Nehemia 11

Kitabu cha Nehemia 11

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii inahusisha orodha nyingine inayounganika moja kwa moja na 7:4, 73. Baada ya maungamo na agano kufanyika, sasa ni wakati wa kuujaza (watu) Mji wa Yerusalemu. Asilimia kumi ya jamii iliyokuwa ikizunguka inachaguliwa kwa kura ili kuishi ndani ya Yerusalemu. Orodha hii imegawanyika kama kawaida: makuhani (aya ya 10-14), Walawi (aya ya 15-18), walinzi (aya ya 19), watu wengine.


 

1 Basi, wakuu wa watu walikuwa wakikaa Yerusalemu; nao watu waliosalia wakapiga kura, ili katika watu kumi kumleta mmoja akae ndani ya Yerusalemu mji mtakatifu, na wale kenda wakae mijini.

2 Na hao watu wakawabariki wote waliojitoa kwa hiari wakae Yerusalemu.

3 Basi hawa ndio wakuu wa jimbo waliokaa Yerusalemu; ila mijini mwa Yuda wakakaa kila mtu katika milki yake mijini mwao, yaani, Israeli, makuhani, na Walawi, na Wanethini, na akina watumwa wa Sulemani.

4 Tena wakakaa Yerusalemu wengine wa wana wa Yuda, na wengine wa wana wa Benyamini. Wa wana wa Yuda; Athaya, mwana wa Uzia, mwana wa Zekaria, mwana wa Amaria, mwana wa Shefatia, mwana wa Mahalaleli, wa wana wa Peresi;

5 na Maaseya, mwana wa Baruki, mwana wa Kolhoze, mwana wa Hazaya, mwana wa Adaya, mwana wa Yoyaribu, mwana wa Zekaria, Mshelani.

6 Wana wa Peresi wote waliokaa Yerusalemu walikuwa watu mia nne sitini na wanane, mashujaa.

7 Na wana wa Benyamini ndio hawa; Salu, mwana wa Meshulamu, mwana wa Yoedi, mwana wa Pedaya, mwana wa Kolaya, mwana wa Maaseva, mwana wa Ithieli, mwana wa Yeshaya.

8 Na baada yake Gabai, Salai, watu mia kenda ishirini na wanane.

9 Na Yoeli, mwana wa Zikri, alikuwa msimamizi wao; na Yuda, mwana wa Hasenua, alikuwa wa pili juu ya mji.

10 Wa makuhani; Yedaya, Yoyaribu, Yakini,

11 na Seraya, mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu, msimamizi wa nyumba ya Mungu,

12 na ndugu zao waliofanya kazi ya nyumbani, watu mia nane ishirini na wawili; na Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pelalia, mwana wa Amzi, mwana wa Zekaria, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya,

13 na ndugu zake, wakuu wa mbari za mababa, watu mia mbili arobaini na wawili; na Maasai, mwana wa Azareli, mwana wa Azai, mwana wa Meshilemothi, mwana wa Imeri,

14 na ndugu zao, waume mashujaa, watu mia na ishirini na wanane; na msimamizi wao alikuwa Zabdieli, mmojawapo wa hao wakuu.

15 Na wa Walawi; Shemaya, mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, mwana wa Buni;

16 na Shabethai na Yozabadi, wa wakuu wa Walawi, walioisimamia kazi ya nje ya nyumba ya Mungu;

17 na Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zikri, mwana wa Asafu, mkuu mwenye kuanzisha shukrani katika sala, na Bakbukia, wa pili wake miongoni mwa nduguze; na Obadia, mwana wa Shemaya, mwana wa Galali, mwana wa Yeduthuni.

18 Walawi wote waliokaa katika mji mtakatifu walikuwa watu mia mbili themanini na wanne.

19 Pamoja na hao, mabawabu; Akubu, Talmoni, na ndugu zao waliolinda malangoni, walikuwa watu mia na sabini na wawili.

20 Na Israeli waliosalia, katika hao makuhani, na Walawi, walikuwamo mijini mwote mwa Yuda, kila mtu katika milki yake.

21 Lakini Wanethini walikuwa wakikaa Ofeli; na juu ya Wanethini walikuwa Siha na Gishpa.

22 Naye msimamizi wa Walawi huko Yerusalemu, ni Uzi, mwana wa Bani, mwana wa Hashabia, mwana wa Matania, mwana wa Mika, wa wana wa Asafu, hao waimbaji, alikuwa juu ya kazi ya nyumba ya Mungu.

23 Kwa kuwa palikuwa na amri ya mfalme juu yao, na agizo la hakika walilowekewa waimbaji, kama ilivyohusika na kila siku.

24 Na Pethahia, mwana wa Meshezabeli, wa wana wa Zera, mwana wa Yuda, alikuwa wakili wa mfalme kwa habari ya mambo yote ya watu.

25 Na katika habari za vijiji na mashamba yake; wengine wa wana wa Yuda walikuwa wakikaa Kiriath-arba na vijiji vyake, na katika Diboni na vijiji vyake, na Yekabzeeli na vijiji vyake;

26 na katika Yeshua, na Molada, na Beth-peleti;

27 na Hazar-shuali, na Beer-sheba na vijiji vyake;

28 na katika Siklagi, na Mekona na vijiji vyake;

29 na katika Enrimoni, na Sora, na Yarmuthi;

30 Zanoa, Adulamu na vijiji vyake, Lakishi na mashamba yake, Azeka na vijiji vyake. Hivyo wakatua toka Beer-sheba mpaka bonde la Hinomu.

31 Wana wa Benyamini nao walikuwa wakikaa Geba, na Mikmashi, na Aiya, na Beth-eli na vijiji vyake;

32 Anathothi, Nobu, Anania;

33 Hazori, Rama, Gitaimu;

34 Hadidi, Seboimu, Nebalati;

35 Lodi, na Ono, bonde la Wakarashi.

36 Na wa Walawi, wengine walikaa katika Yuda na wengine katika Benyamini.


 

UFUPISHO WA NEHEMIA 11

Mungu alimwagiza Musa amjengee Patakatifu ili aweze kukaa miongoni mwa watu Wake (Kutoka 25:8). Kwa nini, basi, watu wasingechagua kukaa mahali lilipokuwa Hekalu ili waweze kuwa karibu na uwepo wa Mungu (aya ya 1-2)? Kukiwa na kuta zilizolizunguka, sasa ilikuwa salama zaidi kuishi ndani ya Yerusalemu kuliko nje. Kwa hiyo, kwa nini watu wasimiminike kwa wingi ili waishi ndani?

Jambo la kutafakari:

  • (1) Je, inawezekana kuwa kuishi karibu zaidi na uwepo wa Mungu kuliwalazimu watu wafuate mtindo makini zaidi wa maisha ya utakatifu, na huenda wengi hawakupenda jambo hilo?
  • (2) Je, inawezekana kwamba kama wangekuwa ndani ya Mji wa Yerusalemu, matendo yao yangetazamwa kwa ukaribu zaidi na walitegemewa kufuata mapenzi ya Mungu? Kwa mfano, wasingeweza kununua wala kuuza katika siku ya Sabato (Nehemia 13:15-17).

“Baba wa mbinguni, tusaidie kutambua, sasa kuliko wakati mwingine wowote, kwamba daima uwepo Wako ni mahali salama kwetu.”

Pardon Mwansa: Former General Vice President, General Conference