2 Nyakati 16

Kitabu cha 2 Nyakati Sura ya 16

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii inazungumzia mabadiliko ya utegemezi alioonesha Mfalme Asa kwa Mungu hapo awali, jambo lililosababisha aletewe taarifa mbaya kupitia nabii Hanani. Pia, 1 Wafalme 15:7-24


 

1 Katika mwaka wa thelathini na sita wa kutawala kwake Asa, Baasha mfalme wa Israeli akapanda juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu ye yote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.

[“Baasha”—mfalme wa Israeli aliyetawala kwa muda wa miaka 20 katikati ya uadui dhidi ya ufalme wa Yuda.]

2 Ndipo Asa akatoa fedha na dhahabu katika hazina za nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, akampelekea Ben-hadadi mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,

3 Kwangu na kwako na liwe agano kama lilivyokuwa kwa baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea fedha na dhahabu; basi, uvunje agano lako na Baasha, mfalme wa Israeli, ili aniondokee mimi.

4 Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawapeleka maakida wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli; wakapiga Iyoni, na Dani, na Abel-maimu, na miji ya hazina yote ya Naftali.

5 Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo, akaacha kuujenga Rama, akaikomesha kazi yake.

6 Ndipo mfalme Asa akawatwaa Yuda wote; nao wakayachukua mawe ya Rama, na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye akajenga kwa vitu hivyo Geba na Mispa.

7 Wakati ule Hanani mwonaji akamwendea Asa mfalme wa Yuda, akamwambia, Kwa kuwa umemtegemea mfalme wa Shamu, wala hukumtegemea Bwana, Mungu wako, kwa hiyo limeokoka jeshi la mfalme wa Shamu mkononi mwako.

[“Hanani mwonaji”—babaye Yehu, nabii (2 Nyakati 19:2 ; 20:34).]_

8 Je! Hao Wakushi na Walubi hawakuwa jeshi kubwa mno, wenye magari na wapanda farasi wengi sana? Lakini, kwa kuwa ulimtegemea Bwana, aliwatia mkononi mwako.

9 Kwa maana macho ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita.

10 Ndipo Asa akamkasirikia mwonaji, akamtia nyumbani mwa mkatale; maana amemghadhibikia kwa sababu ya neno hilo. Na Asa akawaonea baadhi ya watu wakati ule ule.

11 Na tazama, mambo yake Asa, ya kwanza na ya mwisho, angalia, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

12 Akashikwa Asa na ugonjwa wa miguu katika mwaka wa thelathini na kenda wa kumiliki kwake; ugonjwa wake ukazidi sana; lakini hakumtafuta Bwana katika ugonjwa wake, bali waganga.

[Mfalme Asa alishindwa kuamini uwezo wa Mungu katika kuuponya ugonjwa wake. Tofauti naye, mfalme Hezekia alimtegemea Bwana katika ugonjwa wake, akapona (Isaya 38).]

13 Asa akalala na babaze, akafa katika mwaka wa arobaini na mmoja wa kumiliki kwake.

14 Wakamzika katika makaburi yake mwenyewe, aliyojichimbia katika mji wa Daudi, wakamlaza juu ya kitanda kilichojazwa manukato, na kila namna ya machanganyiko ya hao mafundi wa dawa; wakamfukizia mafukizo makuu sana.


UFUPISHO WA 2 NYAKATI 16

Je, utaimaliza safari yako vizuri? Wapo watu wengi wanaoanza vizuri. Tumewaona wakijitokeza mwanzoni mwa safari—Sauli, Sulemani, Rehoboamu, na sasa, Asa. Sauli alikuwa mrefu kabisa kuliko wengine wote. Hakuna mtu yeyote ambaye angeliweza kulinganishwa na Sulemani. Lakini safari ni ndefu kiasi kwamba hata wanariadha bora huchoka.

Asa aliyaondoa macho yake kwa Bwana na akatumia fedha na dhahabu toka kwenye hazina ya Mungu ili kununua msaada wa kijeshi kwa Ben-hadadi wa Shamu. Nabii Hanani akaja kumkumbusha mfalme huyu kuwa ni kosa kumtegemea mwanadamu. Kilichotokea baada ya hapo kinastaajabisha. Mfalme Asa alighadhibika sana kiasi cha kumtupa nabii wa Bwana gerezani. Baadaye, aliposhikwa ugonjwa wa miguu akakataa kutafuta uponyaji wa Bwana, bali aliwaendea waganga. Muda mfupi baadaye akafa.

Kiburi cha kipumbavu sana kiasi hicho ndicho kituzuiacho kutubu! Mungu ni mwenye rehema nyingi, na yuko tayari sana kusamehe. Hakuna dhambi yoyote asiyoweza kuisamehe, isipokuwa ile ya kukataa kumwomba.

“Kwa maana macho ya Bwana huzunguka huku na kule duniani mwote, ili kuwapa nguvu wale walio waaminifu Kwake” (2 Nyakati 16:9, NKJV).

Amka. Anza safari tena. Maliza vizuri. “Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; Bali wasio haki hukwazwa na mabaya.” Mithali 24:16.