Ayubu 13

Kitabu cha Ayubu 13

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI:
Muhtasari  wa Ayubu 12:13-25. Kimsingi katika sura hii anasema: Tazama niko tayari kujua hoja Yako.

  1. Ayubu anajitetea dhidi ya shutuma za rafiki zake.
  2. Anawatazama kama watu wanaojaribu kuupindisha ukweli (Ayubu 13:1-8).
  3. Anawakumbusha juu ya hukumu za Mungu (Ayubu 13:9-12).
  4. Anatamani kama angelipata unafuu kutokana na hali yake.
  5. Anadhihirisha ujasiri na imani kubwa sana katika Mungu (Ayubu 13:13-19).
  6. Anamsihi Mungu, anahuzunika sana juu ya hali yake mbaya ya majaribu na mateso yasiyoelezeka (Ayubu 13:20-28).

 
1 Tazama, jicho langu limeyaona hayo yote, Sikio langu limeyasikia na kuelewa nayo.

2 Hayo myajuayo ninyi, na mimi pia nayajua; Mimi si duni kuliko ninyi.

3 Hakika ningenena naye huyo Mwenyezi, Nami nataka kuhojiana na Mungu.

  • [Tangu mwanzo, Ayubu amekuwa akimwangalia Mungu (linganisha Ayubu 9:3, 14-16, 19-20, 32-35).]

4 Lakini ninyi hubuni maneno ya uongo, Ninyi nyote ni matabibu wasiofaa.

  • [“Lakini ninyi mnaupakaa uongo chokaa; ninyi nyote ni waganga wasiofaa kitu” (Biblia Habari Njema).]

5 Laiti mngenyamaza kabisa! Hilo lingekuwa hekima kwenu.

6 Sikieni sasa basi hoja zangu, Mkayasikie mashindano ya midomo yangu.

7 Je! Mtanena yasiyo ya haki kwa ajili ya Mungu, Na kusema kwa udanganyifu kwa ajili yake?

8 Je! Mtamwonyesha yeye upendeleo? Mtamtetea Mungu?

9 Je! Itafaa yeye kuwatafuta ninyi? Au, kama kumdanganya mtu, je! Mtamdanganya yeye?

10 Hakika atawakemea ninyi, Mkiwapendelea watu kwa siri.

11 Je! Huo ukuu wake hautawatia hofu, Na utisho wake hautawaangukia?

12 Matamko yenu ya hekima ni mithali ya majivu, Ngome zenu ni ngome za udongo.

13 Nyamazeni, niacheni, ili nipate kunena, Na hayo yatakayonijilia na yaje.

14 Nitaitwaa nyama ya mwili wangu katika meno yangu, Na kuutwaa uhai wangu mkononi mwangu!

15 Tazama, ataniua; sina tumaini; ila hata hivyo nitaithibitisha njia yangu mbele yake.

  • [“Hata kama akiniua, bado nitamtumaini Yeye…” (NKJV). Licha ya yote ambayo Ayubu amepitia maishani mwake, anadumisha tumaini lake kwa Mungu wakati akiendelea katika uadilifu wake.]

16 Hili nalo litakuwa ni wokovu wangu; Kwani asiyemcha Mungu hatakaribia mbele yake.

17 Sikieni sana maneno yangu, Maelezo yangu na yaingie masikioni mwenu.

18 Angalieni sasa, nimekwisha kulitengeneza neno langu, Najua ya kuwa ni mwenye haki mimi.

19 Yuko nani atakayeshindana nami? Maana sasa nitanyamaa kimya na kutoa roho.

20 Lakini msinifanyie mambo mawili, hayo tu, Ndipo nami sitajificha usoni pako;

21 Uondoe mkono wako usinilemee; Na utisho wako usinitie hofu.

22 Basi uite wakati huo, nami nitaitika; Au, niache ninene mimi, nawe unijibu.

23 Maovu yangu na dhambi zangu ni ngapi? Nijulishe kosa langu na dhambi yangu.

24 Mbona umeuficha uso wako, Na kunihesabu kuwa ni adui yako?

25 Je! Utalitaabisha jani lipeperushwalo? Au, je! Utayafuatia hayo mabua makavu?

26 Kwani umeandika maneno ya uchungu juu yangu, Na kunirithisha maovu ya ujana wangu;

27 Waitia miguu yangu katika mkatale, na kuyaaua mapito yangu yote; Wajiandikia alama kuzizunguka nyayo za miguu yangu;

  • [“mkatale”—kifaa cha mbao kitukacho kumfungia miguu mhalifu gerezani. Ayubu anadokeza hapa kwamba hata hawezi kutembea.]

28 Nijapokuwa ni kama kitu kilichooza, kinachosinyaa, Mfano wa nguo iliyoliwa na nondo.


 

UFUPISHO WA AYUBU 13

Ayubu anamwomba Bwana amfanyie mambo mawili: Amwondolee maumivu yake na asiruhusu aogopeshwe na kweli juu ya Mungu (aya ya 20, 21). Mungu anamlinda Ayubu mikononi Mwake na amemzungushia neno la kweli. Mambo haya mawili yanapaswa kuwa vilevile hata kwetu pia. Hebu tuzungumze na Mungu: “Basi uite wakati huo, nami nitaitika; Au, niache ninene mimi, Nawe unijibu” (aya ya 22).

Ayubu anaendelea, akihitaji kufahamu maovu yake (aya ya 23). “Mbona umeuficha uso Wako, Na kunihesabu kuwa ni adui Yako?” (aya ya 24). Vitabu vya mbinguni vina kumbukumbu ya dhambi za Ayubu na Ayubu anajiuliza iwapo sasa anaadhibiwa kwa dhambi za ujanani mwake (aya ya 26).

Je, katika wakati huu wa hukumu ya upelelezi nimemwuliza Yesu anisamehe na kufutilia mbali dhambi zangu na kunifunika kwa Haki Yake?

Mungu Mpendwa, uzuri wa imani ya Ayubu hung’aa kila wakati, na kwetu sisi tuishio katika kipindi hiki cha mwisho wa historia ya ulimwengu, sisi pia tunakusihi kwamba uweze kutudhihirishia uasi wetu na wakati muda ungalipo tuwezeshe kutubu na kuachana nao. Katika Jina la Yesu Kristo, Amina.