Ayubu 16

Kitabu cha Ayubu 16

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Ayubu anazungumza dhidi ya rafiki zake wasio na huruma.

  1. Anamjibu Elifazi, na kupitia kwake, anawajibu rafiki zake wote, ambao, badala ya kumfariji, walizidishi taabu yake; na huonesha kuwa, kama wangelikuwa katika hali yake, angeliwatendea kwa namna tofauti (Ayubu 16:1-5).
  2. Anajikita katika hali yake ya kina kabisa ya mateso yake, (16:6-16).
  3. Anajifajiri mwenyewe kwa utambuzi wa kutokuwa kwake na hatia, ambapo anamwendea Mungu kama Shahidi wake, na kwa uvumilifu anategemea kukoma kwa mateso yake yote (16:17-22).

 
1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2 Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha.

3 Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini kinachokukasirisha, hata ukajibu?

4 Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na kuwatikisia ninyi kichwa changu.

5 Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na utuzo wa midomo yangu ungetuliza.

  • [“Ningeweza kuwatia moyo kwa maneno yangu, na maneno yangu ya faraja yangewatuliza” (Biblia Habari Njema). Ayubu anadai kwamba yeye angekuwa mfariji bora kuliko walivyo rafiki zake wanaomwumiza na kumkatisha tamaa zaidi “kwa maneno yasiyo faida” (aya ya 3).]

6 Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi; Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani?

7 Lakini sasa amenichokesha; Jamii yangu yote umeifanya ukiwa.

8 Umenishika sana, ni ushahidi juu yangu; Na kukonda kwangu kwaniinukia, kwanishuhudia usoni pangu.

9 Amenirarua katika ghadhabu zake, na kunionea; Amesaga-saga meno juu yangu; Mtesi wangu hunikazia macho makali.

10 Wamenifumbulia vinywa vyao; Wamenipiga shavuni kwa kunitukana; Hujikutanisha pamoja juu yangu.

11 Mungu amenitia kwa hao wapotovu, Na kunitupa mikononi mwao waovu.

12 Nilikuwa katika raha, naye akanivunja-vunja; Naam, amenishika shingo, na kuniponda; Tena amenisimamisha niwe shabaha yake.

13 Wapigaji wake wa mishale hunizingira kotekote, Hunipasua viuno vyangu, asinihurumie; Nyonga zangu amezimwaga juu ya nchi.

14 Hunivunja kwa uvunjifu juu ya uvunjifu; Hunishambulia mfano wa jitu shujaa.

  • [Masaibu ya Ayubu hutazamwa kama hali iliyotendwa na Mungu, kwamba kile anachokiruhusu kimpate mwanadamu, kwa namna fulani Yeye ndiye akitendaye. Lakini hii haina maana kuwa Mungu hasa ndiye msababishi au mtekelezaji wa tendo hilo baya, bali katika ukweli kuwa katika hekima Yake ameruhusu (ijapokuwa anao uwezo wa kulizuia).]

15 Nimeshona nguo ya magunia juu ya mwili wangu, Na pembe yangu nimeidhili uvumbini.

  • -[Ishara ya nje ya maombolezo]_

16 Uso wangu umeharibika kwa kutoa machozi, Na giza tupu li katika kope zangu;

17 Ijapokuwa hapana jeuri mikononi mwangu, Na kuomba kwangu ni safi.

18 Ee nchi, usiifunike damu yangu, Na kilio changu kisipate mahali pa kupumzika.

19 Hata sasa, tazama, shahidi wangu yuko mbinguni. Na huyo atakayenidhamini yuko juu.

  • [Ayubu anakiri katika imani kwamba yuko Mungu Mbinguni aliye katika upande wake na kumtetea. “14 Basi, iwapo tunaye Kuhani Mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. 15 Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali Yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” Waebrania 4:14-16.]

20 Rafiki zangu hunidharau; Lakini jicho langu humwagia Mungu machozi;

21 Laiti angemtolea mtu hoja mbele ya Mungu, Amtetee na mwanadamu mbele ya jirani yake.

22 Kwani ikiisha pita miaka michache, Nitakwenda njia hiyo ambayo sitarudi tena.

  • [Mauti ni hatima ya yote; tumaini la Ayubu la ufufuo na maisha baada ya mauti linapatikana katika Ayubu 14:13-14; 19:25-27]

 

UFUPISHO WA AYUBU 16

Ayubu alilia sana kiasi kwamba kope zake zilikuwa giza tupu (aya ya 16). Licha ya yote haya, Ayubu hana ujeuri wowote moyoni mwake na maombi yake ni safi (aya ya 17). Mtetezi na Shahidi wa Ayubu yuko katika Patakatifu pa Mbinguni na anamdhamini Ayubu akiwa mahali pa juu (aya ya 19). Hicho ndicho ambacho nabii Mika vilevile aliona: “Bwana MUNGU na ashuhudie juu yenu, Yeye Bwana kutoka hekalu Lake takatifu.” Mika 1:2

Mtetezi huyu ni Mwombezi na Rafiki wa Ayubu. “Lakini jicho langu humwagia Mungu machozi” (aya ya 20). Musa na Ayubu waliujua ukweli wa Kristo aliye Haki yetu, Mtetezi wetu na Kuhani wetu Mkuu kwa niaba yetu mbinguni. Matendo yote ya Mungu huelekezwa kwetu kutoka Patakatifu pa Mbinguni; na matendo yetu yote yanapaswa kuelekezwa katika Patakatifu pa Mbinguni.

Ayubu anatamani iwapo pangelikuwepo na mwanadamu imara ambaye angelizungumza na Mungu kwa niaba yake kama mwanadamu azungumzavyo na rafiki yake (aya ya 21). Kristo alikusudia kufanya jambo hilo hasa! (rejea Danieli 7).


 

Mungu Mpendwa, Tunaishi katika jamii ya ulimwengu wa kisasa ambapo ukatili huonekana kupendwa, kutukuzwa, na kutetewa, kupendezeshwa, na hata kutakaswa. Tusaidie kujitenga mbali nao. Hebu maombi yetu yawe safi kama yalivyokuwa maombi ya Ayubu. Katika Jina la Yesu, Amina.