Ayubu 12

Kitabu cha Ayubu 12

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Jibu la tatu la Ayubu kwa rafiki zake:

 1. Anasema Mungu ni Bwana, lakini rafiki hufanya makosa, ni wanadamu wenye ukomo.
 2. Ayubu anaonesha kuwa kujivuna kwa rafiki zake hakufai.
 3. Anaonyesha kwamba wanakosa kuwa na huruma kwa ajili yake (Ayubu 12:1-5);
 4. Anadai kwamba hata makazi ya wanyang’aji hustawi—kwa maneno mengine, sio wote wanaofanikiwa ni wenye haki (Mathayo 5:45),
 5. Na pia sio wote wanaoteseka wana hatia;
 6. Anasema pia kuwa, licha ya hilo, Mungu ndiye Mtawala Mkuu wa ulimwengu;
 7. Na huu ndio ukweli unaotangazwa na uumbaji Wake wote ama ni wanyama, mimea, viumbe hai wengine na visivyo hai,
 8. Na pia kwa mabadiliko ya uongozi yanayofanyika katika mataifa, nchi na falme za dunia (aya ya 6-25).

 
1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2 Hapana shaka ninyi ndinyi watu halisi, Nanyi mtakapokufa, ndipo na hekima itakoma.

 • [Ayubu anahuzunika sana kwa sababu ya ufidhuli wa kutojali kwa rafiki zake.]

3 Lakini mimi pia, nina fahamu kama ninyi; Mimi si duni yenu ninyi; Naam, ni nani asiyejua mambo kama hayo?

4 Mimi ni mtu wa kuchekwa na jirani yake, Ni mtu niliyemwita Mungu, naye akanijibu; Huyo mwenye haki, aliye mtimilifu, amekuwa ni kicheko.

 • [Ayubu anasikitika kwa sababu ya hali ya rafiki zake ya kukosa uaminifu.]

5 Katika mawazo yake huyo aliye na raha mna kudharau mashaka; Tayari kwa ajili ya wenye kuteleza miguu.

 • [Wale walio katika raha na amani huwadhihaki wale waliotaabani: “Mtu anayestarehe hudharau msiba; kwake [kwa mtazamo wake] msiba huwajia wale wanaoteleza [wanaoanguka maovuni]” (Biblia Habari Njema).]

6 Hema za wapokonyi hufanikiwa, Na hao wamkasirishao Mungu hukaa salama; Mikononi mwao Mungu huleta vitu vingi.

7 Lakini sasa waulize hao wanyama, nao watakufundisha; Na nyuni wa angani, nao watakuambia;

8 Au nena na nchi, nayo itakufundisha; Nao samaki wa baharini watakutangazia.

9 Katika hawa wote ni yupi asiyejua, Kwamba ni mkono wa Bwana uliofanya haya?

10 Ambaye nafsi ya kila kilicho hai i mkononi mwake, Na pumzi zao wanadamu wote.

11 Je! Sikio silo lijaribulo maneno, Kama vile kaakaa lionjavyo chakula?

12 Wazee ndio walio na hekima, Na katika kuishi siku nyingi iko fahamu.

13 Hekima na amri zina yeye Mungu; Yeye anayo mashauri na fahamu.

14 Tazama, yuavunja, wala haiwezekani kujenga tena; Humfunga mtu, wala haiwezekani kumfungua.

15 Tazama, yuayazuia maji, nayo yakatika; Tena, huyapeleka, nayo yaipindua dunia.

16 Kwake yeye ziko nguvu, na makusudi kufanikiwa; Huyo adanganywaye, na mdanganyi pia ni wake.

17 Yeye huwaondoa washauri hali wametekwa nyara, Naye huwafanya waamuzi kuwa ni wapumbavu.

18 Yeye hulegeza kifungo cha wafalme, Na kuwafunga viuno vyao kwa mshipi.

19 Yeye huwaondoa makuhani hali wametekwa nyara. Na kuwapindua mashujaa.

20 Huondoa matamko ya hao walioaminiwa, Na kuondoa fahamu za wazee.

 • [Mungu, “Mzee wa Siku,” si tu kwamba ana hekima yote, kuliko wote, lakini pia ndiye mwenye nguvu sana, Mtawala wa vyote, hata huwa juu zaidi ya mpangilio na mchafuko—ambalo kimsingi ni wazo la wale rafikize Ayubu.]

21 Humwaga aibu juu ya hao wakuu, Na kulegeza mshipi wa wenye nguvu.

22 Huvumbua mambo ya siri tokea gizani, Na hicho kilicho giza tupu huleta mwangani.

23 Huyaongeza mataifa, na kuyaangamiza; Huyaeneza mataifa mbali, na kuyaacha.

24 Huwaondolea moyo wakuu wa watu wa nchi, Na kuwapoteza nyikani pasipokuwa na njia.

25 Wao hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga, Naye huwafanya kupepesuka kama vile mlevi.


UFUPISHO WA AYUBU 12

Katika kumjibu Sofari, Ayubu anasema kuwa maarifa ya pekee na bora ya mwanadamu hutoka katika “mafunuo” ya Mungu. Kitabu cha “Education” uk. 154-156, Roho ya Unabii inasisitiza dhana hii kwa kina. Ayubu anadhihakiwa na rafiki zake kwa sababu mtazamo wao wa mambo huishia katika maisha ya hapa duniani tu, lakini Ayubu “Ni mtu niliyemwita Mungu, Naye [akamjibu]” (aya ya 4). Siri ya wokovu ni upumbavu kwa ulimwengu. Hata kama Mungu yuko juu kuliko uumbajiasili—jambo ambalo kwa kweli rafiki za Ayubu wanakiri kwa msisitizo wao katika ukuu wa Mungu—Ayubu anamdhihirisha Mungu afanyaye mahusiano binafsi na wanadamu na ambaye humjibu yule amwitaye Yeye (aya ya 4).

Waovu wanafanikiwa na wako salama kwa sababu wakati fulani Mungu anawaruhusu waendelee hivyo (aya ya 6). Ayubu anawahimiza rafiki zake wachunguze sayansi zote za wanyama—“ndege” (aya ya 7); “dunia” (aya ya 8); “bahari” (aya ya 8). Sayansi zote hizi hutuelekeza kwa Muumba kama anavyoonekana katika kitabu cha Mwanzo Sura ya 1. Na Ayubu anathibitisha hili kwa kusema, “Ambaye nafsi ya kila kilicho hai i mkononi Mwake, Na pumzi zao wanadamu wote” (aya ya 10; linganisha Mwanzo 2:7).

Mungu Mpendwa, tafadhali tupatie mtazamo mzuri wa mafunuo Yako ili tuweke mawazo yetu yote katika mwelekeo sahihi ili tuweze kushiriki maarifa na wokovu Wako katika ulimwengu huu, kwa ajili ya maandalizi ya ule ujao. Katika Jina la Yesu, Amina!