Ayubu 18

Kitabu cha Ayubu 18

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Haya ni mazungumzo ya pili ya Bildadi kuhusiana na mustakabali wa waovu. Dai lake ni kwamba daima wanaoteseka lazima watakuwa ni wadhalimu—watenda mabaya.

 1. Anamshutumu Ayubu kuwa hata uvumilivu na kicho (Ayubu 18:1-4);
 2. Anaonesha mwisho wa kuogofya wa waovu pamoja na uzao wao; na ni wazi kuwa anatumia kielelezo hiki kama hatima ya maisha ya Ayubu, ambaye anamtisha kwamba anakabiliana na mwisho wenye maangamizi (Ayubu 18:5-21).

 
1 Ndipo Bildadi, Mshuhi, akajibu, na kusema,

2 Je! Hata lini utayategea maneno mitambo? Fikiri, kisha baadaye tutanena.

 • [“Utawinda maneno ya kusema hata lini? Tafakati vizuri nasi tutasema” (Biblia Habari Njema). “Ni kwa muda mrefu kiasi gani hadi utakapokomesha maneno? Pata ufahamu, na baadaye tutasema.”]

3 Twahesabiwa kuwa wanyama kwa sababu gani, Tena kuwa wanajisi machoni pako?

4 Wewe ujiraruaye mwenyewe katika hasira yako, Je! Dunia itaachwa kwa ajili yako wewe? Au jabali litaondolewa mahali pake?

5 Naam, mwanga wa waovu utazimika, Wala mwali wa moto wake hautang’aa.

6 Mwanga hemani mwake utakuwa giza, Nayo taa iliyo juu yake itazimishwa.

 • [“Nuru ya mwenye haki yang’aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.” Mithali 13:9. “Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu; Taa ya mtu mbaya itazimika.” Mithali 24:20.]

7 Hatua zake za nguvu zitasongwa, Na shauri lake mwenyewe litamwangusha chini.

8 Kwani ametupwa katika wavu na miguu yake mwenyewe, Naye huenda juu ya matanzi.

 • [Waovu hujinasa wenyewe; hatima yao i katika makosa yao wenyewe. “Mataifa wamezama katika shimo walilolifanya; Kwa wavu waliouficha imenaswa miguu yao.” Zaburi 9:15. “Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.” Zaburi 35:8.]

9 Tanzi litamshika kisigino chake, Na mtambo utamgwia.

 • [“Mtego humkamata kisiginoni, tanzi humbana kabisa” (Biblia Habari Njema).]

10 Amefichiwa tanzi chini, Na mtego amewekewa njiani.

11 Matisho yatamtia hofu pande zote, Na kumfukuza karibu na visigino vyake.

12 Nguvu zake zitaliwa na njaa, Na msiba utakuwa tayari kwa kusita kwake.

13 Utakula via vya mwili wake, Naam, mzaliwa wa kwanza wa mauti atavila via vyake.

14 Atang’olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini; Naye atapelekwa kwake mfalme wa utisho.

 • [“mfalme wa utisho”= mauti]

15 Ambacho si chake kitakaa katika hema yake; Kiberiti kitamwagwa juu ya makazi yake.

16 Chini, mizizi yake itakaushwa; Na juu, tawi lake litasinyaa.

17 Kumbukumbu lake litakoma katika nchi, Wala hatakuwa na jina mashambani.

18 Atakimbizwa kutoka mwangani hata gizani, Na kufukuzwa atoke duniani.

19 Hatakuwa na mwana wala mjukuu kati ya watu wake, Wala hatasalia mtu hapo alipokaa.

20 Hao wanaokaa magharibi watastaajabia siku yake, Kama vile wanaokaa mashariki walivyotiwa hofu.

 • [“wanaokaa magharibi… wanaokaa mashariki”—kila mtu, kila mahali]

21 Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotovu, Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu.


 

UFUPISHO WA AYUBU 18

Jambo alilonalo Bildadi mawazoni mwake ni teolojia ya mauti ya Wamisri

 • wote wanaokufa huondoka duniani kwa boti (mashua) na mungu-jua (Ra) ili kuifanikisha safari katika “mbingu” ya Mto Naili.
 • Wanapitia malango 12 wakikabiliana na madubwana (majinamizi) wanaowatisha wakiwa safarini.
 • Wakati wa usiku wa manane, juu, utosini mwa Naili ya duniani, wanasimama kwenye jukwaa la hukumu la mungu Osiris kwa ajili ya hukumu ya uchunguzi na kungojea hukumu ya moto.

Bildadi anaendelea:

 • Mtu mwovu afapo, “Atang’olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini; Naye atapelekwa kwake mfalme wa utisho” (aya ya 14).
 • Kumbukumbu lake duniani litakoma na kusahaulika;
 • Hana jina wala mitaa ya makazi wala mashamba yake;
 • Anaondolewa toka mwangani na kupelekwa gizani, na wala hatakuwa na watoto kabisa (aya ya 17-19).

 

OMBI: Mungu Mpendwa, udanganyifu ulioko kila mahali kutuzunguka unavumbuliwa na wale wasiolisoma Neno Lako inavyopaswa. Mtazamo wa Bildadi wa utisho na hofu baada ya mauti unafanana na imani kadhaa katika ulimwengu wa leo. Lakini, kama ilivyokuwa kwa Ayubu, sisi tuna shauku ya kukumbukwa utakapokuja katika Marejeo Yako ya Pili. Vilevile, tunahitaji kukaa katika Kristo aliye Haki yetu kwa kuwa ndiye mwenye dhamana ya wokovu wetu ujao. Hii ndiyo dua yetu ya unyenyekevu. Katika Jina la Yesu, Amina!