2 Nyakati 17

Kitabu cha 2 Nyakati Sura ya 17

 

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Kisa cha Yehoshafati, Mfalme mwema wa Yuda, kinaelezewa katika sura 4 (17 hadi 20) katika kitabu hiki. Kisa hiki hupatikana pia katika 1 Wafalme 22.


 

1 Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake, akajitia nguvu juu ya Israeli.

  • [“Yehoshafati”—jina la huyu mfalme humaanisha “Bwana anahukumu.”]

 

2 Akaweka jeshi katika miji yote yenye maboma ya Yuda, akatia na askari walinzi katika nchi ya Yuda, na katika miji ya Efraimu, aliyoitwaa Asa babaye.

3 Naye Bwana alikuwa pamoja na Yehoshafati, kwa kuwa alikwenda katika njia za kwanza za Daudi babaye, asiyatafute mabaali;

  • [“asiyatafute mabaali”—tofauti na ilivyokuwa kwa mfalme Ahabu, Yehoshafati aliishi kwa kufuata maagizo ya Bwana.]

 

4 lakini alimtafuta Mungu wa baba yake, akaenda katika amri zake, wala si katika matendo ya Israeli.

5 Kwa hiyo Bwana akauthibitisha ufalme mkononi mwake; Yehoshafati akaletewa zawadi na Yuda wote; basi akawa na mali na heshima tele.

6 Ukainuliwa moyo wake katika njia za Bwana; na zaidi ya hayo akapaondoa mahali pa juu, na maashera, katika Yuda.

7 Tena, katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake, akawatuma wakuu wake, yaani, Ben-haili, na Obadia, na Zekaria, na Nethaneli, na Mikaya, ili kufundisha mijini mwa Yuda;

8 na pamoja nao Walawi, yaani, Shemaya, na Nethania, na Zebadia, na Asaheli, na Shemiramothi, na Yehonathani, na Adonia, na Tobia, na Tob-adonia, Walawi; na pamoja nao Elishama na Yehoramu, makuhani.

  • [“Walawi”—walihudumu Hekaluni, na katika kisa hiki wanaonekana dhahiri kuwa miongoni mwa wale wanaowaelimisha watu wafuate mapenzi ya Mungu. “Watamfundisha Yakobo hukumu Zako, Na Israeli torati Yako, Wataweka uvumba mbele zako, Na sadaka nzima za kuteketezwa madhabahuni mwako.” Kumbukumbu 33:10. “Makuhani” walikuwa na wajibu wa kufundisha Neno la Mungu (Malaki 2:7).]

 

9 Wakafundisha katika Yuda, wenye kitabu cha torati ya Bwana; wakazunguka katika miji yote ya Yuda, wakafundisha kati ya watu.

  • [“kitabu cha torati ya Bwana”—2 Nyakati 6:16; 34:14-15; Nehemia 9:3.]

 

10 Hofu ya Bwana ikaziangukia falme za nchi zote zilizozunguka Yuda, wasipigane vita na Yehoshafati.

  • [“Hofu ya Bwana”—kicho au heshima kuu kwa Mwenyezi Mungu.]

 

11 Na baadhi ya Wafilisti walimletea Yehoshafati zawadi, na fedha ya kodi; Waarabu nao wakamletea makundi, kondoo waume saba elfu na mia saba, na mabeberu saba elfu na mia saba.

12 Ukuu wake Yehoshafati ukazidi sana; akajenga katika Yuda ngome na miji ya hazina.

13 Naye alikuwa na kazi nyingi katika miji ya Yuda; na watu wa vita, watu mashujaa humo Yerusalemu.

14 Na hivi ndivyo walivyohesabiwa kwa mbari za baba zao; wa Yuda, maakida wa maelfu; Adna jemadari, na pamoja naye watu mashujaa mia tatu elfu;

15 na wa pili wake Yehohanani akida, na pamoja naye mia mbili na themanini elfu;

16 na baada yake Amasia mwana wa Zikri, aliyejitoa kwa Bwana kwa moyo, na pamoja naye mia mbili elfu, watu mashujaa;

17 na wa Benyamini; Eliada mtu shujaa, na pamoja naye mia mbili elfu wenye nyuta na ngao;

18 na wa pili wake Yehozabadi, na pamoja naye mia na themanini elfu waliojiweka tayari kwa vita.

19 Hao ndio waliomngojea mfalme, zaidi ya hao mfalme aliowaweka katika miji yenye maboma katika Yuda yote.


 

UFUPISHO WA 2 NYAKATI 17

Mfalme Yehoshafati “alikwenda katika njia za kwanza za Daudi babaye, asiyatafute mabaali; lakini alimtafuta Mungu wa baba yake, akaenda katika amri Zake,…. Ukainuliwa moyo wake katika njia za Bwana” (aya ya 3 na 6). Ni maelezo mazuri kiasi gani ya jinsi Mkristo anavyopaswa kuwa! “Kwenda” katika njia au amri za Mungu ni suala la kivitendo, ambalo ni zaidi ya kukiri tu imani. “Ukainuliwa moyo wake”—alipenda sana toka moyoni mwake kumtumikia Mwenyezi Mungu—hili ni suala hata la kina zaidi. Huonesha kazi ya ndani kabisa ya utendaji wa Roho Mtakatifu, akiandika sheria Yake moyoni hadi inapofikia furaha kuwa pamoja na Mungu na kufanya lolote analoagiza.

“Kwa hiyo Bwana akauthibitisha ufalme mkononi mwake; Yehoshafati akaletewa zawadi na Yuda wote” (aya ya 5). Mungu hupenda kuwabariki watoto Wake. Utii kwa Mungu mara zote huleta mafanikio pamoja na fadhila kutoka kwa watu.

Yehoshafati aliondoa sanamu zingine zaidi na katika mwaka wa tatu wa utawala wake aliwatuma viongozi kote katika taifa la Yuda ili kuifundisha Sheria ya Bwana. Huu pia ni mfano wa jinsi tunavyoweza kuwaongoza wale walio chini ya utawala wetu ili wapate furaha kuu zaidi kwa njia ya kuwashirikisha na kuwaeleza mausia ya Mungu.

Leo, tafuta njia fulani ya kuwa kama Yehoshafatiukitumika, ukifundisha, ukimfurahia Mungu!