2 Nyakati 11

Usomaji wa Biblia kwa Mpango

  • Kitabu cha 2 Nyakati Sura ya 11

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii huelezea jinsi Rehoboamu, mfalme wa Kusini (Yuda) anavyojiimarisha dhidi ya ufalme ule wa Kaskazini (Israeli) uliomeguka kutoka kwake; anajaribu kutumia karibu kila mbinu ya kibinadamu ili kuuweka utawala wake katika usalama.


 

1 Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na Benyamini, watu wateule mia na themanini elfu waliokuwa hodari, watu wa vita, ili wapigane juu ya Israeli, ili wamrudishie Rehoboamu huo ufalme.

  • [“Benjamini”—ingawa mfalme Sauli alikuwa wa kabila la Benjamini, familia nyinyi kutoka katika kabila lake hili zinaendelea kubaki katika utawala wa Kusini (Yuda).]

2 Lakini neno la Bwana likamjia Shemaya mtu wa Mungu, kusema,

3 Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, uwaambie na Israeli wote waliomo Yuda na Benyamini, ukisema,

4 Bwana asema hivi, Hamtapanda wala kupigana na ndugu zenu; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi, wakayasikiliza maneno ya Bwana, wakarudi katika kumwendea Yeroboamu.

Miji ya Ngome ya Yeroboamu:

5 Naye Rehoboamu akakaa Yerusalemu, akajenga miji yenye ngome katika Yuda.

6 Akajenga na Bethlehemu, na Etamu, na Tekoa,

7 na Bethsuri, na Soko, na Adulamu,

8 na Gathi, na Maresha, na Zifu,

9 na Adoraimu, na Lakishi, na Azeka,

10 na Sora, na Aiyaloni, na Hebroni, iliyoko katika Yuda na Benyamini, miji yenye maboma.

  • [“Hebroni”—mji muhimu sana unaopatikana katikati mwa Yuda ambako wazee wa imani walizikiwa, na ambako Daudi alitawala kwa muda wa miaka 7.]

11 Akazifanya imara hizo ngome, akaweka majemadari humo, na akiba ya vyakula, na mafuta, na mvinyo.

12 Na ndani ya miji yote mmoja mmoja aliweka ngao na mikuki, akaifanya kuwa na nguvu nyingi mno. Yuda na Benyamini ikawa milki yake.

Makuhani na Walawi Wahamia Yuda (1 Wafalme 14:21-24):

13 Wakamwendea makuhani na Walawi waliokuwa katika Israeli yote, kutoka mpaka wao wote.

  • [“Walawi”—walikuwa wahudumu Hekaluni na walihamia Yuda kwa sababu walikataa kushiriki katika ibada ya sanamu iliyoingizwa na mfalme Yeroboamu.]

14 Kwani Walawi wakaacha malisho yao, na milki yao, wakaja Yuda na Yerusalemu; kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwatupa, ili wasimfanyie Bwana ukuhani;

15 naye akajiwekea makuhani wa mahali pa juu, na wa wale majini, na wa zile ndama alizozifanya.

  • [“majini”—lugha ya asili ya Kiebrania inasema “sanamu za mbuzi.” Sanamu moja iliwekwa kwenye mji wa Betheli (kusini), wakati nyingine ikiwekwa katika mji wa Dani (kaskazini), 1 Wafalme 12:29.]

16 Na kutoka katika kabila zote za Israeli, wakaandamwa na hao waliojikaza nia kumtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, wakaja Yerusalemu, ili wamtolee dhabihu Bwana, Mungu wa baba zao.

17 Hivyo wakaufanya imara kwa miaka mitatu ufalme wa Yuda, na kumtia nguvu Rehoboamu mwana wa Sulemani; kwa maana muda wa miaka mitatu wakaiendea njia ya Daudi na Sulemani.

Familia ya Rehoboamu:

18 Rehoboamu akaoa mke, Mahalathi binti Yerimothi mwana wa Daudi, na wa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese;

19 akamzalia wana, Yeushi, na Shemaria, na Zahamu.

20 Kisha baada yake akamwoa Maaka, binti Absalomu; na yeye akamzalia Abiya, na Atai, na Ziza, na Shelomithi.

21 Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wote na masuria yake; (maana alioa wake kumi na wanane, na masuria sitini, akazaa wana ishirini na wanane na binti sitini).

22 Rehoboamu akamsimamisha Abiya, mwana wa Maaka, kuwa mkuu, mtawala kati ya nduguze, kwa kuwa aliazimia kumtawaza awe mfalme.

23 Akafanya kwa akili, akawatawanya wanawe wote kati ya nchi zote za Yuda na Benyamini, katika kila mji wenye boma; akawapa vyakula tele. Akawatafutia wake wengi.


UFUPISHO WA 2 NYAKATI 11

Mfalme Yeroboamu aliwafunza na kuwaandaa watu wa aina mbalimbali kuwa makuhani baada ya kuanzisha ibada ya sanamu ya ndama na ibada ya mashetani. Makuhani, Walawi, na wengine walikataa kushiriki kwa namna yoyote ile katika jambo hili. Katika kipindi kilichofuatia cha miaka 3 walihama toka Israeli kuja Yuda. Tukio hili muhimu la kuhama kwa viongozi hawa wa kiroho kwa kiwango kikubwa liliimarisha ufalme wa Yuda na kuharakisha uangamivu uliofuata wa taifa la Israeli (kaskazini).

Leo hii adui huyohuyo yuko kazini akitafuta kuwadhoofisha watu wa Mungu. Anatenda kazi kupitia aina mbalimbali za ibada ya sanamu, akitumia chochote kile awezacho ili kujitwalia muda bora wa watu wa Mungu na kuondoa usikivu wao toka kwa Mungu wao mwenye upendo.

Je, ni misukumo gani iliyopo katika maisha yako? Ni mambo gani yanayominya muda wako na kuhafifisha upendo wako kwa Bwana? Wewe, vilevile, unaweza kuhamia mahali salama kiroho—huenda ni kuwa mbali na kompyuta yako au simu yako kwa muda wa siku moja ukimtafuta Mungu. Pengine hilo likamaanisha tendo la dhati na la kuthubutu la kuihamisha familia yako kwenda katika mahali pengine papya ambako muda wa kufanya ushirika na Mungu au fursa za kumtumikia hupatikana kwa kiwango kikubwa. Chukua hatua leo. Jiimarishe. Imarisha familia yako. Imarisha na kudumisha Ufalme wa Mungu. “Basi sasa mcheni Bwana, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na uaminifu;… chagueni hivi leo mtakayemtumikia” (Yoshua 24:14, 15).