Ezra 5

Kitabu cha Ezra 5

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii inadokeza jinsi viongozi walivyokabiliana na changamoto kutoka kwa mfalme wa Uajemi, iliyowataka wakome kuendelea na kazi ya ujenzi. Hata hivyo kazi hiyo makini inasonga mbele pamoja na upinzani huo usio kuwa na mantiki.


1 Basi manabii, Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido, wakawafanyia unabii Wayahudi waliokuwako Yerusalemu na Yuda; waliwafanyia unabii kwa jina la Mungu wa Israeli.

2 Ndipo akaondoka Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, wakaanza kuijenga nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na pamoja nao walikuwa manabii wa Mungu, wakiwasaidia.

3 Wakati ule ule Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzi wao, wakawajia, wakawaambia, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu?

4 Ndipo wakawauliza hivi, Majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani na nani?

5 Lakini jicho la Mungu lilikuwa likiwaelekea wazee wa Wayahudi, hao wasiwazuie, hata habari ile imfikilie Dario, ndipo jawabu litakapopatikana kwa waraka.

6 Hii ndiyo nakala ya waraka waliyompelekea mfalme Dario; na Tatenai, liwali wa ng’ambo ya Mto, na Shethar-Bozenai, na wenzake wa Kiajemi, waliokuwako huko ng’ambo ya Mto,

7 walimpelekea waraka nao; na maneno haya yakaandikwa ndani yake; Kwa Dario, mfalme; Salamu sana.

8 Na ajue mfalme ya kuwa sisi tuliingia nchi ya Yuda, tukafika kunako nyumba ya Mungu mkuu, iliyojengwa kwa mawe makubwa, na miti imetiwa katika kuta zake, na kazi hii inaendelea kwa bidii, na kusitawi katika mikono yao.

9 Ndipo tukawauliza wale wazee, tukawaambia hivi, Ni nani aliyewapa amri kuijenga nyumba hii, na kuumaliza ukuta huu?

10 Tukawauliza pia majina yao, ili kukuarifu wewe, tupate kuandika majina ya watu waliokuwa wakubwa wao.

11 Wakatujibu hivi, wakasema, Sisi tu watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunaijenga nyumba iliyojengwa zamani sana, yapata miaka mingi, ambayo mfalme mkuu wa Israeli aliijenga na kuimaliza.

12 Lakini hapo baba zetu walipomkasirisha Mungu wa mbingu na nchi, hata akaghadhibika, akawatia katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, Mkaldayo, naye ndiye aliyeiharibu nyumba hii, akawachukua watu mateka mpaka Babeli.

13 Lakini katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Babeli, Koreshi, mfalme, alitoa amri ijengwe tena nyumba ya Mungu.

14 Na vyombo vya dhahabu na fedha, vya nyumba ya Mungu, alivyovitoa Nebukadreza katika hekalu lililokuwako Yerusalemu, na kuviingiza katika hekalu la Babeli, vyombo hivyo mfalme Koreshi alivitoa katika hekalu la Babeli, akakabidhiwa mtu, jina lake Sheshbaza, ambaye alikuwa amemfanya liwali;

15 naye akamwambia, Chukua vyombo hivi, uende, ukavitie katika hekalu lililoko Yerusalemu, na nyumba ya Mungu na ijengwe mahali pake.

16 Ndipo ye yule Sheshbaza alipokuja, akaupiga msingi wa nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na tangu wakati ule hata leo imekuwa ikijengwa, wala bado haijamalizika.

17 Basi, sasa, mfalme akiona vema, watu na watafute katika nyumba ya hazina ya mfalme, iliyoko huko Babeli, kama ni kweli ya kuwa mfalme Koreshi alitoa amri kuijenga nyumba hiyo ya Mungu katika Yerusalemu, na mfalme akatuletee habari ya mapenzi yake katika jambo hili.


 

UFUPISHO WA EZRA 5

Katika sura ya 4, Mfalme wa Uajemi aliwaamuru watu wa Mungu kuacha kulijenga upya Hekalu la Mungu. Katika sura hii, manabii wa Mungu ambao ni Hagai na Zekaria waliwahimiza watu waendelee na kazi ya mradi huo wa ujenzi, wakiwataka wamtumaini Mungu. Zerubabeli na Yeshua walihimizwa ili kuwahamasisha watu waendelee. “Lakini jicho la Mungu lilikuwa likiwaelekea wazee wa Wayahudi, [kiasi kwamba] hao wasiwazuie, hata habari ile imfikilie Dario” ambaye sasa alikuwa ameingia katika utawala (aya ya 5).

Daima macho ya Bwana huwa juu ya wale wanaofanya mapenzi Yake, lakini huwahitaji wanaume na wanawake wenye elimu na wenye uwezo wa kuwasilisha suala lao kwa hoja thabiti kwa wale walioko madarakani. Wakati Tatenai, ambaye alikuwa mtawala wa eneo hilo kwa niaba ya serikali ya Uajemi, alipomwandikia Zerubabeli barua akimtaka aikomeshe kazi hiyo, watu wa Mungu waliandika jibu ambalo kwalo waliwasilisha taarifa ya ziada na kutaka ufanyike uchunguzi kuhusiana na historia ya suala hilo. Mungu anatutaka kuwa vichwa na wala si mikia, hata katika maarifa.

“Mungu, tafadhali kuza imani yetu kila siku ili, pamoja na upinzani, tuweze kuendelea kukutumaini Wewe kwa kusonga mbele.”