Ayubu 8

Kitabu cha Ayubu 8

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Mazungumzo ya kwanza ya Bildadi kuhusiana na mkasa wa Ayubu.

  1. Bildadi anajibu, akimkaripia Ayubu kwamba anadai kutokuwa na makosa (Ayubu 8:1, 2).
  2. Anaonesha kwamba mateso humpata tu yule mwovu na huadhibiwa kwa sababu ya udhalimu wake (Ayubu 8:3, 4);
  3. Anadokeza kuwa ni kwa sababu ya dhambi zao, ndiyo maana watoto wake walikufa. Anaonesha jinsi waovu wanavyoweza kuadhibiwa muda si mrefu na kutoweka kwa tumaini la wadhalimu (Ayubu 8:8-19).
  4. Anadai kuwa kamwe Mungu hajawahi kumtupa mtu mkamilifu wala kumsaidia mwovu, na kwamba endapo Ayubu hana hatia mwisho wake utavikwa kwa fanaka (Ayubu 8:20-22).

1 Ndipo Bildadi huyo Mshuhi akajibu, na kusema,

2 Wewe utanena maneno haya hata lini? Maneno ya kinywa chako yatakuwa kama upepo mkuu hata lini?

3 Je! Mungu hupotosha hukumu? Au, huyo Mwenyezi hupotosha yaliyo ya haki?

4 Kwamba watoto wako wamemfanyia dhambi, Naye amewatia mkononi mwa kosa lao;

5 Wewe ukimtafuta Mungu kwa bidii, Na kumsihi huyo Mwenyezi;

6 Ukiwa wewe u safi na mwelekevu; Hakika yeye sasa angeamka kwa ajili yako, Na kuyafanya makazi ya haki yako kufanikiwa.

7 Tena ujapokuwa huo mwanzo wako ulikuwa ni mdogo, Lakini mwisho wako ungeongezeka sana.

  • [Hapa Bildadi, kama ilivyokuwa kwa Elifazi (Ayubu 4:6), anazungumza kwa usahihi kuliko ajuavyo.]

8 Basi, uwaulize, tafadhali, vizazi vya zamani, Ujitie kuyaangalia yale baba zao waliyoyatafuta;

9 (Kwani sisi tu wa jana tu, wala hatujui neno, Kwa kuwa siku zetu duniani ni kivuli tu;)

10 Je! Hawatakufunza wao, na kukueleza, Na kutamka maneno yatokayo mioyoni mwao?

11 Je! Hayo mafunjo yamea pasipo matope Na makangaga kumea pasipo maji?

12 Yakiwa yakali mabichi bado, wala hayakukatwa, Hunyauka mbele ya majani mengine.

13 Ndivyo ulivyo mwisho wa hao wamsahauo Mungu; Na matumaini yake huyo mbaya huangamia;

14 Uthabiti wake utavunjika, Na matumaini yake huwa ni nyuzi za buibui.

15 Ataitegemea nyumba yake, isisimame; Atashikamana nayo, isidumu.

  • [Tumaini la wasiohaki halidumu kama ulivyo utando wa buibui.]

16 Yeye huwa mti mbichi mbele ya jua, Nayo machipukizi yake huenea katika bustani yake.

  • [Waovu huonekana kustawi tu lakini kihalisia, muda kitambo watangamizwa na hakuna chembechembe yao itakayosalia.]

17 Mizizi yake huzonga-zonga chuguu, Huangalia mahali penye mawe.

18 Lakini, aking’olewa mahali pake, Ndipo patamkana, na kusema, Mimi sikukuona.

  • [Matumizi ya kanuni ya maswali ya balagha (rhetorical quetions) katika aya ya 11—kwamba mafunjo na makangaga (mimea ya majini) hukauka haraka ikikoswa maji; kwa hiyo wasiohaki lazima watoweke. Bildadi anamweka Ayubu katika kundi la wasiohaki.]

19 Tazama, furaha ya njia yake ni hii, Na wengine watachipuka kutoka katika nchi.

20 Tazama, Mungu hatamtupa mtu mkamilifu, Wala hatawathibitisha watendao uovu.

  • [Muhtasari wa mustakabali wa wema na wovu: mkamilifu hatatupwa (ataokolewa), waovu hawatathibitika (watapatikana na hatia—wataangamizwa).]

21 Bado atakijaza kinywa chako kicheko, Na midomo yako ataijaza shangwe.

22 Hao wakuchukiao watavikwa aibu; Nayo hema yake mwovu haitakuwako tena.


 

UFUPISHO WA AYUBU 8

Katika sura hii, Bildadi Mshuhi anazungumza. Hayuko hapo ili kumsaidia Ayubu bali kuutetea mtazamo wake mwenyewe wa mambo. Bildadi anazungumza ukweli nusu uliosukwa kwenye makosa. Alikuwa anafahamu kile kilichogunduliwa na “mababa” wa zamani na kuandikwa na Musa katika Mwanzo 1-11 (aya ya 8-10). Kwa hiyo anamwambia Ayubu asiangalie katika historia, bali pia awe radhi kuongozwa na kweli zitokanazo na mitazamo (aya ya 8).

Ushauri wa Bildadi una mdokezo uonekanao kana kwamba ni mzuri sana, lakini kwa kuzingatia Ayubu 18, ambayo tutaiona baadaye, ni dhahiri kwamba anajaribu kuyafanya mambo yatakayotokea wakati ujao kuwa ya sasa. Fikra kama hizo ni matokeo ya mtu anayetaka tu kuishi kwa kuzingatia kile aonacho, na anayedhani kuwa anaufahamu ukweli wote bila kuzingatia historia ya Uasi Mbinguni.

Mungu Mpendwa, Musa alituainishia hatari kuendelea kushikilia kanuni za ghiliba katika ulimwengu huu na kujenga katika msingi usio imara. Hili linaweza kusababisha hiana ya Shetani na mashambulizi yake katika maisha yetu. Tafadhali tuokoe toka kwa akina Bildadi wa wakati wetu huu. Katika Jina la Yesu. Amina!