Ezra 10

Kitabu cha Ezra 10

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Ombi na maungamo ya Ezra yanaleta badiliko kubwa sana na la pekee kwa umati wa watu wa Mungu waliokuwa wamemwasi Bwana.


1 Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume, na wanawake, na watoto; maana watu hao walikuwa wakilia sana.

2 Hata Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, Sisi tumemkosa Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko tumaini kwa Israeli katika jambo hili.

3 Haya basi! Na tufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati.

4 Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.

5 Ndipo Ezra akaondoka, akawaapisha wakuu wa makuhani, na Walawi, na Israeli wote, ya kwamba watafanya kama hayo. Basi wakaapa.

6 Kisha Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu, akaingia katika chumba cha Yehohanani, mwana wa Eliashibu; hata, alipofika huko, hakula mkate, wala hakunywa maji; kwa maana alilia kwa sababu ya kosa lile la watu wa uhamisho.

7 Wakapiga mbiu katika Yuda yote na Yerusalemu, ya kwamba wana wote wa uhamisho wakusanyike pamoja huko Yerusalemu;

8 na ya kwamba mtu awaye yote asiyekuja katika muda wa siku tatu, kwa shauri lile la wakuu na wazee, basi aondolewe mali zake zote, akatengwe yeye mwenyewe na mkutano wa uhamisho.

9 Ndipo wanaume wote wa Yuda na Benyamini wakakusanyika katika muda wa siku tatu; ulikuwa mwezi wa kenda, siku ya ishirini ya mwezi; na watu wote wakaketi katika uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakitetemeka kwa sababu ya neno hilo, na kwa sababu ya mvua kubwa.

10 Kisha Ezra, kuhani, akasimama, akawaambia, Mmekosa, mmeoa wanawake wageni, kuiongeza hatia ya Israeli.

11 Sasa basi, ungameni mbele za Bwana, Mungu wa baba zenu, mkatende alipendalo; mkajitenge na watu wa nchi, tena na wanawake wageni.

12 Ndipo mkutano wote wakajibu, wakasema, kwa sauti kuu, Kama ulivyosema katika habari yetu, ndivyo vitupasavyo kutenda.

13 Lakini watu hawa ni wengi, tena ni wakati wa mvua nyingi, nasi hatuwezi kusimama nje, tena kazi hii si kazi ya siku moja, wala ya siku mbili; maana tumekosa sana katika jambo hili.

14 Basi maakida wetu na wawekwe kwa ajili ya mkutano wote, na watu wote walio katika miji yetu, waliooa wanawake wageni, na waje nyakati zilizoamriwa, tena pamoja nao na waje wazee wa kila mji, na makadhi wa miji hiyo, hata ghadhabu kali ya Mungu wetu itakapotuondokea mbali, jambo hili likamalizike.

15 Yonathani, mwana wa Asaheli, na Yazeya, mwana wa Tikwa, hawa peke yao ndio waliosimama kulipinga neno hilo; na Meshulamu, na Shabethai Mlawi, wakawasaidia.

16 Basi wana wa uhamisho wakafanya hivyo. Na Ezra, kuhani, akatengwa, pamoja na baadhi ya wakuu wa mbari za mababa, kwa hesabu ya mbari ya baba zao; na hao wote kwa majina yao. Wakaketi siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, ili kulichunguza jambo hilo.

17 Wakamaliza mambo ya wanaume wote, waliokuwa wameoa wanawake wageni, siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza.

18 Basi, miongoni mwa makuhani walionekana wengine waliokuwa wameoa wanawake wageni; wa wana wa Yoshua, mwana wa Yosadaki, na nduguze; Maaseya, na Eliezeri, na Yaribu, na Gedalia.

