Ayubu 3

Kitabu cha Ayubu 3

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI:
Kilio cha kwanza cha maombolezo ya Ayubu kutokana na hali yake ya taabu.

  1. Ayubu analaani siku ya kuzaliwa kwake. Ayubu 3:1-12.
  2. Anaelezea hali ya ulimwengu wa mauti.  Ayubu 3:13-19.
  3. Anaombolezea hali yake ya taabu, majanga yaliyokuwa yamemghubika. Ayubu 20-26.

 
1 Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake.

  • [Bila kutumia vibaya jina la Mungu, isipokuwa akidokeza kwamba kuzaliwa kwake ndiko kumesababisha yeye kuwepo katika hali yake ya sasa.]

2 Ayubu akajibu, na kusema;

3 Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba.

4 Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie.

5 Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe.

6 Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi.

7 Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe.

8 Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo lewiathani.

  • [“lewiathani”—Lewiathani, mnyama wa baharini anawakilisha nguvu ya uovu ambao Mungu pekee ndiye angeweza kuuzuia (Ayubu 41; Zaburi 74:14; 104:26; Isaya 27:1). Maneno haya huonesha kuwa Ayubu yuko katika hali mbaya sana kwa sababu ya taabu yake.]

9 Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone makope ya asubuhi;

10 Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni.

  • [Sulemani, mwandishi wa kitabu cha Mhubiri, alisema maneno ambayo kimsingi yanakaribiana na hayo ya Ayubu: “Kwa hiyo nikawasifu wafu waliokwisha kufa kuliko wenye uhai walio hai bado; naam, zaidi ya hao wote nikamwita heri yeye asiyekuwako bado, ambaye hakuyaona mabaya yanayotendeka chini ya jua. Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo.” Mhubiri 4:2-4.]

11 Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni?

12 Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya?

  • [“magoti”—magoti ya mama na babaye (angalia Mwanzo 50:23).]

13 Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika;

14 Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni;

15 Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza fedha nyumba zao;

16 Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa.

17 Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wapumzika

18 Huko wafungwa waona raha pamoja; Hawaisikii sauti yake msimamizi.

19 Wakuu na wadogo wako huko; Mtumishi yu huru kwa bwana wake.

  • [Kifo kinaonekana kuwa nafuu kwake.]

20 Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai;

21 Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika;

22 Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi?

23 Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo?

  • [Ayubu ambaye hapo awali alionekana kana kwamba alikuwa akipokea ulinzi wa Mungu, sasa anajisikia kama vile “amemzingira” asiepuke mateso yake ya sasa.]

24 Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji.

25 Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia.

26 Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini huja taabu.


 

UFUPISHO WA AYUBU 3

Katika sura hii na kuendelea, Ayubu anaanza kutafakari juu ya hali yake. Wakati huohuo, Shetani anawatumia rafiki zake ili kuendeleza mashambulizi yake. Ayubu anajiuliza kwa nini Mungu hauzuii uovu huu ingawa hamlaumu Mungu.

Zamani katika nchi ya Uyunani, majukwaa kwa ajili ya michezo yalikuwa yakijengwa kwa sakafu tatu katika ngazi tatu: sehemu ya juu kwa ajili ya mbingu, chini kabisa kwa ajili ya ulimwengu chini ya ardhi, na katikati kwa ajili ya maisha ya kila siku. Hadhira ilikuwa inaweza kuona kabisa kila kitu kwa sababu wangeliweza kuona nguvu za ulimwengu wa roho kwa juu zikiigizwa na pia kwa chini na athari za nguvu hizo kwa maisha ya kila siku (katika sehemu ya kati).

Kitabu cha Ayubu kiliandikwa ili kutupatia mtazamo wa utendaji huo katika sehemu ya juu na matokeo yake katika maisha ya kila siku upande wa chini. Maumivu makali ya Ayubu yalitokana na ukosefu wa maarifa kamili kuhusu mipango ya hila ya kiongozi wa Uasi Mbinguni. Lakini, sisi, wasomaji, tumefahamishwa vilivyo, kiasi cha kutosha, na tunaweza kuiona kila kitu.

Mungu Mpendwa, tunaishi na majanga ya kila siku na misukosuko inayotuzunguka na kutukabili sisi. Asante kwa ajili ya historia hii aliyoiandika Musa juu ya maisha ya Ayubu, akituarifu jinsi ya kushughulikia mateso na maumivu katika maisha yetu. Katika Jina la Yesu. Amina!