

 1. Yesu Kristo – (Masihi ajaye)
 2. Roho Mtakatifu
 3. Yohana Mbatizaji
 4. Wafarisayo
 5. Jacob, (Yakobo)
 6. Yusufu, (Joseph)
 7. Mwanamke wa Samaria
 8. Mume Wake; (Waume zake)
 9. Diwani Mmoja
 10. Mtoto Wake.

OMBI: Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

MWANAMKE MSAMARIA

1 Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza,

2 (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi Wake,)

3 aliacha Uyahudi, akaenda zake tena mpaka Galilaya.

4 Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria.

5 Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe.

6 Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari Yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.

7 Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe.

8 Kwa maana wanafunzi Wake wamekwenda mjini kununua chakula.

 

WAYAHUDI HAWACHANGAMANI NA WASAMARIA

9 Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.)

 

KAMA UNGALIIJUA KARAMA YA MUNGU

10 Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.

11 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai?

12 Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?

 

KILA ANYWAYE MAJI HAYA ATAONA KIU TENA

13 Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;

14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.

15 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.

 

BWANA, NAONA YA KUWA U NABII!

16 Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa.

17 Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume;

18 kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli.

19 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!

20 Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.

 

KUMWABUDU KATIKA ROHO NA KWELI.

21 Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.

22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.

24 Mungu ni Roho, nao wamwabuduo Yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

 

KRISTO; “MIMI NINAYESEMA NAWE, NDIYE”.

25 Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); Naye atakapokuja, Yeye atatufunulia mambo yote.

26 Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, NDIYE.

 

NJONI, MTAZAME MTU

27 Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye?

28 Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu,

29 Njoni, mtazame Mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?

30 Basi wakatoka mjini, wakamwendea.

 

CHAKULA CHANGU NDICHO HIKI

31 Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule.

32 Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.

33 Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula?

34 Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi Yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi Yake.

 

UFAHAMU WA KRISTO KATIKA NAFSI ZA WATU

35 Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.

36 Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja.

37 Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine.

38 Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.

 

UINJILISTI KATIKA SAMARIA

39 Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda.

40 Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili.

41 Watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake.

42 Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.

 

NABII HAPATI HESHIMA KATIKA NCHI YAKE MWENYEWE.

43 Na baada ya siku mbili hizo akaondoka huko, akaenda Galilaya.

44 Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba Nabii hapati heshima katika nchi Yake mwenyewe.

45 Basi alipotoka Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu.

 

ENENDA; MWANAO YU HAI.

46 Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu.

47 Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani.

48 Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?

49 Yule diwani akamwambia, Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu.

50 Yesu akamwambia, Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia.

51 Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai.

52 Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, Jana, saa saba, homa ilimwacha.

53 Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake.

54 Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Uyahudi kufika Galilaya.


 

HITIMISHO:

Maarifa ya kiungu ya Yesu Kristo yanathibitisha uwezo na upeo wa utambuzi Wake (His Omniscience). Yesu anajua vyema mawazo, maneno na matendo yote ya kila binadamu, na kwa uwezo wa Neno Lake, bado anafunua dhambi za siri zilizofichwa ndani ya mioyo ya binadamu.

Yesu Kristo ndiye  “karama ya Mungu”; “the gift of God” {Yohana 4:10}

 • Yeye ni ishara ya utajiri wa upendo wa Mungu,
 • Yeye ni chanzo na chemchemi ya maji ya Uzima
 • Ndani Yake kuna “chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.”
 • Yeye anao uwezo wa kuridhisha nafsi iliyo na kui ya Neno La Mungu
 • Yeye anao uwezo wa kubadilisha maisha kabisa, (toka mdhambi kwenda mteule)
 • Wale wanaokuja Kwake, kamwe hawataona Kiu Tena

Yohana 4:14

 • Walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa Mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu mpendwa, tunashukuru kwa tafakari ya Neno Lako katika sura hii. Twaomba Roho Wako aendelee kutufundisha sura hii tena na tena. Tukumbushe kuyasoma maandiko, na kuendelea kuyasikia “maneno ya Unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu”.Tusaidie kuwa “watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali tukijidanganya nafsi zetu”. Ebu mmoja aguswe na kubadilishwa na Neno hili zuri la Kristo Yesu. Asante Bwana, na twaja katika Jina la Yesu Kristo, aliye Bwana na Mkombozi wetu, Amina!


NYONGEZA, AUDIO MESSAGE

 • Sikiliza Injili fupi ya Sura hii hapo chini.
 • Somo hili linapatikana katika Tovuti, Facebook na Mobile App: (The Gospel’s Voice)
 • BWANA ATUBARIKI SOTE!

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

 • Sauti Ya Injili SDA © 2016. All Rights Reserved.
 • tgvs.org