19 Nao wakatoa ahadi ya kwamba wataachana na wake zao; na kwa kuwa walikuwa na hatia, wakatoa kondoo mume kwa hatia yao.

20 Na wa wana wa Imeri; Hanani, na Zebadia.

21 Na wa wana wa Harimu; Maaseya, na Eliya, na Shemaya, na Yehieli, na Uzia.

22 Na wa wana wa Pashuri; Elioenai, na Maaseya, na Ishmaeli, na Nethaneli, na Yozabadi, na Elasa.

23 Na wa Walawi; Yozabadi, na Shimei, na Kelaya (ndiye Kelita), na Pethahia, na Yuda, na Eliezeri.

24 Na wa waimbaji; Eliashibu. Na wa mabawabu; Shalumu, na Telemu, na Uri.

25 Na wa Israeli; wa wana wa Paroshi; Ramia, na Izia, na Malkiya, na Miyamini, na Eleazari, na Malkiya, na Benaya.

26 Na wa wana wa Elamu; Matania, na Zekaria, na Yehieli, na Abdi, na Yeremothi, na Eliya.

27 Na wa wana wa Zatu; Elioenai, na Eliashibu, na Matania, na Yeremothi, na Zabadi, na Aziza.

28 Na wa wana wa Bebai; Yehohanani, na Hanania, na Zakai, na Athlai.

29 Na wa wana wa Bani; Meshulamu, na Maluki, na Adaya, na Yashubu, na Sheali, na Yeremothi.

30 Na wa wana wa Pahath-Moabu; Adna, na Kelali, na Benaya, na Maaseya, na Matania, na Besaleli, na Binui, na Manase.

31 Na wa wana wa Harimu; Eliezeri, na Ishiya, na Malkiya, na Shemaya, na Shimeoni,

32 na Benyamini, na Maluki, na Shemaria.

33 Na wa wana wa Hashumu; Matenai, na Matata, na Zabadi, na Elifeleti, na Yeremai, na Manase, na Shimei.

34 Na wa wana wa Bani; Maadai, na Amramu, na Ueli,

35 na Benaya, na Bedeya, na Keluhi,

36 na Wania, na Meremothi, na Eliashibu,

37 na Matania, na Matenai, na Yaasu.

38 Na wa wana wa Binui; Shimei,

39 na Shelemia, na Nathani, na Adaya,

40 na Maknadebai, na Shashai, na Sharai,

41 na Azareli, na Shelemia, na Shemaria,

42 na Shalumu, na Amaria, na Yusufu.

43 Na wa wana wa Nebo; Yeieli, na Matithia, na Zabadi, na Zebina, na Ido, na Yoeli, na Benaya.

  • [Zingatia mpangilio, katika orodha, wa wale ambao walikuwa wamewaoa wake wa kigeni. Huanza na makuhani (watu 17), kisha Walawi (watu 10), na hatimaye wana wa Israeli wengine (watu 86).]

44 Hao wote walikuwa wameoa wanawake wageni; na wake zao wengine walikuwa wamezaa watoto.

  • [Kwa bahati mbaya, wakati ambapo tatizo hili la ndoa za kigeni lilishughulikiwa hapa, lilijitokeza tena baadaye (Nehemia 9:2; 10:28-30; 13:23-27).]

 

UFUPISHO WA EZRA 10

Neema ya Mungu inatosha kwa kila hali endapo tu watu Wake watakuwa tayari kurejea Kwake. Na ili jambo hili liweze kutokea, watu wa Mungu wanahitaji kufanya jambo fulani zaidi ya kuomba tu—wanapaswa kupokea neema Yake na kujitahidi kuyafanya mapenzi Yake.

Sasa, wakati Ezra akiomba, na wakati akiungama, akilia, na kusujudu mbele ya Nyumba ya Mungu, Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, ambaye pamoja na wengine walikuwa wamemwasi Mungu kwa kuwaoa wanawake toka nchi za kigeni, akatubu, na akazungumza akimwamwambia Ezra, “Sisi tumemkosa Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko tumaini kwa Israeli katika jambo hili” (aya ya 2). Aliitisha matengenezo na kufanya upya agano kwa kuifuata sheria ya Mungu (aya ya 3), na akasema, “sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende” (aya ya 4).

Matengenezo yoyote daima huwa ni kurejea katika kuyafanya mapenzi ya Mungu. Kazi ya matengenezo si tendo la siku moja. Jambo la msingi ni pale watu wa Mungu wanapoamua kuachana na njia zao mbaya kila siku—kuacha kila siku kile kisichopatana na mapenzi ya Mungu.