Ezra 9

Kitabu cha Ezra 9

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI:

  • Sura hii inahusisha ombi la Ezra la toba kwa ajili ya Waisraeli.
  • Maombi ni sehemu ya msingi katika kitabu cha Ezra (8:21-23; 10:1) na huhusisha vipengele vya shukrani, maungamo, na kutafuta msaada.
  • Ombi lake la sura hii ya 9 inahusiana kabisa na kipengele cha pili cha utume wake ambacho ni kutangaza na kufundisha sheria ya Bwana katika harakati ya matengenezo ya kiroho.
  • Katika Maandiko, mabadiliko yote muhimu na ya dhati pamoja na mianzo mipya ni matokeo ya maombi (rejea katika 2 Wafalme 19:14-34; 2 Nyakati 6:12-42; Matendo 2:1-4).

 

1 Na mambo hayo yalipokwisha kutendeka, wakuu wakanikaribia, wakisema, Watu wa Israeli, na makuhani, na Walawi, hawakujitenga na watu wa nchi hizi, wamefanya sawasawa na machukizo yao, yaani, ya Wakanaani, na Wahiti, na Waperizi, na Wayebusi, na Waamoni, na Wamoabi, na Wamisri, na Waamori.

2 Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili.

3 Nami niliposikia hayo, nikararua nguo yangu na joho yangu, nikang’oa nywele za kichwa changu, na ndevu zangu, nikaketi kwa mshangao.

4 Ndipo wakanikusanyikia watu wote walioyatetemekea maneno ya Mungu wa Israeli, kwa sababu ya lile kosa la watu wa uhamisho; nami nikaketi kwa mshangao hata wakati wa sadaka ya jioni.

5 Na wakati wa sadaka ya jioni nikainuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za Bwana, Mungu wangu;

6 nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni.

7 Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo.

8 Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na Bwana, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu.

9 Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha, kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu.

10 Na sasa, Ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo? Maana tumeziacha amri zako,

11 ulizoziamuru kwa midomo ya watumishi wako, manabii, ukisema, Nchi ile, mnayoiendea ili kuimiliki, ni nchi ya uchafu, kwa sababu ya uchafu wa watu wa nchi zile, kwa ajili ya machukizo yao, yaliyoijaza tangu upande huu mpaka upande huu, kwa uchafu wao.

12 Basi, msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake za wana wenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa milele.

13 Na baada ya hayo yote yaliyotupata kwa sababu ya matendo yetu mabaya, na kwa sababu ya hatia yetu iliyo kuu, ikiwa wewe Mungu wetu hukutuadhibu kama tulivyostahili kwa maovu yetu, tena umetupa mabaki;

14 je! Tuzivunje tena amri zako, tukajiunge na watu wanaotenda machukizo hayo, kwa kuoana nao? Je! Usingekasirika nasi hata kutuangamiza kabisa, pasisalie mabaki yo yote, wala mtu wa kuokoka?

15 Ee Bwana, Mungu wa Israeli, wewe ndiwe mwenye haki, maana sisi tumesalia, mabaki yaliyookoka, kama hivi leo; tazama, sisi tupo hapa wenye hatia mbele zako; maana hapana mtu awezaye kusimama mbele zako kwa sababu ya jambo hili.

  • [Ombi la Ezra linadokeza juu ya historia iliyopita ya Israeli (aya ya 7) na kisha hulenga kwenye fursa ya Mungu, ambako Mungu anawatumia wafalme ili kuwaruhusu masalia ya watu Wake warejee Yerusalemu na kulijenga upya Hekalu na ukuta wa mji huo (aya ya 8-9). Ombi lake humdhihirisha si tu kama kiongozi, lakini pia kama mpatanishi. Anajihusianisha na hatia ya watu Wake.]

UFUPISHO WA EZRA 9

Uaminifu kwa mapenzi ya Mungu ni zaidi ya kutoa sadaka na kujenga mahekalu. Mungu alikuwa amewaagiza watu Wake wasiwaruhusu watoto wao waoane na wale wa mataifa mengine, lakini, hata hivyo, “Watu wa Israeli, na makuhani, na Walawi, hawakujitenga na watu wa nchi hizi, wamefanya sawasawa na machukizo yao, yaani, ya Wakanaani, na Wahiti, na Waperizi, na Wayebusi, na Waamoni, na Wamoabi, na Wamisri, na Waamori” (aya ya 1). Jambo la kusikitisha, hasa, ni kwamba viongozi na watawala ndio waliokuwa mstari wa mbele kabisa katika uasi kwa kuwachukua baadhi ya binti toka katika mataifa haya kuwa wake zao wenyewe na kwa ajili ya wana wao (aya ya 2).

Matengenezo humaanisha kubadilisha au kurekebisha njia zetu ili zipatane na mapenzi ya Mungu. Na ili matengenezo yaweze kuanza, viongozi wa kiroho pamoja na watu wote lazima wajinyenyekeshe kwa Mungu katika maombi na kufunga.

Ezra aliposikia kile kilichokuwa kikifanyika, aliyararua mavazi yake, akafanya saumu na kuendelea kumwomba Mungu, akitafuta msamaha na badiliko la moyo la watu wa Mungu (aya ya 5-6). Isipokuwa tu kama tunaona jinsi dhambi ilivyo mbaya sana kiasi cha kuchukiza na kutafuta msamaha na mabadiliko kamili, kamwe hatufanikiwa kufanya matengenezo.