Ayubu 5

Kitabu cha Ayubu 5

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI:

  1. Elifazi anaendelea kuonesha kuwa daima waovu huadhibiwa kwa haki ya Mungu, ingawa wanaweza kuonekana kustawi kwa muda fulani (Ayubu 5:1-8).
  2. Huinua na kusifu kudra au majaliwa ya Mungu, ambayo kwayo mashauri ya waovu hutoweshwa, na maskini huwandishwa (Ayubu 5:9-16).
  3. Huonesha baraka ya kurudiwa (rekebishwa) na Mungu, katika matunda bora ambayo ni matokeo yake.
  4. Anamsihi Ayubu awe na subira na kujisalimisha, pamoja na ahadi ya mafanikio yote ya kidunia, na mwisho wenye furaha (Ayubu 5:17-27).

 
1 Haya, ita sasa; je! Yuko atakayekujibu? Nawe utamwelekea yupi katika hao watakatifu?

  • [“watakatifu”—rejea pia Mwanzo 15:5; Danieli 4:17; 7:18-27; 8:24.]

2 Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga.

3 Nimewaona wapumbavu wakishusha mizizi; Lakini mara niliyalaani maskani yake.

  • [Waovu, wajinga na wapumbavu wanaelekea katika uangamivu (Ayubu 4:8; 5:2; Mithali 10:14; 11:29).]

4 Watoto wake wako mbali na wokovu, Nao wamesongwa langoni, Wala hapana atakayewaponya.

5 Mavuno yake wale wenye njaa huyala, Na kuyatwaa hata kuyatoa miibani, Nao wenye kiu huzitwetea mali zao.

  • [“Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili. Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.” Mithali 24:30-31]

6 Kwani taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi;

7 Lakini mwanadamu huzaliwa ili apate mashaka, Kama cheche za moto zirukavyo juu.

8 Lakini mimi ningemtafuta Mungu, Ningemwekea Mungu daawa yangu;

9 Yeye afanyaye mambo makuu, yasiyotambulikana; Mambo ya ajabu yasiyo na hesabu;

10 Yeye atoaye mvua inyeshe juu ya nchi, Na kuyapeleka maji mashambani;

11 Awainuaye juu hao walio chini; Na hao waombolezao hukuzwa wawe salama.

12 Yeye huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao.

  • [“Kisha ikawa, adui zetu waliposikia ya kuwa tumekwisha kupata habari, na ya kuwa Mungu amelibatilisha shauri lao, ndipo sisi sote tukarudi ukutani, kila mtu kwa kazi yake.” Nehemia 4:15]

13 Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao wenyewe; Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka.

14 Wao hupatwa na giza wakati wa mchana, Hupapasa mchana vilevile kama usiku.

15 Lakini yeye huokoa na upanga wa kinywa chao, Hata kumwokoa mhitaji na mkono wake aliye hodari.

16 Basi hivi huyo maskini ana matumaini, Na uovu hufumba kinywa chake.

  • [Matumaini kwamba udhalimu na uonevu vitakwisha: “Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.” Zaburi 107:42.]

17 Tazama, yu heri mtu yule Mungu amwadhibuye; Kwa hiyo usidharau kurudiwa na huyo Mwenyezi.

18 Kwani yeye huumiza, lakini tena huuguza; Yeye hutia jeraha, na mikono yake huponya.

19 Yeye atakuokoa na mateso sita; Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa.

  • [“mateso sita; Naam, hata katika saba”—yaani kadiri inavyohitajika (Ayubu 33:14, 29).]

20 Wakati wa njaa atakukomboa na mauti; Na vitani atakukomboa na nguvu za upanga.

21 Utafichwa na mapigo ya ulimi; Wala usiogope maangamizo yatakapokuja.

22 Wewe utayacheka maangamizo na njaa; Wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi.

23 Kwani utakuwa na mapatano na mawe ya bara; Nao wanyama wa bara watakuwa na amani kwako.

24 Nawe utajua ya kwamba hema yako ina salama; Na zizi lako utaliaua, wala usikose kitu.

25 Tena utajua ya kwamba uzao wako utakuwa mwingi, Na vizazi vyako watakuwa kama nyasi za nchi.

26 Utafika kaburini mwenye umri mtimilifu, Kama mganda wa ngano ulivyo wakati wake.

27 Tazama, haya tumeyapeleleza, ndivyo yalivyo; Yasikie, uyajue, ili upate mema.


 

UFUPISHO WA AYUBU 5

Elifazi anafikiri kwamba tatizo la Ayubu hutokana na Ayubu mwenyewe. “Upandacho ndicho uvunacho,” ndilo wazo lake kuu. Kwa hiyo anadai kuwa hakuna haja ya Ayubu kutafuta msaada wa Mungu (aya ya 1-5).

Siyo sehemu ya uwezo wa dunia kuleta uovu. Katika aya ya 7, Elifazi anazungumza juu ya malaika wakija na kuleta taabu kisha wakaruka tena kwenda juu. Kwa sababu hii, kuna haja ya kumtafuta Mungu (aya ya 8), ambaye ndiye Mtawala Mkuu (aya ya 11-12) na Yeye hufanya kama apendavyo hata kama ni uangamivu wa viumbe Wake, akivifanya kama vitu visivyokuwa na maana. Kama anataka kuviharibu, nani atakayemzuia? Mtazamo huu juu ya Ukuu wa Mungu sio wa Biblia na hupoteza kabisa ufunuo wa upendo wa Mungu.

Elifazi anakosa uwezo wa kuyaelewa mambo—mtazamo sahihi wa Biblia. Hapa kuna dhana mbili kinzani: ile ya kujitolea nafsi kwa upande mmoja, na ile ya “kula na kunywa, kwa kuwa kesho twafa” kwa upande mwingine, ndiyo tofauti kati ya mtazamo wa Ayubu na Elifazi.

Mungu Mpendwa, tunakugeukia ili kupata mahitaji yetu yote, siyo kwa sababu tunataka kuunda mbingu yetu wenyewe hapa duniani, bali kwa sababu tunaliweka tumaini letu Kwako, kwa ajili ya siku ya leo na kwa ajili ya wakati ujao. Katika Jina la Yesu. Amina!