2 Nyakati 15

Kitabu cha 2 Nyakati Sura ya 15

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii inazungumzia matengenezo mengine zaidi aliyofanya Mfalme Asa, baada ya kutiwa moyo na nabii wa Mungu. Alimwambia: Bwana yu pamoja nanyi, nanyi jipeni moyo, wala msilegee; kwa maana mtapata tuzo kwa kazi mfanyayo.


 

1 Ndipo roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi;

  • [“Azaria”—jina la nabii huyu humaanisha “Bwana ndiye msaada wangu.”]

2 naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; Bwana yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.

  • [“ tafuteni, nanyi mtaona” (Mathayo 7:7). “Mkaribieni Mungu, Naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.” Yakobo 4:8.]

3 Basi tangu siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati;

  • [“kuhani afundishaye”—jukumu muhimu sana la makuhani wa Biblia lilikuwa kuwafundisha watu Neno la Mungu na sheria Yake (Walawi 10:11; Kumbukumbu 17:9, 11; 24:8; 33:10; Ezra 7:10, 25; Yeremia 18:18; Ezekieli 44:23; Malaki 2:7).]

4 lakini walipomgeukia Bwana, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao.

5 Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi.

6 Wakavunjika-vunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwani Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote.

7 Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara.

8 Naye Asa alipoyasikia maneno hayo, yaani, unabii wa mwana wa Odedi nabii, akatiwa nguvu, akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi ya Yuda na Benyamini, na katika miji aliyoitwaa milimani mwa Efraimu; akaifanyiza tena madhabahu ya Bwana, iliyokuwako mbele ya ukumbi wa Bwana.

9 Akakusanya Yuda wote na Benyamini, na hao wageni waliokaa kwao, wa Efraimu, na wa Manase, na wa Simeoni; kwa kuwa walimwangukia wengi katika Israeli, walipoona kwamba Bwana, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.

  • [Kabila la Simeoni, Yuda pamoja na baadhi ya koo za kabila la Benjamini ziliunda Ufalme wa Kusini uliokuwa ukijulikana kama Yuda.]

10 Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu, katika mwaka wa kumi na tano wa kumiliki kwake Asa.

11 Wakamchinjia Bwana siku ile, katika nyara walizozileta, dhabihu za ng’ombe mia saba, na kondoo elfu saba.

12 Wakafanya agano, ya kuwa watamtafuta Bwana, Mungu wa baba zao, kwa mioyo yao yote, na kwa roho zao zote;

13 na ya kwamba ye yote asiyemtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, atauawa, akiwa mdogo au mkubwa, kwamba ni mwanamume au mwanamke.

14 Wakamwapia Bwana kwa sauti kuu, na kwa kelele, na kwa mapanda, na kwa baragumu.

15 Na Yuda wote wakakifurahia kile kiapo; kwani wameapa kwa moyo wao wote, na kumtafuta kwa mapenzi yao pia; naye ameonekana kwao; naye Bwana akawastarehesha pande zote.

16 Hata na Maaka mamaye Asa, mfalme akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake, akaiponda, akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.

  • [“Maaka mamaye Asa”—bibi yake Mfalme Asa alikuwa mjukuu wake Absalomu. Kupitia ibada yake ya sanamu alijaribu kuzuia matengenezo ya kiroho katika taifa la Yuda. “Ashera” ilikuwa miungu (ya kike) ya Wakanaani iliyoaminiwa kuwa chanzo cha kuleta upendo, uzazi, na vita.]

17 Lakini mahali pa juu hapakuondolewa katika Israeli; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu siku zake zote.

18 Akavileta nyumbani mwa Mungu vitu alivyovitakasa babaye, na vile alivyovitakasa mwenyewe, fedha, na dhahabu, na vyombo.

19 Wala hapakuwa na vita tena hata mwaka wa thelathini na tano wa kutawala kwake Asa.


UFUPISHO WA 2 NYAKATI 15

Baada ya Mungu kumpatia Mfalme Asa ushindi mkuu dhidi ya jeshi kubwa sana la Wakushi, alimtumia ujumbe maalum kupitia nabii Azaria. Ulikuwa umejaa maneno ya kumtia moyo na onyo la upole. “Bwana yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja Naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.” Aya ya 2.

Hata baada ya kuupata ushindi wa hakika kiasi hicho, Mfalme Asa alihitaji kusikia wito wa kusonga mbele. Kulikuwa na mambo mengi zaidi yaliyopaswa kufanywa. Kwa hiyo “alijipa moyo” na kwenda kila mahali akiondoa sanamu. Alirejesha madhabahu ya Mungu. Kinachoshangaza, idadi kubwa sana ya wahamiaji walianza kumiminika toka Israeli (taifa la Kaskazini) kuja katika Ufalme wa Yuda. Wafuasi wa Mungu wa kweli Walitaka wawe na kiongozi ambaye kwa kweli alikuwa na moyo wa kutenda mema.

Sisi vilevile, lazima tukumbuke kuwa uongofu wetu wa zamani na ushindi wetu wa jana havitoshi kutusaidia kwa ajili ya vita vya leo. Kuna sanamu zilizofichika mioyoni mwetu ambazo bado zinapaswa zichunguzwe na kuondolewa kabisa. Huu ndio wakati kwa ajili yetu kuja pamoja toka ulimwenguni kote, tukiungana katika kujitolea kikamilifu ili kumpenda Mungu na kupendana sisi kwa sisi.

“Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na ijara” (2 Nyakati 15:7).