2 Nyakati 10

“Usomaji wa Biblia kwa Mpango”

  • Kitabu cha 2 Nyakati Sura ya 10

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana na kukutukuza kwa namna ya pekee kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Tunaalika uwepo Wako katika Mfululizo wa Usomaji wa Biblia kwa Mpango. Tunaomba Roho Mtakatifu, katika tafakari ya somo hili, atukirimie hekima ya utambuzi wa sauti Yako na nguvu ya kuitii. Tusaidie kufanya uamuzi wa busara, kila wakati, tukikuchagua Wewe na kuuchagua wokovu. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tubadilishe ili tufanane Nawe. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

UTANGULIZI: Sura hii huelezea juu ya kusimikwa kwa Rehoboamu kuwa mfalme na pia kugawanyika kwa taifa la Israeli.]


 

 

1 Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekuja Shekemu, ili wamfanye mfalme.

[“Rehoboamu”—mwana wa Sulemani na mrithi wa ufalme baada ya babaye. Kukosa kwake hekima kulisababisha kugawanyika kwa taifa la Israeli.]

2 Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia, (maana alikuwako Misri, ambako amekimbilia mbele ya mfalme Sulemani), Yeroboamu akarudi kutoka Misri.

3 Wakapeleka ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,

4 Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.

5 Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao.

6 Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa?

7 Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote.

8 Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, waliosimama mbele yake.

9 Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, Utufanyie jepesi kongwa alilotutwika baba yako.

10 Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.

11 Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu akiwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge.

12 Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu.

13 Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana,

14 akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge.

15 Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Mungu, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni.

[“ Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi, (lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli); kwa sababu wameniacha mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba yake.1 Wafalme 11:29-33.]

16 Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hawasikilizi, watu wakamjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli, kila mtu; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Daudi. Basi wakaenda zao Israeli wote hemani kwao.

17 Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu alitawala juu yao.

[“miji ya Yuda”—makabila ya Yuda na Simeoni pamoja na baadhi ya wazawa wa kabila la Benjamini walidumu kuwa waaminifu kwa ufalme wa Daudi na warithi wake waliomfuatia.]

18 Ndipo mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, msimamizi wa shokoa; nao wana wa Israeli wakamtupia mawe, hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda garini mwake, ili akimbilie Yerusalemu.

19 Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi, hata leo.


UFUPISHO WA 2 NYAKATI 10

Mfalme Rehoboamu alikuwa na “vitabu vitatu vya kujifunzia” stadi za uongozi bora: maisha ya kushangaza ya Sauli, Daudi na Sulemani. Pengine hakutumia muda wa kutosha kujifunza kutokana na makosa yao au mafanikio yao. Badala yake, aliwasikiliza vijana wa rika lake. Alitangaza kuwa angewalundikia kodi nyingi zaidi na kwamba serikali yake ingeendeshwa kwa mijeledi yenye miiba. Angetawala badala ya kutumika.

Mara moja ufalme wa Israeli ukagawanyika na kutoweka kwake, kama vile hasa ambavyo Mungu alikuwa ametabiri. Makabila ya Yuda na Benjamini ndiyo pekee yaliyobaki.

Mfalme Yesu ametuita mimi na wewe katika kazi Yake yenye aina fulani maalum ya uongozi. Naye anatuelekeza kwamba: “Mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu” (Marko 10:43). “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi Yake iwe fidia ya wengi” (aya ya 45).

Ukiwa kama baba, utaamuru tu au utawaelekeza watoto wako kwa upendo na kwa kuwasaidia? Je, wewe ni kiongozi wa kanisa na katika wadhifa wako unatafuta kiuhalisia kufanikisha hitaji bora la kila mmoja wenu kama washiriki? Hali ikoje katika sehemu za kazi? Je, kanuni za utumishi na kuimarishana zinachukua nafasi ya juu zaidi kuliko shauku yoyote ya kupata faida na mafanikio? Kitu kingine chochote zaidi ya hayo kitabomoa na kuondoa kabisa sehemu yako katika Ufalme wa Mungu.


 

  • Scott Griswold: Mratibu wa Utume, ASAP Ministries.🔭📝
  •  “Waaminini Manabii Wake”
  • (2 Mambo ya Nyakati 20:20).