43-002 Kitabu cha Yohana 2

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

MUHTASARI WA SURA HII

Yaliyomo: (Mawazo Makuu)

  1. Miujiza ya Yesu Kristo
  2. Maji kuwa Divai
  3. Kutakaswa kwa Hekalu
  4. Yeye ajuaye yaliyomo ndani ya mwanadamu.

Wahusika:

  • Yesu Kristo, Mama Yake, Wanafuzi, Wafanyabiashara hekaluni, Wayahudi, Watu wa kawaida

Neno Kuu: Utii/ Imani Iokoayo

Mistari Ya Msisitizo: Yohana 2:5,16, 23-24

OMBI: Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, kuachana na dhambi, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!


 

MAJI YAGEUZWA KUWA DIVAI

1 Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo.

2 Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.

3 Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai.

4 Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.

5 Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni.

6 Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu.

7 Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu.

8 Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka.

9 Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi,

10 akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.

11 Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.

12 Baada ya hayo akashuka mpaka Kapernaumu, Yeye na mama Yake na ndugu Zake na wanafunzi Wake; wakakaa huko siku si nyingi.

 

YESU ATAKASA HEKALU

13 Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu.

14 Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi.

15 Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao;

16 akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.

17 Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba Yako utanila.

18 Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya?

19 Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.

20 Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?

21 Lakini Yeye alinena habari za hekalu la mwili Wake.

22 Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.

 

YEYE AJUAYE YALIYOMO NDANI YA MWANADAMU.

23 Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini Jina Lake, walipoziona ishara Zake alizozifanya.

24 Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa Yeye aliwajua wote;

25 na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana Yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu.


 

HITIMISHO:

Baada ya tukio hili, Yesu aliendelea kukaa katika Yerusalemu kwa ajili ya Pasaka na ya sikukuu ya mikate isiyotiwa Chachu ambayo ilifuatia. Ndani ya kipindi hicho, alitenda miujiza mbalimbali ambayo haijarekodiwa katika maandiko: “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. (Yohana 20:30); “Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa”(Yohana 21:25).

Matokeo yake, watu wengi waliamini Jina Lake, huki wakuchunguza ishara Zake nyingi ambazo alikuwa akifanya. Aidha, wengine walidhani kuwa Yeye ni nabii (cf Mathayo 21:11; Luka 7:16), au hata Masia waliokuwa wakimatarajia (cf. Yohana 6:14 – 15, 26).

Lakini imani kama hiyo ilikuwa si ya kina kirefu, ya juu-juu, na si ya dhati. Haikuwa imani ya kweli, imani  iokoayo, {hii inadhihirishwa na tumizi ya vitenzi vilivyotumika hapa}

  • [Believed in verse 23 and Entrusting in verse 24 both come from the same Greek verb, pisteuō].
  • [“Waliamini” katika mstari wa 23 na “hakujiaminisha” katika mstari 24 zote zinatoka katika kitenzi kimoja cha Kigiriki, pisteuō].

ANGALIZO: Ingawa waliamini katika Yesu, Yesu hakuwa na imani kati/ ndani yao; “hakuwa na Imani katika imani yao“.


 

OMBI: Baba yetu na Mungu wetu mpendwa, tunashukuru kwa tafakari ya Neno Lako katika sura hii. Twaomba Roho Wako aendelee kutufundisha sura hii tena na tena. Tukumbushe kuyasoma maandiko, na kuendelea kuyasikia “maneno ya Unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu”.Tusaidie kuwa “watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali tukijidanganya nafsi zetu”. Ebu mmoja aguswe na kubadilishwa na Neno hili zuri la Kristo Yesu. Asante Bwana, na twaja katika Jina la Yesu Kristo, aliye Bwana na Mkombozi wetu, Amina!

 

 

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

© The Gospel’s Voice

© Sauti Ya Injili SDA