Nehemiah 10

Kitabu cha Nehemia 10

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Ahadi ya pamoja ya utii inawekwa katika maandishi na kutiwa muhuri na viongozi, makuhani, Walawi na watu wengine. Hii ni tukio la kufanya upya agano na Bwana. Nehemia ndiye wa kwanza kusaini akifuatiwa na viongozi 83.


 

1 Basi hawa ndio waliotia muhuri; Nehemia, ndiye Tirshatha, mwana wa Hakalia, na Sedekia;

2 Seraya, Azaria, Yeremia;

3 Pashuri, Amaria, Malkiya;

4 Hamshi, Shekania, Maluki;

5 Harimu, Meremothi, Obadia;

6 Danieli, Ginethoni, Baruki;

7 Meshulamu, Abiya, Miyamini;

8 Maazia, Bilgai, Shemaya; hao ndio waliokuwa makuhani.

9 Na Walawi; ndio, Yeshua, mwana wa Azania, Binui wa wana wa Henadadi, Kadmieli;

10 na ndugu zao, Shebania, Hodia, Kelita, Pelaya, Hanani;

11 Mika, Rehobu, Hashabia;

12 Zakuri, Sherebia, Shebania;

13 Hodia, Bani, Beninu;

14 Na wakuu wa watu; Paroshi, Pahath-Moabu, Elamu, Zatu, Bani;

15 Buni, Azgadi, Bebai;

16 Adonikamu, Bigwai, Adini;

17 Ateri, Hezakia, Azuri;

18 Hodia, Hashumu, Besai;

19 Harifu, Anathothi, Nobai;

20 Magpiashi, Meshulamu, Heziri;

21 Meshezabeli, Sadoki, Yadua;

22 Pelatia, Hanani, Anaya;

23 Hoshea, Hanania, Hashubu;

24 Haloheshi, Pilha, Shobeki;

25 Rehumu, Hashabna, Maaseya;

26 Ahia, Hanani, Anani;

27 Maluki, Harimu, na Baana.

28 Na watu waliosalia, makuhani, Walawi, mabawabu, waimbaji, Wanethini, na hao wote waliojitenga katika watu wa nchi kwa torati ya Mungu; wake zao, na wana wao, na binti zao, kila mwenye maarifa na akili;

29 wakaambatana na ndugu zao, wakuu wao, nao wakaingia katika laana na kiapo, ya kuwa wataiendea torati ya Mungu, iliyotolewa kwa mkono wa Musa, mtumishi wa Mungu, na kuziangalia, na kuzitenda, amri zote za Bwana, Bwana wetu, na hukumu zake na sheria zake;

  • [Kwa kawaida maagano yalihusisha baraka na laana (angalia Kumbukumbu 28:1-14; 27:11-26 na katika Nehemia 10:38-39). Yalihusisha kujiepusha kuwa na ndoa za kigeni—zisizoruhusiwa (Nehemia 10:30), utunzaji wa kweli wa Sabato (Nehemia 10:31), kufuta madeni (Nehemia 10:31), ulipaji wa fedha kwa ajili ya hekalu (Nehemia 10:32-33), huduma za hekaluni na matoleo na zaka (Nehemia 10:34-39). Watu wanatiwa changamoto ya kusimama mbele ya Mungu kama mtu binafsi na kuweka vipaumbele mahali sahihi, toka “mimi kwanza” na kufuata mtazamo wa Biblia wa “sisi kwa pamoja.”]

30 wala tusiwaoze watu wa nchi binti zetu, wala kuwatwalia wana wetu binti zao;

31 tena watu wa nchi wakitembeza biashara, au chakula cho chote, siku ya sabato, tusinunue kwao siku ya sabato, au siku takatifu; tena kwamba tuuache mwaka wa saba, na madai ya kila deni.

32 Tena tukajifanyia maagizo, kujitoza mwaka kwa mwaka theluthi ya shekeli kwa huduma ya nyumba ya Mungu wetu;

33 kwa mikate ya wonyesho, na kwa sadaka ya unga ya daima, na kwa sadaka ya kuteketezwa ya daima, ya sabato, na ya siku za mwezi mpya, na ya sikukuu, tena kwa vitu vile vitakatifu, na kwa sadaka za dhambi, za kuwafanyia Israeli upatanisho, na kwa ajili ya kazi yote ya nyumba ya Mungu wetu.

34 Kisha tukapiga kura, makuhani, na Walawi, na watu, juu ya matoleo ya kuni, ili kuzileta nyumbani kwa Mungu wetu, kwa kadiri ya mbari za baba zetu, kwa nyakati zilizoamriwa, mwaka kwa mwaka, kukoka moto madhabahuni mwa Bwana, Mungu wetu, kama ilivyoandikwa katika torati;

35 tena kuleta malimbuko ya ardhi yetu, na malimbuko ya matunda yote ya miti ya namna zote, mwaka kwa mwaka, nyumbani kwa Bwana;

36 tena wazaliwa wa kwanza wa wana wetu, na wa wanyama wetu, kama ilivyoandikwa katika torati, na wazaliwa wa kwanza wa ng’ombe zetu na kondoo zetu, ili kuwaleta nyumbani mwa Mungu wetu, kwa makuhani watumikao nyumbani mwa Mungu wetu;

37 tena tuyalete malimbuko ya unga wetu, na sadaka zetu za kuinuliwa, na matunda ya miti ya namna zote, mvinyo, na mafuta, kwa makuhani, hapo vyumbani kwa nyumba ya Mungu wetu; na zaka za ardhi yetu kwa Walawi; kwa kuwa hao Walawi wazitwaa zaka mijini mwote mwa kulima kwetu.

38 Naye kuhani, mwana wa Haruni, atakuwako pamoja na Walawi, watwaapo zaka Walawi; nao Walawi wataipandisha zaka ya hizo zaka nyumbani kwa Mungu wetu, vyumbani, katika nyumba ya hazina.

39 Kwa kuwa wana wa Israeli na wana wa Lawi wataleta sadaka ya kuinuliwa ya nafaka, na mvinyo, na mafuta, vyumbani, kwa kuwa ndimo vilimo vyombo vya patakatifu, na makuhani watumikao, na mabawabu, na waimbaji; wala sisi hatutaiacha nyumba ya Mungu wetu.


 

UFUPISHO WA NEHEMIA 10

Agano la “kutembea katika sheria ya Mungu” lilifanywa.

  1. Ni wapi ambapo Walawi, makuhani, waimbaji, na walinzi walijifunzia jinsi ya kutembea katika sheria ya Mungu?
  2. Walijifunza katika Neno la Mungu kama lilivyokuwa limeandikwa na Musa, mtumishi wa Mungu.

Maeneo matatu yameorodheshwa ambayo kwayo waliamua kutembea katika sheria ya Mungu:

  • (1) Hatutawapatia wenyeji wa nchi binti zetu, wala kuwatwalia wana wetu binti zao;
  • (2) Tena watu wa nchi wakitembeza biashara, au chakula chochote, siku ya Sabato, tusinunue kwao siku ya Sabato, au siku takatifu;
  • (3) Tutaleta zaka na sadaka zetu, na kila mwaka wa saba tutaipumzisha ardhi na pia hatutakusanya madai ya kila deni (Nehemia 10:30-33).

Wakati ambapo watu wana haki ya kuwa na mawazo yao wenyewe, hata hivyo pale ambapo Neno la Mungu liko dhahiri na bayana, kuna njia moja tu ya “kutembea katika sheria ya Mungu;” na njia hiyo ni kutii kile lisemacho Neno, hata kama ni jambo linaloonekana kutofaa kwetu.