Nehemia 6

Kitabu cha Nehemia 6

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii inahusu jaribio la kusababisha hofu na kudhoofisha lengo thabiti la Nehemia la kukamilisha jukumu lake. Maadui wa Yuda wanasikia kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kuta na malango ya Mji wa Yerusalemu na wanapanga njama za vitisho na shutuma ili kuikomesha kazi hiyo. Kulingana na aya ya 1, kuta zilikuwa zimekamilika ila malango yalikuwa bado.


 

 

1 Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakusalia mavunjiko ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango);

2 Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya.

3 Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?

4 Nao wakaniletea maneno kama hayo mara nne; nikawajibu maneno kama yale.

5 Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumwa wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake;

6 nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mwakusudi kuasi; ndiyo sababu waujenga huo ukuta; nawe wataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo.

7 Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu, kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa ataarifiwa mfalme sawasawa na maneno haya. Njoo sasa basi, na tufanye shauri pamoja.

8 Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni.

9 Kwani hao wote walitaka kutuogofisha, wakisema, Italegea mikono yao katika kazi, isifanyike. Lakini sasa nitaitia mikono yangu nguvu.

  • [Maadui wa Nehemia wanabadilisha mbinu. Kwa sababu ukinzani pamoja na vitisho vya moja kwa moja havikufanikiwa, sasa wanatumia uzushi wakishutumu mwenendo na nia ya Nehemia na kwa siri wanadai kuwa ameazimu kujitwalia ukuu. Hata hivyo vitisho hivyo (aya ya 7) havileti matokeo waliyokusudia maadui hao. Nehemia kamwe habadilishi mawazo yake na kuondolewa katika jukumu muhimu; huzitazama shutuma hizo kama madai ya uongo. Badala ya kulisafisha jina lake, anatambua kusudi lao na anamwomba Mungu: “Lakini sasa, Ee Mungu, imarisha mikono yangu” (aya ya 9, KJV).]

10 Nikaingia nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa; naye akasema, Tukutane nyumbani mwa Mungu, ndani ya hekalu, tukaifunge milango ya hekalu; kwa maana watakuja kukuua; naam, wakati wa usiku watakuja kukuua.

11 Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.

12 Nikatambua, na tazama, siye Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.

13 Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie.

14 Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, Tobia na Sanbalati sawasawa na hayo matendo yao, na yule nabii mke Noadia, na hao manabii waliosalia, waliotaka kuniogofya.

  • [Ujumbe wa nabii Shemaya haukutoka kwa Mungu, ni njama walizofanya pamoja na adui wa Yuda—Sanbalati na Tobia. Amenunuliwa ili kutekeleza mipango yao ya upinzani. Nehemia anatambua kutofaa kwa pendekezo la Shemaya: Inawezekanaje, yeye asiye Kuhani aingie katika chumba cha ndani cha hekalu?”]

15 Basi huo ukuta ukamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli, katika muda wa siku hamsini na mbili.

16 Ikawa adui zetu wote waliposikia, ndipo makafiri wote waliotuzunguka wakaogopa, nao wakakata tamaa sana machoni pao wenyewe; maana waliitambua kazi hiyo ilivyotendwa na Mungu wetu.

17 Tena siku zile wakuu wa Yuda walimletea Tobia nyaraka nyingi, nazo nyaraka za Tobia zikawafikilia.

18 Kwa maana walikuwa watu wengi katika Yuda waliomwapia, kwa sababu alikuwa mkwewe Shekania, mwana wa Ara; naye Yehohanani mwanawe amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia.

19 Tena waliyanena mema yake mbele yangu, nayo maneno yangu humwambia yeye. Tobia naye akaniletea mimi nyaraka za kuniogofisha.


 

UFUPISHO WA NEHEMIA 6

“Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata siwezi kushuka; kwa nini kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?” (Nehemia 6:3), ndilo lililokuwa jibu la Nehemia kwa wale waliopanga njama za kuvuruga maendeleo ya kazi yao. Ili kujikita katika kazi ya Mungu wakati mwingine kunaweza kuhitajika jibu ambalo kimsingi ni kukataa tu kushawishiwa toka katika utendaji wa mapenzi ya Mungu.

Adui anaposhindwa katika njia moja ya mashambulizi, hubadilisha na kutumia zingine ambazo ni za hila na hatari zaidi, zote zikiwa na lengo la kuwahafifisha wale wanaomtumikia Mungu kwa uaminifu. Tobia, Geshemu, na Sanbalati walitunga taarifa za uongo, wakawaajiri watu ambao walikusudiwa kudhoofisha shughuli ya Nehemia na watu wake, wakatuma barua za kumtisha Nehemia—walitumia njia zote ili kumvunja nguvu. Nehemia aliogopa, lakini Mungu alimpatia kiongozi Wake huyu hekima ya kutambua mipango hii ya siri na akajibu kwa usahihi.

Kazi ambayo Mungu aliiweka moyoni mwa Nehemia hatimaye ikamalizika kwa muda wa siku 52. Hii ilitimizwa kwa msaada wa Mungu wakati Nehemia na watu wake walipodumu kumtegemea Mungu huku wakiifanya kazi Yake.

“Mungu mpendwa, tusaidie ili tuweze kutambua njama za yule adui; tupatie ujasiri wa kusonga mbele katika kuiendeleza kazi Yako.”