Ayubu 1

Kitabu cha Ayubu 1

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Katika sura hii kunadhihirisha onesho la ajabu la kisa cha Ayubu.

 1. Tabia ya Ayubu, Ayubu 1:1.
 2. Familia Yake, Ayubu 1:2.
 3. Mali Zake, Ayubu 1:3.
 4. Uangalizi wa Familia Yake  Ayubu 1:4, 5.
 5. Shetani anamshutumu Ayubu kuwa anamtumikia Mungu kwa nia binafsi ya kujipatia mali na mafanikio, Ayubu 1:6-11.
 6. Shetani anaruhusiwa kuangamiza mali na watoto wa Ayubu, Ayubu 1:12-19.
 7. Sifa kuu ya kustaajabisha ya Ayubu ya kukubali kwa utulivu na uvumilivu hali hiyo, Ayubu 1:20-22.

1 Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.

 • [Ayubu hakuwa Mwisraeli ingawa alikuwa mfuasi wa Mungu, alikuwa Mwedomu (nasaba moja na uzao wa Esau, nduguye Yakobo). Nchi ya Usi ilikuwa na eneo kubwa mashariki mwa Bonde la Yordani ambalo lilihusisha eneo la kusini mwa Edomu.]

2 Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu.

3 Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng’ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.

4 Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao.

5 Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu siku zote.

6 Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.

7 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.

8 Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.

 • [“huyo mtumishi wangu Ayubu”—Mungu anajivunia Ayubu, mtumishi Wake mwaminifu.]

9 Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure?

10 Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.

 • [“Wewe hukumzingira kwa ukigo [boma, wigo] pande zote”—kutokana na nia dhahiri la kumwangamiza Ayubu, Shetani anapotosha wema wa Mungu.]

11 Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.

12 Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana.

13 Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa,

14 mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng’ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao;

15 mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.

16 Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.

17 Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.

18 Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa;

19 mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.

20 Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia;

21 akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe.

 • [Mashambulizi ya Shetani ya maangamizi hayabadilishi uaminifu wa Ayubu.]

22 Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.


UFUPISHO WA AYUBU 1

Shetani alikuwa na uwezo wa kumwendea Kristo kabla ya tukio la kifo Chake msalabani, lakini si baada ya hapo (rejea kitabu cha “Story of Redemption,” uk. 26). Katika kitabu cha Ayubu, kusudi la Shetani lilikuwa kutoa taarifa za sifa na hatia za viumbe wa Mungu. Pale Mwana wa Mungu alipomwuliza Shetani endapo alimwona Ayubu na ukamilifu wake (aya ya 8), jibu lilikuwa ovu. Shetani hazingatii wala kuvutiwa na mambo mema. Alimshutumu Mungu kwa sababu ya uaminifu wa Ayubu, kwamba alimbariki na kumtukuza (aya ya 10) na akaomba nafasi ya kumwangusha.

Shetani anahitimisha kuwa Ayubu atamwacha Mungu endapo mambo yatabadilika na kumwendea vibaya. Baada ya majanga makubwa manne kutokea, kwa mshtuko Ayubu alifanya mambo 6: aliinuka, akayararua mavazi yake, kisha akanyoa nywele kichwani pake, akaanguka chini, akasujudia, kisha akazungumza na kumbariki Mungu. Mungu alipendezwa kwa jambo hili. Shetani hakuvutiwa. Ayubu hakutenda dhambi na wala hakumlaumu Mungu.

Mungu Mpendwa, Wewe ndiwe umetuagizwa kuomba “usitutie majaribuni” kwa hiyo sasa tunajua sababu yake. Tafadhali tupatie ustahimilivu wa Ayubu ili kusema katika wakati wa mafanikio na taabu, “Abarikiwe Mungu wangu.” Katika Jina la Yesu, Amina.