2 Nyakati 9

 “Usomaji wa Biblia kwa Mpango”

Kitabu cha 2 Nyakati Sura ya 9

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii huelezea utukufu na mafanikio ya Sulemani yaliyofikia kiwango cha kimataifa. Sura hii hulandana na 1 Wafalme 10 na 11.

Malkia wa Sheba Ashangazwa na Utukufu wa Sulemani (1 Wafalme 10:1-13)
1 Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.

[“Sheba”—ufalme wa zamani wa Seba uliopatikana kusini magharibi mwa peninsula (rasi) ya Arabia (Mwanzo 10:28).)

2 Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie.

3 Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga,

4 na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana; roho yake ilizimia.

5 Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.

6 Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.

7 Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.

8 Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake Bwana, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.

[“Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako”—baraka hizi za malkia wa Sheba hutukumbusha juu ya zile alizotamka mfalme Hiramu wa Tiro katika 2 Nyakati 2:11. Hiramu alikuwa mfalme wa nchi ya kaskazini, wakati malkia wa Sheba alitokea kusini. Baraka hizi mbili huwakilisha utambuzi wa ulimwengu mzima juu ya ukuu wa Mungu wa Sulemani.]

9 Basi akampa mfalme talanta mia na ishirini za dhahabu, na manukato mengi mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja wingi wa manukato, kama hayo aliyopewa mfalme Sulemani na malkia wa Sheba.

[“talanta mia na ishirini za dhahabu” = tani 4]

10 Tena watumishi wa Hiramu, pamoja na watumishi wa Sulemani, walioleta dhahabu kutoka Ofiri, wakaleta miti ya msandali, na vito vya thamani.

11 Mfalme akayafanya kwa miti hiyo ya msandali madari ya nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haijatokea kama hiyo katika nchi ya Yuda.

12 Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya vile alivyomletea mfalme. Basi akarudi, akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.

Utajiri Mkuu wa Sulemani (1 Wafalme 10:14-29; 2 Nyakati 1:14-17):
13 Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita za dhahabu;

[“talanta mia sita sitini na sita za dhahabu” = kadiri ya tani 23. Matumizi ya nadra ya tarakimu 666. Maana yake hapa ni halisi, tofauti na ile inayopatikana katika Ufunuo 13:18 ambayo ni alama au “hesabu ya kibinadamu” ya “mnyama yule.”]

14 mbali na ile waliyoileta wachuuzi na wafanya biashara; tena wafalme wote wa Arabuni, na maliwali wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.

[“Arabia”—eneo linalopatikana kusini mashariki mwa Palestina ambako watu wa uzao wa Ishaeli mwana wa Ibrahimu waliishi.]

15 Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; ngao moja hupata shekeli mia sita za dhahabu iliyofuliwa.

[“shekeli mia sita za dhahabu” = kilo 7]

16 Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kigao kimoja hupata shekeli mia tatu za dhahabu; mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni.

[“shekeli mia tatu za dhahabu” = kilo 3.5. “nyumba ya mwitu wa Lebanoni”—jengo hili lilipewa jina hili kwa sababu safu zake za nguzo za mierezi zilikuwa na mwonekano wa msitu mkubwa.]

17 Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi.

18 Kiti kile kilikuwa na daraja sita, tena na kikao cha miguu cha dhahabu, navyo vilikuwa vimeshikamana na kiti; na mikono huko na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.

19 Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya daraja sita, huko na huko; wala hakikufanyika kwa mfano wake katika ufalme wo wote.

[“simba kumi na wawili”—wakiwakilisha nguvu na umoja wa makabila 12 ya Israeli.]

20 Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.

21 Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu zilizokwenda Tarshishi pamoja na watumishi wa Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.

22 Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.

23 Wafalme wote wa duniani wakamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.

24 Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka.

25 Sulemani akawa na mazizi ya farasi na magari elfu nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.

26 Akatawala juu ya wafalme wote toka Mto hata nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri.

[Mto Frati ni mojawapo wa mipaka ya asili ya nchi ambayo Mungu aliwaahidi wazee wa imani. “Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati” (Mwanzo 15:18). “Na awe na enzi toka bahari hata bahari, Toka Mto hata miisho ya dunia.” Zaburi 72:8.]

27 Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifanya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.

28 Wakamletea Sulemani farasi kutoka Misri, na kutoka nchi zote.

29 Basi mambo yake Sulemani yaliyosalia, ya kwanza, na ya mwisho, je! Hayakuandikwa katika tarehe ya Nathani nabii, katika unabii wa Ahiya, Mshiloni, na katika maono ya Ido mwonaji juu ya Yeroboamu mwana wa Nebati?

[“Ahiya, Mshiloni”—nabii aliyetabiri mtenguko na kusambaratika kwa ufalme wa Sulemani (1 Wafalme 11:29-30).]

30 Akatawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote miaka arobaini.

[“miaka arobaini”—Daudi, babaye Sulemani, pia alitawala kwa muda wa miaka 40.]

31 Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa mjini mwa Daudi babaye; akatawala Rehoboamu mwanawe badala yake.


UFUPISHO WA 2 NYAKATI 9

Malkia wa Sheba alivutiwa sana katika ziara yake kwa Mfalme Sulemani, hasa kutokana na hekima aliyoiona kwake na mwonekano wa kustaajabisha wa Nyumba ya Bwana. Sulemani alipomweleza alivutiwa na maajabu hayo kiasi kwamba alisema, “Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako!” Heshima haikumwendea Sulemani, bali Mungu Mwenyewe.

Je, hali ingekuwaje endapo Sulemani angechagua kuendelea kuwa mnyenyekevu? Ni mataifa mangapi yangeweza kufikia hatua ya kumfahamu Mungu wa kweli? Badala yake, alienenda kinyume kabisa na maagizo dhahiri ya Mungu aliyowaamuru wafalme kwamba wasijilimbikizie mali na hazina nyingi kupita kiasi.

Katika utelezi huu wa Sulemani kutoka kwa Mungu uliofanyika taratibu lakini kwa hakika, hutujia onyo sisi sote: haiwezekani kabisa kumpenda Mungu na mali kwa wakati mmoja (Mathayo 6:24).

“Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”  1 Timotheo 6:10.

Unakuja wakati ambapo hatutaweza kuuza wala kununua kama tunataka kumwabudu Mungu wa kweli kwa kuitunza Sabato Yake aliyoiamuru (Ufunuo 13:16, 17).

Mara kwa mara tunaghubikwa na kushambuliwa na matangazo yanayokuza shauku yetu juu ya kitu fulani tusichokuwa nacho. Mara nyingi huwa tunatumia fedha nyingi kununulia vitu tusivyohitaji wakati ambapo ndugu na dada zetu ulimwenguni wanakufa kwa kukosa chakula, fursa ya elimu, matunzo ya kiafya na nuru ya uzima wa milele.
Je, utafanya nini leo ili kuwabariki wengine, badala ya wewe mwenyewe? “Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana; Naye atamlipa kwa tendo lake jema.” Mithali 19:17.

Scott Griswold: Mratibu wa Utume, ASAP Ministries.
___
. 🔭📝.
. “Waaminini Manabii Wake”
. (2 Mambo ya Nyakati 20:20).