Ayubu 2

Kitabu cha Ayubu 2

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI:

  1. Kwa mara nyingine tena wana wa Mungu wanajihudhurisha mbele Yake; na Shetani anakuja pia, akimshutumu Ayubu kama mtu ambaye uimara wake wa kiroho ungelitikiswa muda si mrefu, kama mwili wake ungelikabiliwa na mateso makali, Ayubu 2:1-5.
  2. Anapewa ruhusa ya kumgusa Ayubu, 2:6-8.
  3. Mkewe anamkejeli, Ayubu 2:9.
  4. Karipio lake la kitauwa, Ayubu 2:10.
  5. Rafiki zake 3 wanakuja kumtembelea na kuomboleza pamoja naye, Ayubu 2:11-13.

 
1 Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhurisha mbele za Bwana.

  • [“Shetani naye akaenda kati yao”—hali ya kustaajabisha ya kwenda kwa Shetani katika uwepo wa Mungu (1:6) huoneshwa kwa mrudio wa maneno, “kujihudhurisha mbele za Bwana.”]

2 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.

3 Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu.

4 Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake.

  • [“Ngozi kwa ngozi”—Maneno haya hudokeza biashara ya ngozi ya mnyama mmoja kwa ajili ya ile ya mnyama mwingine. Kwa mtazamo wa Shetani, Ayubu angelikuwa radhi kumtoa mkewe (mpendwa wake pekee aliyebaki) ili kuyaokoa maisha yake, na kwa namna hiyo kusalimisha uadilifu wake (aya ya 3). Shutuma ya Shetani ni kuwa Ayubu hajajaribiwa kwa sababu nafsi yake imelindwa.]

5 Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.

6 Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake.

7 Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa.

  • [“majipu mabaya”—ugonjwa mbaya wa ngozi usiotamanika kutazamwa.]

8 Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni.

9 Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe.

  • [“Umkufuru Mungu, ukafe”—kama hili lingefanyika, hoja ya shitaka la Shetani ingethibitishwa. Wazo hili la mkewe hutokana na mfadhaiko badala ya nia mbaya juu yake.]

10 Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.

  • [“Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake”—ni dhahiri hapa kuwa tabia, mamlaka na uadilifu ni sifa zinazoathiriwa pia na midomo—maneno (Ayubu 11:5; 23:12). “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake” (Mithali 18:21)]

11 Basi ikawa hao rafikize Ayubu watatu walipopata habari ya mabaya hayo yote yaliyomfikilia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili waende kumlilia Ayubu na kumtuliza moyo.

12 Basi walipovua macho yao, nao wakali mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho yake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni.

13 Kisha wakaketi nchi pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lo lote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.


UFUPISHO WA AYUBU 2

Tangu Shetani ajitwalie sayari hii, ikawa kama kondoo pekee aliyepotea ulimwenguni. Mungu alipomwuliza Shetani alikotokea alisema, “Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.” Alikuwa kwenye juhudi kubwa zisizokoma katika kubuni uovu na majanga, siyo tu kwa Ayubu bali pia kwa jamii nzima ya wanadamu.

Mungu alijivunia Ayubu na akamwuliza Shetani iwapo alikuwa ametafakari juu ya “huyo mtumishi Wangu Ayubu? Kwa kuwa [ni]… mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake” (aya ya 3). Hebu jiweke katika hali ya Ayubu kisha jifunze kutokana na uzoefu wake. Mungu anamruhusu Shetani amkabili Ayubu, lakini kamwe hamwachi mtumishi Wake. Ukweli ni kwamba, Mungu angelimtuma Mwanawe aje na kumfia Ayubu ili aweze kuishi, kitendo ambacho amekifanya kwa ajili ya kila mmoja wetu ili tuweze kuishi. Na watoto wote wa Mungu pamoja na malaika walioasi wataona upendo wa Mungu na kushangilia kwa furaha.

Mungu Mpendwa, wapo watu wengi sana wasio na hatia wanaoteseka na Wewe pekee ndiwe ujuaye kikamilifu sababu ya hilo kutokea. Lakini unajua pia kuwa hakuna chochote kinacholingana na baraka na thawabu ambazo Wewe utawapatia waaminifu wote utakapokuja na hata baada ya hapo. Kwa hiyo tafadhali Bwana tujuimuishe nasi pia kuwa miongoni mwa washirika katika Ufalme Wako wa Neema. Katika Jina la Yesu, Amina.