Ezra 3

 

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii inazungumzia urejeshwaji wa ibada katika Mji wa Yerusalemu na mwanzo wa ujenzi wa Hekalu.

1 Hata ulipowadia mwezi wa saba, na wana wa Israeli walipokuwa katika miji yao, watu wakakusanyika pamoja huko Yerusalemu kama mtu mmoja.

  • [“mwezi wa saba”—ulifahamika kama mwezi “Tishri” (inaendana sawa na mwezi wa 9 na 10 kwenye kalenda yetu ya kisasa. Huu ulikuwa mwezi mtakatifu sana kuliko yote katika kalenda ya Waisraeli katika masuala ya kidini (Walawi 23:23-43; Hesabu 29) ikiwa ni pamoja na Sikukuu ya Tarumbeta (Baragumu) (Walawi 23:23-25) na Siku ya Upatanisho (Walawi 16).]

2 Ndipo akasimama Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zake makuhani, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na ndugu zake, nao wakaijenga madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili kutoa sadaka za kuteketezwa juu yake, kama ilivyoandikwa katika torati ya Musa, mtu wa Mungu.

  • [Kazi ya urejeshwaji wa masuala ya kiroho inaanza kwa kufuatana na maagizo yaliyotolewa (Walawi 20:24-26).]

3 Wakaiweka madhabahu juu ya msingi wake; maana hofu imewashika kwa sababu ya watu wa nchi; wakamtolea Bwana sadaka za kuteketezwa juu yake, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni.

  • [Wakati wa Tukio la Kutoka, Mungu alituma “hofu” mbele ya Waisraeli (Kutoka 23:27; Yoshua 2:9) ili kuwahafifisha maadui wao. Hata hivyo, tukio hili la pili la Kutoka hudhihirishwa na hofu ya watu wa Mungu.]

4 Wakaishika Sikukuu ya Vibanda, kama ilivyoandikwa, wakatoa sadaka za kuteketezwa za kila siku kwa hesabu yake, kama ilivyoagizwa, kama ilivyopasa kila siku;

5 na baadaye sadaka ya kuteketezwa ya daima, na za mwandamo wa mwezi, na za sikukuu za Bwana, zilizoamriwa na kuwekwa wakfu, na za kila mtu aliyemtolea Bwana sadaka kwa hiari yake.

6 Tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba walianza kumtolea Bwana sadaka za kuteketezwa, lakini msingi wa hekalu la Bwana ulikuwa haujawekwa bado.

7 Tena waliwapa waashi na maseremala fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na mafuta, ili walete mierezi kutoka Lebanoni mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi.

8 Hata mwaka wa pili wa kufika kwao nyumbani kwa Mungu, huko Yerusalemu, mwezi wa pili, Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine, makuhani na Walawi, na watu wote, waliotoka katika uhamisho na kufika Yerusalemu, wakaanza; nao wakawaweka Walawi, hao wenye miaka ishirini na waliozidi, ili kuisimamia kazi ya nyumba ya Bwana.

9 Ndipo wakasimama Yeshua, na wanawe na ndugu zake, Kadmieli, na wanawe, wana wa Hodavia, pamoja, ili kuwasimamia hao wafanyao kazi katika nyumba ya Mungu; wana wa Henadadi, pamoja na wana wao, na ndugu zao, Walawi.

10 Hata wajenzi walipouweka msingi wa hekalu la Bwana, wakawaweka makuhani, wamevaa mavazi yao, wenye baragumu, na Walawi, wana wa Asafu, wenye matoazi, ili wamhimidi Bwana, kama alivyoagiza Daudi, mfalme wa Israeli.

11 Wakaimbiana, wakimhimidi Bwana, na kumshukuru, wakasema, Kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake kwa Israeli ni za milele. Kisha watu wote wakapaza sauti zao, na kupiga kelele, walipomhimidi Bwana, kwa sababu msingi wa nyumba ya Bwana umekwisha kuwekwa.

  • [“kupiga kelele”—maneno kama haya yametumika katika Yoshua 6:5, 20 wakati wa kuiangusha Yeriko. Pia, yametumika kuelezea mwitikio wa jeshi wakati wa mfalme Sauli pale Sanduku la Agano la Mungu lilipoletwa kambini (1 Samweli 4:5). Watu hawa waliorejea wanatambua kuwa maisha na uwezo wao wa kujenga upya Hekalu hutegemea uwepo na utendaji wa Mungu.]

12 Bali makuhani wengi, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa, waliokuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakati msingi wa nyumba hii ulipowekwa mbele ya macho yao, walilia kwa sauti kuu; na watu wengi walipiga kelele za furaha;

13 hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikilikana mbali sana.

UFUPISHO WA EZRA 3

Jambo la kwanza walilofanya wale waliorejea toka utumwani, kabla ya kuanza kuijenga upya Nyumba ya Bwana, lilikuwa kujenga madhabahu ya sadaka za kuteketeza. Mara tu baada ya kujenga madhabahu, walianza kuteketeza sadaka za “asubuhi na jioni” (aya ya 3). Jambo la kwanza ambalo ni la msingi kabisa kwa watoto wa Mungu mahali popote wanapokwenda au wanapoweza kupatikana ni kuanzisha maisha ya mara kwa mara ya maombi. Maombi ni njia ambayo kwayo watoto wa Mungu hudumu kukaa pamoja na Mungu.

Msingi ulipowekwa na watu wakakusanyika ili kumshukuru Mungu, kulikuwa na mitazamo tofauti. Wale waliokuwa wameliona Hekalu la Sulemani walilia, wakati ambapo wale ambao walikuwa hawakuliona walishangilia kwa furaha kwa kuwekwa kwa msingi huu. Vizazi tofauti vinaweza kuona mambo kwa namna tofauti kwa sababu ya uzoefu wao na historia ya maisha yao ya zamani. Hata leo, vizazi tofauti huwa na mtazamo tofauti kwa mambo yaleyale. Mungu hukutana nasi mahali tulipo.

“Baba wa Mbinguni, tusaidie ili tukutane Nawe katika madhabahu ya maombi kila asubuhi na kila jioni na wakati wote.”