Zaburi 104:24

AFYA NA FURAHA INAYOPATIKANA NJE

“Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo Yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali Zako” (Zaburi 104:24).

Kutokana na maisha ya kuwa nje ya nyumba, watu, wanaume kwa wanawake watapata shauku ya kuwa safi na kutokuwa na mawaa. Kwa mvuto unaotokana na sifa zilizo ndani ya rasilimali tiba kuu zitokanazo na mazingirasili ambazo huhuisha, huamsha na kujenga uhai, kazi za mwili zinaimarishwa, akili inaamshwa, fikra hupewa uhai, roho huchangamshwa. Akili inakuwa imeandaliwa kuthamini uzuri wa Neno la Mungu.

Kwa sababu hii, kazi ya kuilima ardhi ni nzuri kwa watoto na vijana. Hii inawafikisha moja kwa moja hadi kwenye mazingirasili na Mungu wa viumbe hivyo. Kwa mtoto au kijana mwenye wasiwasi hilo ni la thamani kabisa. Kuna afya na furaha kwa ajili yake kwenye mafunzo ya viumbeasili; miguso itakayofanywa na zoezi hilo haitafifia akilini mwake, kwani itahusishwa na vile vitu ambavyo vinaendelea kuwepo machoni pake.

Katika ulimwengu wa asili, Mungu ameweka mikononi mwa watu ufunguo kwa ajili ya kufungulia nyumba ya hazina ya Neno Lake. Yasiyoonekana yanaoneshwa katika vielelezo vya vile vinavyoonekana; hekima ya Mungu, ukweli wa milele, neema isiyo na mwisho, vinaeleweka kutokana na vitu ambavyo Mungu amevifanya… Mungu ameufanya ulimwengu huu vizuri kwa sababu anapendezwa na furaha yetu.

Ili watoto na vijana wapate afya, uchangamfu, ucheshi na misuli na akili zilizokuzwa vizuri, sharti wawe nje mahali pa wazi muda mwingi, na wawe na shughuli yenye utaratibu mzuri na burudani nzuri. Furaha ya kweli haipatikani kwa kuendekeza kiburi na starehe, bali katika kuwasiliana na Mungu kupitia uumbaji Wake wa asili.