“KUSIMAMA IMARA LICHA YA DHIHAKA NA DHARAU”

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Asante kwa kutupenda na kutusamehe dhambi zetu. Tunaalika uwepo Wako katika tafakari ya asubuhi ya leo. Tusaidie kulifahamu Neno Lako, tubadilishe ili tufanane Nawe, na pia tupatie uwezo wa kuyatenda mapenzi Yako. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

“Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha” (Zaburi 1:1).

Waovu ni wale ambao hawapendi wala hawatii amri za Mungu, bali wanakwenda kinyume nazo. Hili ndilo kundi la washauri unaoonywa ufanye kila liwezekanalo ili kuwaepuka kabisa,—kundi analolitumia Shetani ili kuwapotosha vijana. Ushauri wao, mapendekezo yao, yana sifa ile ya kuhafifisha ubaya wa dhambi, kudhihaki uadilifu. Wanadhihirishwa kuwa kama watu wanaosimama njiani pa wenye dhambi, daima wakiwaongoza wengine watoke kwenye njia nyofu ya wajibu na utii wa amri za Mungu na kuingia katika njia ya uasi.

Wasingekuwepo hawa watendao mabaya na ambao huwajaribu wengine kutenda mabaya, wadhambi wengi wangeichagua njia ya kutenda wajibu wao, na kuishi maisha ya usafi ma ucha Mungu. Hofu ya kudhihakiwa huwafanya vijana wengi wajisalimishe kwenye jaribu na kutembea katika njia ya uovu. Kamwe Yesu hakujiweka mwenyewe katika hatari ili kumpendeza yule mwovu. Lakini ni wangapi leo wanaoweza kusimama na kudiriki kufanya hivyo kama Kristo?

Usiruhusu dhihaka, wala vitisho, wala kauli za dharau, zikushawishi kwenda kinyume na dhamiri yako hata katika jambo dogo kabisa, kwani kwa kufanya hivyo utafungua mlango ambao Shetani anaweza kuingilia na kuitawala akili yako. Lazima uwe mwanafunzi anayependa kujifunza Biblia. Neno Lake ni mwongozo thabiti; kama likisomwa kwa uangalifu, hakutakuwa na hatari ya kuangushwa na nguvu ya majaribu ambayo huwazunguka vijana, na kuwashambuliwa kwa wingi.

Baadhi wanaweza kukudhihaki kwa kuwa makini sana; wanaweza kukuita kwamba u mtu mwenye kujidai kuwa mtakatifu na mwenye haki; lakini uwe mwangalifu kuenenda kwa usahihi, na kisha uendelee kwa utulivu. Endapo kisa chote cha Danieli kingeandikwa, historia yake hiyo ingebainisha majaribu ambayo alipaswa kukabiliana nayo, pamoja na dhihaka, wivu na chuki; lakini aliinuka juu zaidi na kushinda dhihaka; na ndivyo itakavyokuwa kwa kila mmoja aliye mshindi.


  • 🔭📝
  • “Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
  • (Maombolezo 3:22, 23).