“WANAHITAJIKA WATU IMARA ZAIDI”

🌺 “WANAHITAJIKA WATU IMARA ZAIDI” 🌺

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Asante kwa kutupenda na kutusamehe dhambi zetu. Tunaalika uwepo Wako katika tafakari ya asubuhi ya leo. Tusaidie kulifahamu Neno Lako, tubadilishe ili tufanane Nawe, na pia tupatie uwezo wa kuyatenda mapenzi Yako. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

  • “Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika Mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata” (Kutoka 32:1).

Musa alipokuwa hayupo, Haruni alikabidhiwa mamlaka ya kisheria na umati mkubwa wa watu ukakusanyika hemani pake ukidai, “katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu…”

Ili kuikabili zahama ya namna hiyo, alihitajika mtu thabiti, mwenye uamuzi na ujasiri usioyumba, mtu ambaye alichukulia heshima ya Mungu katika hali ya juu kuliko mapenzi ya wengi, usalama binafsi na hata uhai wenyewe.

Kwa unyonge, Haruni alipingana na watu hao, lakini hali yake ya kutokuwa imara na hofu katika wakati huo makini, viliwafanya wawe jasiri zaidi katika uovu wao. Ghasia iliongezeka. Haruni alihofia usalama wake; na badala ya kusimama kiuadilifu kwa ajili ya kumheshimu Mungu, akakubaliana na matakwa ya umati wa watu.

Kitendo chake cha kwanza kilikuwa ni kuelekeza kwamba hereni zao za dhahabu zikusanywe kutoka kwa watu wote ziletwe kwake, akitegemea kwamba ufahari ungewafanya wakatae kujitoa kiasi hicho. Lakini kwa hiari kabisa walikabidhi mapambo yao; na kutokana na haya akatengeneza sanamu ya ndama aliyetokana na vito hivyo vilivyoyeyushwa, mfano wa miungu ya Misri.

Huwa tunarudia dhambi ya Haruni, tukikaa kimya, wakati ambapo uwezo wetu wa kuona ungepaswa kuwa wazi kutambua uovu na kusema wazi kabisa, hata kama kufanya hivyo kunatuweka katika hali isiyo nzuri, kwa sababu makusudi yetu yanaweza yasieleweke vizuri. _Haitupasi kuuvumilia ubaya ambao upo ndani ya ndugu au mtu yeyote ambaye tunahusiana naye.-

Hali hii ya kupuuza kusimama imara kwa ajili ya kweli ndiyo iliyokuwa dhambi ya Haruni. Angesema ukweli waziwazi, ndama huyo wa dhahabu asingetengenezwa. Bado wapo akina Haruni ambao ni wepesi kushawishika, ambao huwa wanakubali tamaa za watu wasio safi na kwa namna hiyo wanawatia moyo na kuwahamasisha kuenenda katika dhambi.

Wale ambao wamepewa heshima ya utume wa Mungu, hawapaswi wawe wanyonge wala kuyaepuka majukumu yasiyopendwa, bali wafanye kazi ya Mungu kwa uaminifu usioyumba.


. 🔭📝.
. “Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
. (Maombolezo 3:22, 23).