Yakobo 1:6

“HATARI YA KUWA NA MASHAKA” 

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Asante kwa kutupenda na kutusamehe dhambi zetu. Tunaalika uwepo Wako katika tafakari ya asubuhi ya leo. Tusaidie kulifahamu Neno Lako, tubadilishe ili tufanane Nawe, na pia tupatie uwezo wa kuyatenda mapenzi Yako. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

“Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yoyote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku” (Yakobo 1:6).

Baadhi ya watu hawana uthabiti katika tabia. Wako kama bonge la gundi na wanaweza kuminywa na kuwa katika umbo lolote linaloweza kufikirika. Lazima hali hii ya unyonge, kutokuwa na uamuzi na kutokuwa na ufanisi idhibitiwe. Kuna hali ya kutokata tamaa na kutoshindwa kuhusiana na tabia ya kweli ya Kikristo ambayo haiwezi kubadilishwa au kutiishwa na mazingira yoyote magumu na yasiyofaa. Lazima watu wawe na uthabiti wa kimaadili, uadilifu ambao hauwezi kughilibiwa (hadaa), kushawishika wala kuogopeshwa.

Tunaye adui mwenye nguvu. Watu wanapokubali kuwa watumwa wa Shetani, haoneshi uadui juu yao kama anavyowafanyia wale wanaolikiri Jina la Kristo na kujitolea ili kumtumikia Mungu. Anawachukia kwa ghadhabu kali ya kutisha. Anajua kwamba anaweza kumhuzunisha Yesu kwa kuwaweka chini ya nguvu ya udanganyifu wake, kwa kuwajeruhi, kwa kudhoofisha imani yao.

Shetani atawaruhusu wale ambao wamefungwa kama watumwa kwenye gari lake wawe na kiwango fulani cha pumziko, kwani wao ni mateka wake ambao wamekubali kwa hiari yao wenyewe; lakini uadui wake huamshwa na kuchochowa wakati ujumbe wa rehema unawapofikia watumwa wake waliofungwa, na wanapotafuta wakijikwapua kutoka mikononi mwake, ili waweze kumfuata yule Mchungaji wa kweli. Pambano kati ya roho na Shetani huanza wakati mateka anapoanza kujinasua kwa nguvu kutoka kwenye mnyororo, na akifanya jitihada za kuwa huru.

Wale ambao wanatamani kweli kufundishwa na Mungu na kutembea katika njia Yake, wanayo ahadi thabiti, kwamba ikiwa watajisikia kuwa wahitaji wa hekima na wakamwomba Mungu, Yeye atawapatia kwa ukarimu, na bila kuwashutumu. Mtume anasema, “na aombe kwa imani, pasipo shaka yoyote.” Amini; amini kwamba Mungu atatenda kile hasa ambacho ameahidi. Endelea kupeleka dua zako juu, huku ukikesha, na kufanya kazi na kungoja. Piga vita vizuri vya imani.

Kadiri tunavyoendelea kusafiri kwa kuufuata mkondo wa ulimwengu, hatuhitaji tanga wala kasia. Lakini ni pale tunapogeuka kabisa ili kuuzuia mkondo huo ndipo kazi yetu inapoanza.
. 🔭📝.
. “Rehema za Bwana ni mpya kila siku asubuhi.”
. (Maombolezo 3:22, 23).