Nehemia 1

Kitabu cha Nehemia 1

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Nehemia alikuwa mtumishi katika jumba la kifalme huko Shushani mnamo mwaka 444 KK. Mahali hapo palikuwa ni eneo mojawapo la kiutawala miongoni mwa majimbo ya ufalme wa Uajemi.

1 Habari za Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa katika mwezi wa Kisleu, mwaka wa ishirini, nilipokuwapo Shushani ngomeni,

2 Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akanijia, yeye na watu wengine waliotoka Yuda; nami nikawauliza habari za Wayahudi waliopona, hao watu wa uhamisho waliosalia; na habari za Yerusalemu.

3 Wakaniambia, Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto.

  • [“hali ya dhiki nyingi na mashutumu”—maneno ya namna hii hujirudia mara 4 katika AK. Katika Nehemia 1:3 na 2:17 yanatumika kuelezea hali ya ukiwa ya watu wa Mungu katika Yerusalemu. Katika Zaburi 15:3 na Yeremia 24:9 hutumika kuelezea hali ya shida ya wale waliokuwa wakimpinga Mungu. Kuwa katika hali ya dhidi na mashutumu huonesha mazingira ya kukatisha tamaa kabisa. Kwa hali ya Yerusalemu, sababu ya dhidi hii ilihusisha kuta zilizovunjwa na kuangushwa na milango iliyotekezwa kwa moto.]

4 Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni;

5 nikasema, Nakusihi, Ee Bwana, Mungu wa mbinguni, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake;

6 tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli, watumishi wako; hapo ninapoziungama dhambi za wana wa Israeli, tulizozifanya juu yako; naam, mimi na nyumba ya baba yangu tumefanya dhambi.

7 Tumetenda maovu mengi juu yako, wala hatukuzishika amri, wala sheria, wala hukumu, ulizomwamuru Musa, mtumishi wako.

8 Nakuomba, likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako, ukisema, Mkikosa, nitawatawanya kati ya mataifa;

9 bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo.

10 Basi watu hao ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa uweza wako mwingi, na kwa mkono wako hodari.

11 Ee Bwana, nakusihi, litege sikio lako, uyasikilize maombi ya mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako, wanaofurahi kulicha jina lako; nakuomba sana; unifanikishe mimi, mtumishi wako, leo, ukanijalie rehema mbele ya mtu huyu. (Maana, nalikuwa mnyweshaji wa mfalme).


 

UFUPISHO WA NEHEMIA 1

Mungu alipandikiza hamasa ndani ya moyo wa Nehemia ili kufanya kitu na kushughulikia tatizo fulani na kuleta tofauti. Nehemia aliusikia wito wa Mungu wa kurejea Yerusalemu na kuzijenga upya kuta zake. Ari hiyo ndani yake ilimfanya alie, afunge na kuomba kwa ajili ya jambo hilo ili aweze kupata ufahamu sahihi wa kile ambacho wito wa Mungu ulihusisha (aya ya 4). Kuitikia wito wa Mungu huanza kwa maombi—kutafuta uwepo wa Mungu.

Mara nyingi kuyafanya mapenzi ya Mungu si jambo rahisi, lakini mtu anapoliombea jambo hilo, anaweza kumtumaini Mungu ili kuilainisha mioyo ya wale wanaohusika na humpatia maelekezo kuhusu jambo la kufanya ili kutelekeza mapenzi Yake. Nehemia hakujua jinsi ambavyo mfalme angejibu juu ya shauku yake ya kuitikia wito wa Mungu. Lakini kuna nguvu katika maombi. Nehemia aliomba ili aweze kupata nguvu ya Mungu ya kuulainisha moyo wa mfalme, na Mungu alifanya hivyo.

Bwana Mungu, weka hamasa kwa kila mmoja wetu ili aweze kuyafanya mapenzi Yako na kisha elekeza hatua zetu ili kutekeleza jambo hilo.”