Amri ya Nne

AMRI YA NNE: SIKU YA SABATO

 

Amri hii kwa ufupi inasema (Kutoka 20:8-11)

 • 8 IKUMBUKE SIKU YA SABATO UITAKASE.
 • 9 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote;
 • 10 Lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
 • 11 Maana, kwa siku sita BWANA ALIFANYA MBINGU, NA NCHI, NA BAHARI, NA VYOTE VILIVYOMO, AKASTAREHE SIKU YA SABA; KWA HIYO BWANA AKAIBARIKIA SIKU YA SABATO AKAITAKASA.

 

Sabato ni moja ya Amri zilizoathirika vibaya sana kwa kukanyangwa na kudharauliwa na walimwengu. Wengi wetu tumeitupilia mbali, hatuitambui kabisa wala kuijali na hata tukiambiwa kuwa tumemkosea Mungu kwa kuvunja amri yake hatujali kabisa. Lakini kumbuka, Sheria za Bwana ni “Amri” si “Mapendekezo”.

 1. Mwanzo wa Sabato

Sabato ilianza katika juma la kwanza la uumbaji kabla ya dhambi kuingia (Mwanzo 2:1-3). Kuanzishwa kwake hakuna uhusiano wowote na taifa lolote wala au kuingia kwa dhambi katika jamii ya wanadamu. Aya hizi zinasema Mungu aliibariki siku ya sabato na kuifanya kuwa takatifu.

 1. Sabato: Kumbukumbu ya Uumbaji na Ukombozi

Ezekieli 20:20 “Tena naliwapa sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, Bwana, ndimi niwatakasaye.”Aya hii inasema Sabato ni alama ya mahusiano kati ya Mungu na watu wake. Ni alama maalumu ya kufundishia na kumtambulisha Mungu kama muumbaji na mkombozi wa wanadamu toka dhambini.

 1. Sabato: Yesu Aliitunza Pia

Ilikuwa ni kawaida ya Yesu kutunza sabato.Luka 4:16 “Akaenda Nazareti, …na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, …”

 1. Mitume waliendelea Kutunza Sabato baada ya Yesu Kupaa

Hata baada ya Yesu kuondoka mitume na wakristo wa mataifa yote waliongoka waliendelea kuitunza Sabato kama ilivyokuwa imeamriwa;Matendo 16:13 “Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.”Soma pia Matendo 13;42, 44; 18:4 .

 

 1. Sabato ni Siku Ipi?

  Kuna ushahidi mkubwa unaothibitisha kuwa sabato ni Jumamosi. Ushahidi huu unapatikana katika biblia yenyewe; kamusi, Qurani tukufu, Katekismu ya Waumini, lugha za kale na vitabu mbali mbali vya historia.

 

(5.1) Ushahidi toka katika Biblia

 • Kupitia sikukuu ya pasaka tunajifunza kuwa “Siku hiyo (Yesu alipokufa) ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza… Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria. Jumapili, alfajiri na mapema, wale wanawake walikwenda kaburini … wakalikuta lile jiwe la kaburi limeviringishwa mbali (alikuwa amefufuka)… ” Luka 23: 54 – 24:2 (Kiswahili cha Kisasa)

(5.2) Katekisimu ya Wauumini R.C. (P. Gieremean, 1977, uk. 50)

 • SWALI: Siku ya Sabato ni ipi?
 • JIBU: Jumamosi ni siku ya Sabato

(5.3) Quran Tukufu 2:65; 4:47; 7:163; 16:124

 • Aya zote hizi zinasema sabato ni Jumamosi.

(5.4) Lugha za Kale 

 • Lugha zaidi ya 105 zimeendelea kuiita Jumamosi kwa jina Sabato.
 • Kwa mfano, Kitaliano hiita Sabato, Waarabu hiita Sabt n.k.

Mabadiliko ya Sabato (Kutoka Jumamosi kwenda Jumapili).

 • Danieli 7:25 na Ufunuo 13 kulitabiriwa kuinuka kwa mamlaka ya kidini ambayo ingebadili Sabato ya Mungu na kuipeleka siku nyingine.
 • Unabii huu unasema kuwa mamlaka hii ingewaongoza wengi wengi sana katika mabadiliko hayo yasiyo sahihi. Maandiko yameyaita mabadiliko haya kuwa ni ukengeufu na uasi (mabadiliko haya hatutayatafakari katika mada hii, lakini ukitaka ufahamu wa kina juu ya hili wasiliana na aliyekutumia somo hili).
 • Yesu pia alionya sana juu ya kuacha sheria ya Mungu na kufuata mafundisho ya wanadamu akisema: “Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.” Mathayo 15:8, 9.
 • Ni jambo la hatari sana kuacha amri ya Mungu na kufuata mafundisho ya wanadamu.
 • Kulingana na maandiko, Mungu anaitambua Jumamosi kama sabato yake takatifu na anaita siku zingine zilizofanywa kuwa sabato na wanadamu kuwa ni uasi na kwamba kufuata siku hizo ni kujidanganya kiakili na kufanya ibada ya bure.

HITIMISHO

 • Sabato ni siku ya Mungu, iliyowekwa wakfu kwa ajili ya ibada, na kukumbuka asili yetu na vitu vyote vinavyotuzunguka. Mungu amewaamuru watu wote kusimamisha kazi zao zote kama yeye mwenyewe alivyofanya, akaibariki na kuitenga rasmi kuwa siku takatifu – ni AMRI.

Mungu akubariki sana unapotafakari somo hili.