KAZI HULETA AFYA NA FURAHA

KAZI HULETA AFYA NA FURAHA

“Bwana, Mungu wako, atakubarikia katika maongeo yako yote, na katika kazi zote za mikono yako, nawe uwe katika kufurahi kabisa” (Kumbukumbu la Torati 16:15).

Kukamilishwa kwa uaminifu kwa majukumu ya nyumbani, kuchukua nafasi unayoweza kuijaza kwa manufaa kabisa, iwe ni sahili na duni sana, ni jambo linaloleta ukuaji wa kweli. Mvuto huu wa mbinguni unahitajika. Katika huu kunakuwa na amani na furaha takatifu. Huu una uwezo wa uponyaji. Mvuto huu utapoza, kwa siri tena na bila kujua, makovu ya roho na hata mateso ya mwili. Amani ya akili, ambayo huwa inakuja kutokana na makusudi na matendo yaliyo safi na matakatifu, italeta chemchemi yenye nguvu na huru kwa viungo vyote vya mwili. Amani iliyo ndani pamoja na dhamiri isiyo na kosa kwa Mungu, vitahuisha na kutia nguvu akili, kama vile umande unavyotona kwenye mmea laini. Ndipo nia inapoelekezwa kwa usahihi na kudhibitiwa na inakuwa thabiti zaidi huku ikiwa bila ukaidi. Tafakari zinakuwa za kupendeza kwa sababu zimetakaswa. Amani ya akili ambayo unaweza kuwa nayo, itawabariki wale wote unaohusiana nao… Kadiri unavyoendelea kuonja amani hii ya kimbingu na utulivu wa mawazo, ndivyo itakavyoongezeka. Hii ni raha iliyo hai, ambayo haitupi nguvu zote za kimaadili kwenye ulegevu, bali inaziamsha na kuzifanya zishughulike zaidi. Amani kamilifu ni tabia ya mbinguni ambayo malaika wanayo.

Kamwe watoto na vijana hawatajisikia kuwa na amani ya kuridhika hadi pale ambapo kwa kutekeleza kwa uaminifu majukumu ya nyumbani watapumzisha mikono iliyochoka na moyo na ubongo wenye uchovu wa mama… Wale ambao wanadharau kuchukua sehemu ya majukumu ya nyumbani ndiyo ambao wanafadhaishwa na upweke na kutoridhika; kwani hawajajifunza kuwa watu wenye furaha, wanayo furaha kwa sababu wanashiriki utaratibu wa kila siku wa kazi.

Kazi iliyoelekezwa vyema ndilo hitaji hasa la watoto ili wawe na nguvu, wenye juhudi, wachangamfu, wenye furaha na wenye ujasiri wa kukutana na majaribu mbalimbali ambayo yanaletwa na maisha haya.