Ayubu 10

Kitabu cha Ayubu 10

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI:

  1. Ayubu anaonekana kuwa na fadhaa kubwa kwa sababu ya hali yake (Ayubu 10:15),
  2. Anaonesha hali yake jinsi isivyokuwa na matumaini kwa yenyewe (Ayubu 10:1-7),
  3. Kisha anapata faraja kutokana na ukweli kuwa yu Mkononi mwa Mungu aliyemwumba (Ayubu 10:8-13).
  4. Anaonesha jinsi Mungu alivyoruhusu akabiliane na mateso makali (Ayubu 10:14-17),
  5. Kisha tena anapata faraja kwamba kutakuwa na mwisho wa masaibu haya yote (Ayubu 10:18-22).

 
1 Nafsi yangu inachoka na maisha yangu; Sitajizuia na kuugua kwangu; Nitanena kwa uchungu wa roho yangu.

2 Nitamwambia Mungu, Usinihukumie makosa; Nionyeshe sababu ya wewe kushindana nami.

3 Je! Ni vema kwako wewe kuonea, Na kuidharau kazi ya mikono yako, Na kuyaangazia mashauri ya waovu?

4 Je! Wewe una macho ya kimwili, Au je! Waona kama aonavyo binadamu?

5 Je! Siku zako ni kama siku za mtu, Au je! Miaka yako ni kama siku za mtu,

6 Hata ukauliza-uliza habari za uovu wangu, Na kuitafuta dhambi yangu,

7 Ujapojua ya kuwa mimi si mwovu; Wala hapana awezaye kuokoa na mkono wako?

8 Mikono yako imeniumba na kunifinyanga; Nawe utageuka na kuniangamiza?

9 Kumbuka, nakusihi ulivyonifinyanga kama vile udongo; Nawe, je! Utanirudisha uvumbini tena?

10 Je! Wewe hukunimimina kama maziwa, Na kunigandisha mfano wa jibini?

11 Umenivika ngozi na nyama, Na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa.

12 Umenijazi uhai na upendeleo, Na maangalizi yako yameilinda roho yangu.

13 Lakini mambo haya uliyaficha moyoni mwako; Najua kuwa haya yamo nafsini mwako;

14 Nikifanya dhambi, ndipo waniangalia, Wala hutaniachilia na uovu wangu.

15 Mimi nikiwa mbaya, ole wangu! Nami nikiwa mwenye haki, walakini sitainua kichwa changu; Mimi nimejaa aibu Na kuyaangalia mateso yangu.

16 Kichwa changu kikijiinua, waniwinda kama simba; Tena wajionyesha kwangu kuwa wa ajabu.

17 Wewe warejeza upya hao mashahidi yako juu yangu, Na kasirani yako waiongeza juu yangu; Jeshi kwa jeshi juu yangu.

18 Kwa nini basi kunitoa tumboni? Ningekata roho, lisinione jicho lo lote.

19 Ningalikuwa kama mtu asiyekuwapo; Ningalichukuliwa kaburini kutoka tumboni.

20 Je! Siku zangu si chache? Acha basi, Usinisumbue, nipate ngaa kutuzwa moyo kidogo.

21 Kabla sijaenda huko ambako sitarudi kutoka huko tena, Ni hiyo nchi ya giza, giza tupu;

22 Ni nchi ya giza kuu, kama giza lenyewe lilivyo; Ni nchi ya giza tupu, isiyo na matengezo ya mambo yo yote, Nchi ambayo nuru yake ni kama giza.


UFUPISHO WA AYUBU 10

Ayubu anafahamu kuwa anao uhusiano pamoja na Mungu na kwamba yuko salama mikononi Mwake. “Ujapojua ya kuwa mimi si mwovu; Wala hapana awezaye kuokoa na mkono wako” (aya ya 7). Ayubu yu salama mikononi mwa Mungu kwa sababu Yeye ni Muumba wake: “Kumbuka, nakusihi ulivyonifinyanga kama vile udongo; Nawe, je! Utanirudisha uvumbini tena?” (aya ya 9; Mwanzo 2:7). Mungu ndiye aliyemwumba Ayubu na kumpulizia pumzi ya uhai, akamhuluku kwa silka, wema, na roho—uwezo wa kufanya uhusiano pamoja na Mungu (aya ya 12). Ayubu amefichwa moyoni mwa Mungu (aya ya 13).

Katika aya ya 20 Ayubu anaomba apewe ahueni katika maisha yake. Maisha yake yanaweza kuwa na siku chache, na endapo mateso haya yakiondolewa kwa muda kitambo anaweza kuwa na wakati fulani wa faraja kabla hatima yake ya mwisho katika nchi ya giza na vivuli haijawadia (aya ya 21, 22).

Mungu Mpendwa, sisi vilevile tunatulia katika moyo Wako na akili Yako na Mkono Wako. Kristo ndiye Mtetezi wetu katika hukumu. Tafadhali Bwana tupatie roho kama ile ya Ayubu kwa maana hata mateso yetu yako mkononi Mwako na moyoni Mwako. Katika Jina la Yesu. Amina!