Nehemia 2

Kitabu cha Nehemia 2

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Miezi 4 imepita tangu maombi yale ya sura ya 1. Muda mwafaka wa utendaji wa Mungu mara nyingi huwa haueleweki lakini wakati wote ni timilifu katika kuyatekeleza mapenzi Yake (Danieli 9:24-27). Kazi ya Nehemia inahusisha utendaji wa karibu na mfalme, lakini baada ya kupokea taarifa za fadhaa kuhusu Yerusalemu katika sura ya 1, Nehemia hawezi tena kuendelea na shughuli yake kama kawaida. Ingawaje hili lilikuwa jambo la haraka, muda mwafaka ulikuwa suala la msingi wakati wa kushughulika na ufalme (rejea pia Esta 5 :1-8).


 

1 Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wo wote.

2 Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana.

3 Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto?

4 Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni.

  • [“Una haja gani unayotaka kuniomba?”—si tu kwamba mfalme huyu anautambuzi juu ya hali fulani isiyokawaida inayoendelea kwa Nehemia, lakini pia analenga moja kwa moja kwenye jambo lenyewe. Nehemia anatumia wakati huo vizuri, naye analenga moja kwa moja kwenye jambo lenyewe: nia ya kuujenga upya ukuta kuuzunguka Mji wa Yerusalemu.]

5 Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga.

6 Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda.

7 Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng’ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda;

8 nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu.

  • [Nehemia anaorodhesha miradi 3 mahususi: ujenzi wa malango ya ngome, ukuta wa mji na makazi binafsi.]

9 Ndipo nikafika kwa maliwali walio ng’ambo ya Mto, nikawapa hizo nyaraka za mfalme. Naye mfalme alikuwa amepeleka maakida wa jeshi lake na wapanda farasi pamoja nami.

10 Hata Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, waliposikia habari hizi, ziliwahuzunisha sana, kwa kuwa amekuja mtu kuwatakia heri wana wa Israeli.

  • [Yerusalemu umezungukwa na maadui: Sambalati (wa Samaria) toka upande wa kaskazini, Tobia (wa Amoni) toka mashariki, na Geshemu (Mwarabu, angalia Nehemia 2:19) toka upande wa kusini.]

11 Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu.

12 Kisha nikaondoka usiku, mimi na watu wachache pamoja nami; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe.

13 Nikatoka nje usiku, kwa njia ya lango la bondeni, nikashika njia iendayo kisima cha joka, na lango la jaa; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto.

  • [Lengo la uchunguzi huu wa siri alioufanya Nehemia lilikuwa kupata taarifa za kutosha juu ya ulinzi wa Mji huo wa Yerusalemu bila wapinzani na maadui kufahamu.]

14 Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; lakini hapakuwa na nafasi ya kupita kwa yule mnyama aliyekuwa chini yangu.

15 Kisha nikapanda usiku kando ya kijito, nikautazama ukuta; kisha nikarudi nyuma, nikaingia kwa lango la bondeni, nikarejea hivyo.

16 Wala mashehe hawakujua nilikokwenda, wala nilivyotenda; wala sijawaambia Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala mashehe, wala watu wengine waliokuwa wakiifanya kazi hiyo.

17 Kisha nikawaambia, Mnaona hali hii dhaifu tuliyo nayo, jinsi Yerusalemu ulivyo hali ya ukiwa, na malango yake yalivyoteketezwa kwa moto; haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu, ili tusiwe shutumu tena.

18 Nikawaeleza habari ya mkono wa Mungu wangu ulivyokuwa mwema juu yangu; pia na maneno ya mfalme aliyoniambia. Nao wakasema, Haya! Na tuondoke tukajenge. Basi wakaitia mikono yao nguvu kwa kazi hiyo njema.

  • [Baada ya kujua kwa usahihi hali husika ya Mji, sasa ni wakati wa utendaji. Na hili huanza kwa kuwashawishi viongozi kutambua hali hiyo na kuitikia vilivyo. Anahimiza: “haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu.” Huyu si kiongozi atendaye kivyake kwa kujaribu kuuhamisha mlima mwenyewe, bali ni kiongozi mwenye njozi anayejaribu kueneza na kupitisha njozi yake kwa wengine ili kuwahusisha katika utekelezaji wake. Inavutia kuwa katika kila kipengele cha shughuli yake nzima ya utume, Nehemia anahusisha ushuhuda wake binafsi wa fadhila za Mungu kwake. Watu wanaitikia kwa pamoja, wakisema, “Haya! Na tuondoke tukajenge.”]

19 Lakini waliposikia Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, na Geshemu, Mwarabu, walitucheka, wakatudharau, wakasema, Ni nini neno hili mnalofanya? Je! Mtaasi ninyi juu ya mfalme?

20 Ndipo nikawajibu, nikawaambia, Mungu wa mbinguni, yeye atatufanikisha; kwa hiyo sisi, watumishi wake, tutaondoka na kujenga; lakini ninyi hamna sehemu, wala haki, wala kumbukumbu, katika Yerusalemu.


UFUPISHO WA NEHEMIA 2

Si tu kwamba Nehemia alimtegemea Mungu ili ampatie maneno sahihi ya kumwambia mfalme, lakini pia ili kuulainisha moyo wa mfalme huyu ili aweze kutoa jibu la fadhila kwa ombi lake. Kana kwamba kitendo cha kuomba ruhusa ya kwenda kutembelea Yerusalemu kilikuwa hakitoshi, Nehemia anaomba barua kutoka kwa mfalme ili kumruhusu kutekeleza suala muhimu alilolipandikiza Mungu moyoni mwake—lile la kuzijenga upya kuta za Yerusalemu. Mungu anaugusa moyo wa mfalme huyo na kuliruhusu hata jambo hilo.

Kama ilivyo kila mara, si kila mtu huwa na furaha pale mtu fulani anapoanza kufanya kitu fulani kwa ajili ya Mungu. Shetani huwainua watu wapinge kazi ya Mungu. Katika tukio hili kwenye sura hii, Shetani alimtumia Sambalati na Tobia, ambao walikuwa maafisa wa ufalme wa Amoni, ili kumpinga Nehemia.

Mwitikio wa Nehemia ulikuwa, “Mungu wa mbinguni, Yeye atatufanikisha” (aya ya 20). Kiini cha ustawi na mafanikio yetu yote tunapoazimu kuyafanya mapenzi ya Mungu ni kumtumaini Yeye kikamilifu.

Pia, Nehemia alikuwa mtendakazi makini ambaye hakuanza mradi wake kabla ya kufanya utafiti wa kutosha kuhusiana na matatizo yaliyokuwepo ili aweze kujua ukubwa wa kazi inayopaswa kufanyika. Umakini kamili unahitajika kila wakati tunapoifanya kazi ya Mungu.