2 Nyakati 8

Kitabu cha 2 Nyakati Sura ya 8

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Katika sura hii kuna taarifa ya shughuli zingine alizotenda Sulemani pamoja na mafanikio yake. Sura hii hulandana na 1 Wafalme 9:10-28.


 

1 Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani aliijenga nyumba ya Bwana, na nyumba yake mwenyewe;

2 ndipo Sulemani akaijenga miji ile Hiramu aliyompa Sulemani, akawakalisha humo wana wa Israeli.

  • [“Hiramu”—alikuwa mfalme wa Foenike aliyeishi katika mji wa Tiro. Alifanya mkataba wa pamoja na mfalme Sulemani, na anamwita “ndugu yangu” (1 Wafalme 9:13).]

3 Naye Sulemani akaenda Hamath-zoba, akaushinda.

4 Akaujenga Tadmori wa nyikani, na miji yote ya hazina, aliyoijenga katika Hamathi.

5 Tena akaujenga Beth-horoni wa juu, na Beth-horoni wa chini, miji yenye boma, yenye kuta, na malango, na makomeo;

6 na Baalathi, na miji yote ya hazina Sulemani aliyokuwa nayo, na miji yote ya magari yake, na miji ya wapanda farasi wake, na ya anasa yote aliyopenda Sulemani kujenga humo Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake.

  • [“Lebanoni”—nchi ya milima inayopatikana kaskazini mwa Israeli kandokando ya ukanda wa Bahari ya Mediteraniani.]

7 Basi kwa habari ya watu wote waliosalia wa Wahiti, na wa Waamori, na wa Waperizi, na wa Wahivi, na wa Wayebusi, wasiokuwa wa Israeli;

  • [“Waamori”—jina hili humaanisha “Wamagharibi” na lilitumiwa na watu wa mashariki kuwaita jamii ya watu waliokuwa wakiishi katika eneo la Shamu-Palestina kabla Israeli haijateka Kanaani.]

8 wa watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuwakomesha, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo.

9 Wala katika wana wa Israeli Sulemani hakuwafanya watumwa kazini mwake; lakini hao walikuwa watu wa vita, na wakuu wa majemadari wake, na maakida wa magari yake na wa wapanda farasi wake.

10 Na hao walikuwa maakida wakuu wa Sulemani, watu mia mbili na hamsini, waliotawala juu ya watu.

11 Sulemani akamleta binti Farao kutoka mji wa Daudi mpaka nyumba aliyomjengea; kwa kuwa alisema, Mke wangu hatakaa nyumbani mwa Daudi mfalme wa Israeli, kwa kuwa ni patakatifu, mahali palipofika sanduku la Bwana.

12 Ndipo Sulemani akamtolea Bwana sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana, aliyoijenga mbele ya ukumbi,

13 kadiri ilivyohitajiwa huduma ya kila siku, akitoa sawasawa na amri ya Musa, siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoamriwa, mara tatu kila mwaka, yaani, sikukuu ya mikate isiyochachwa, na sikukuu ya majuma, na sikukuu ya vibanda.

  • [“sikukuu ya mikate isiyochachwa”—iliadhimishwa katika mwezi wa kwanza wa Kalenda ya Kiebrania na ilihusiana kwa ukaribu na Pasaka (Walawi 23:4-8). “sikukuu ya vibanda”—iliadhimishwa katika mwezi wa saba wa Kalenda ya Kiebrania baada ya Siku ya Upatanisho.]

14 Akaziamuru, sawasawa na agizo la Daudi babaye, zamu za makuhani za kutumika, nao Walawi kwa kadiri ya malinzi yao, ili kusifu, na kuhudumu mbele ya makuhani, kama ilivyohitajiwa kila siku; tena mabawabu kwa zamu zao za kila mlango; maana ndivyo alivyoamuru Daudi mtu wa Mungu.

  • [“mtu wa Mungu”—jina la kawaida la kuwaita manabii wa Mungu. Kitendo cha Daudi kuanzisha upya ibada ya pekee katika Israeli hufanana na kazi aliyoifanya Musa (Kumbukumbu 33:1; Zaburi 90).]

15 Wala hawakuyaacha maagizo ya mfalme aliyowaamuru makuhani na Walawi kwa neno lo lote, wala kwa habari ya hazina.

16 Basi ikatengenezwa kazi yote ya Sulemani hata siku ya kutiwa msingi wa nyumba ya Bwana, na hata ilipokwisha. Hivyo ikamalizika nyumba ya Bwana.

17 Ndipo Sulemani akaenda Esion-geberi, na Elothi, pwani ya nchi ya Edomu.

  • [“Esion-geberi”—Mji muhimu wa bandari katika ghuba ya Akaba inayoelekea kwenye Bahari ya Chumvi. “Edomu”—ni nchi ya wana au uzao wa Esau na ilipatikana katika eneo la kusini mwa Bahari ya Chumvi.]

18 Naye Hiramu akamletea merikebu kwa mikono ya watumishi wake, na watumishi waliokuwa wana-maji; nao wakafika Ofiri pamoja na watumishi wa Sulemani, wakachukua kutoka huko talanta mia nne na hamsini za dhahabu, wakamletea mfalme Sulemani.

  • [“Ofiri”—mji wa bandari ambao huenda ulipatikana kaskazini mwa Afrika au Arabia. “talanta mia nne na hamsini za dhahabu” = tani 16.]

UFUPISHO WA 2 NYAKATI 8

Je, mfalme Sulemani alimwoa mke kutoka Misri kwa sababu alimpenda? Je, alikuwa mzuri na mwenye maarifa bora au alimkusudia kwa ajili ya mapatano ya kisiasa? Ingawa kitabu hiki cha pili cha Nyakati hakielezei kisa chake cha kuwa na “wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu” (1 Wafalme 11:3), hutupatia mdokezo bayana kuhusu mwanzo wa anguko lake la kiroho. “Sulemani akamleta binti Farao kutoka mji wa Daudi mpaka nyumba aliyomjengea; kwa kuwa alisema, Mke wangu hatakaa nyumbani mwa Daudi mfalme wa Israeli, kwa kuwa ni patakatifu, mahali palipofika Sanduku la Bwana” (2 Nyakati 8:11).

Hapa kuna maelezo dhahiri ya utambuzi wa Sulemani juu ya kosa lake. Hata hawezi kumweka mkewe akae katika mji mkuu kwa kuwa anajua hapaswi kuwa karibu na Hekalu alilofanya kila jitihadi ili kulijenga. Katika hatua fulani alifanya uamuzi mmoja wa kuliasi agizo dhahiri la Mungu lililokataza asifanye mapatano yoyote wala kuoana na mataifa mengine. Uamuzi huo mmoja ungeliathiri mwenendo wa maisha yake na kuleta ibada ya sanamu na mateso katika Israeli kwa kipindi cha vizazi vingi.

Je, kuna dhambi fulani ambayo Mungu anazungumza nawe kuhusiana nayo? “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” 1 Yohana 1:9. “Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi” (Yohana 5:14).